Fidelis Butahe na Suleiman Msuya
HALI si
shwari CUF. Huo ndio ukweli kutokana na Baraza la Uongozi kueleza vifungu vya Katiba
ya Chama hicho ilivyotumika kumfukuza uanachama Profesa Ibrahim Lipumba ambaye
naye ametaja vifungu vyake, kupinga uamuzi huo.
Msuguano
huo umewaacha wafuasi wa chama hicho njia panda, huku wanaounga mkono pande
hizo mbili zinazovutana wakibaki njiapanda bila kujua hatima ya chama hicho.
Wakati hayo
yakiibuka ndani ya chama hicho, wanasheria waliozungumza na JAMBO LEO walimtaka
mtaalamu huyo wa uchumi kwenda mahakamani kama anaona hakutendewa haki na chama
chake.
Walisema
kuendelea kwake kusimamia ushauri wa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi
aliyemtambua kuwa Mwenyekiti halali wa CUF, hakuwezi kumpa uhakika wa kurejea
kwenye wadhifa wake.
Mkanganyiko
Baraza Kuu
la chama hicho lililokutana juzi Zanzibar, lilisema limemfukuza Profesa huyo
uanachama na si uongozi, kwa sababu aliandika barua ya kujiuzulu na tayari
wajumbe wa Mkutano Mkuu wa chama hicho walisharidhia uamuzi wake.
Profesa
Lipumba ambaye aliandika barua ya kujiuzulu uenyekiti Agosti 5 mwaka jana,
kabla ya Juni kuandika nyingine ya kutengua na kusisitiza kuwa yeye ni
Mwenyekiti halali, alitumia kifungu cha 83 (1) ya Katiba ya chama hicho, kuwa Baraza
la Uongozi lina uwezo wa kuwasimamisha uanachama Katibu Mkuu, Mwenyekiti wa
Taifa na Makamu wake na si kuwafukuza uanachama.
Hata hivyo,
katika maelezo yake, Baraza Kuu lilisema limemfukuza kama mwanachama wa kawaida
kwa mujibu wa kifungu cha 10 (c) kinachosema: “Atafukuzwa au kuachishwa
uanachama na Mkutano Mkuu wa Taifa au Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kwa mujibu
wa masharti ya Katiba hii”.
Katika hoja
ya Profesa huyo kuwa barua yake ya kujiuzulu haikujibiwa, Baraza Kuu lilisema
angeweza kuhoji kutojibiwa barua hiyo au kuandika barua ya malalamiko, huku
ikitumia kifungu cha 108 (5).
Kifungu
hicho kinasema: “Mwanachama au kiongozi yeyote aliyeamua kukata rufaa kwa jambo
lolote lile, atafanya hivyo kwa ngazi iliyo juu ya kikao kilichotoa uamuzi
ambao hakuridhika nao katika kipindi kisichozidi siku 14 tangu siku uliotolewa
uamuzi huo”.
Wakati
Profesa Lipumba akishikilia msimamo wake wa kuwa Mwenyekiti halali, CUF imebainisha
kuwa alitamka kuwa kuanzia wakati akitoa barua ya kujiuzulu, alitamka kuwa hatakuwa
kiongozi tena na atabaki kuwa mwanachama wa kawaida, tayari vikao vya Baraza
Kuu vilishakaa mara tatu na hakuhudhuria vikao hivyo, jambo ambalo lilimpotezea
sifa.
Chama hicho
kilinukuu Ibara ya 117 (2): “Kiongozi atajiuzulu kwa kuandika barua na kuweka
saini yake kwa Katibu wa Mamlaka iliyomchagua au kumteua, na kiongozi huyo
atahesabiwa kuwa amejiuzulu ikifika tarehe aliyoainisha katika barua yake kuwa
atajiuzulu pindi akikubaliwa na Mamlaka iliyomchagua au iliyomteua.
“Au kama
hakuanisha tarehe ya kujiuzulu kwake, basi atahesabiwa amejiuzulu baada ya
Katibu wa Mamlaka iliyomteua au kumchagua, kupokea barua hiyo na Mamlaka
iliyomchagua au kumteua kukubali”.
