Mshtakiwa Leonard Materu |
MFANYABIASHARA Leornad Matelu (31), amepandishwa kizimbani
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kwa kutishia kupindua Ikulu
kupitia mtandao wa kijamii wa WhatsApp.
Matelu alipandishwa kizimbani jana mbele ya Hakimu Mkazi,
Magreth Bankika wa akiwa chini ya ulinzi wa Polisi, akituhumiwa kuchapisha
habari za uongo.
Wakili wa Serikali, Diana Lukondo alidai kuwa Matelu ambaye
ni mkazi wa Moshi Baa kwa Diwani, Mombasa, Dar es Salaam, anatuhumiwa kuchapisha
habari za uongo kwa njia ya mtandao.
Ilidaiwa kuwa Julai 17, Matelu akiwa Dar es Salaam
alichapisha ujumbe wenye lengo la kuudanganya umma kupitia mtandao wa kijamii
wa WhatsApp.
Lukondo alidai kupitia mtandao huo kuwa: “Magu ajiandae
tunakwenda kupindua hadi Ikulu,” maneno hayo yalikuwa na lengo la kumtishia
Rais John Magufuli.
Baada ya mshitakiwa kusomewa mashitaka, alikana kuhusika
na tuhuma hizo, ambapo Lukondo alidai upelelezi haujakamilika na kuomba tarehe
nyingine ya kutajwa.
Pia alidai kuhusu dhamana ya mshitakiwa huyo hana pingamizi
kwa sababu mashitaka yanayomkabili kisheria yanadhaminika.
Wakili wa Matelu, Neema Lamwai aliomba dhamana ya mteja
wake kwa sababu sheria iko wazi kuwa mashitaka hayo yana dhamana.
Mshitakiwa alitimiza masharti na kuachiwa kwa dhamana, na
kesi hiyo itatajwa Septemba 20.
0 comments:
Post a Comment