Wanasheria
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Kitivo
cha Sheria, Dk Onesmo Kyauke alisema kilichobaki sasa ni msomi huyo kwenda
mahakamani ili kudai haki yake.
Dk Kyauke
alisema iwapo aliitwa kwenda kujitetea mbele ya Baraza hilo na hakwenda basi
hawezi kuwa na sifa za kuendelea kuwa katika nafasi hiyo na sehemu sahihi kwa sasa
ni mahakamani.
“Sina mambo
mengi ya kuzungumzia kilichotokea, lakini iwapo Katiba imefuatwa, hana sifa
tena ya kuwa Mwenyekiti, hivyo kwa ushauri wangu aende mahakamani,” alisema.
Mwanasheria
wa Mahakama ya Rufaa, Profesa Abdallah Safari alisema kwa mtazamo wake, sehemu
sahihi kwa Lipumba ni mahakamani, kwani ndani ya chama inaonekana haaminiki
tena.
“Naamini
salama yake ni mahakamani, kwani kikatiba natambua Baraza lina nguvu ya hicho kilichotokea,
hasa kama limemjadili kama mwanachama na si kiongozi,” alisema.
Waunga
mkono
Katika
hatua nyingine, Jumuiya za Vijana, Wanawake, Baraza la Wazee na Bodi ya
Wadhamini ya Chama cha Wananchi (CUF), wameunga mkono uamuzi wa Baraza Kuu la Uongozi
la Taifa kumfukuza Profesa Lipumba.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti jana, viongozi wa taasisi hizo za CUF walisema uamuzi
uliofanywa na chama ni sahihi.
Wazee
Mwenyekiti
wa Baraza la Wazee wa CUF, Hamid Juma Haji alisema wako pamoja na Baraza Kuu na
wanamtaka Lipumba aheshimu uamuzi huo.
“Sisi wazee
tumekuwa katika wakati mgumu kupitia hali hii lakini uamuzi ambao umefanywa na viongozi
wa Baraza ni sahihi na tunaunga mkono,” alisema.
Vijana
Mwenyekiti
wa Juvicuf Taifa, Hamidu Bobali alisema wao vijana wanaungana na Baraza Kuu ili
kunusuru chama. Bobali alisema vijana wamegundua mazingira ya hujuma ndani ya
chama chao hivyo hawako tayari kuona ikitokea.
Wanawake
Makamu
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake, Severine Mwijage alisema wanaunga mkono kwa
asilimia 100 uamuzi huo na kuahidi kutoa ushirikiano katika masuala yote ya
kupigania chama.
Wadhamini
Mwenyekiti
wa Bodi ya Wadhamini ya Chama hicho, Abdallah Katau alisema Bodi inakubaliana
na uamuzi huo huku akimtaka Lipumba aondoke ndani ya chama hicho kwani hana
sifa za kuwa hapo.
Lipumba
Akizungumza
jana Mwenyekiti wa CUF, Profesa Lipumba alisema uamuzi wa Katibu Mkuu Maalim
Seif kumvua uanachama ni batili kwani amevunja Katiba ya chama hicho. Aidha,
amesema hafukuziki CUF na hana mpango wa kuhama hivyo wenye lengo hilo
wajipange na ataitisha kikao cha Baraza Kuu Taifa muda wowote kuanzia sasa.
“Nipo CUF,
na nipo ngangari kinoma, hivyo kiti kimejaa wasiwe na wasiwasi, na kikao cha
Baraza Kuu kitaitishwa hivi karibuni, mimi sifukuziki CUF sina mpango wa kuhama
wala kukiacha na kadi yangu bado inadai,” alisema.
“Kwangu
Katibu Mkuu ni Katibu Mkuu, nafasi na ofisi yake ipo, aje, akija apite hapa kwa
Mwenyekiti anisalimie ili nimwelekeze cha kufanya, pia apate miongozo ya
kukijenga chama maana nipo hapa na nitazidi kuwapo,” alisema.
0 comments:
Post a Comment