Siku moja baada ya vigogo wa CCM kuhojiwa na wasaidizi wa Rais Johh Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama hicho kuhusu sakata la kuuzwa kwa mtambo wa kuchapisha magazeti wa Modern, malimbikizo ya mishahara na kulegalega uongozi, Bodi ya Kampuni ya Uhuru Publications Limited (UPL) imeandika barua ya kujiuzulu.
Msemaji wa
Chama hicho, Christopher ole Sendeka aliiambia JAMBO LEO jana, kuwa hatua iliyochukuliwa
na Bodi hiyo ni ya hiari, ikiwa ni muda mfupi kabla ya kutoa taarifa kwa vyombo
vya habari, kuhusu uamuzi huo chini ya Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Adam Kimbisa.
“Bodi imeandika
barua ya kujiuzulu, sasa ukiniuliza kuwa wamechukua uamuzi huo kutokana na
kuibuliwa kwa uuzwaji wa mtambo na mambo mengine, hapo hutakuwa sahihi, wewe
kama unahitaji kujua hilo fanya uchunguzi wako,” alisema Sendeka.
Uamuzi wa
Bodi hiyo umekuja zikiwa ni siku mbili tangu Rais Magufuli atembelee ofisi za
UPL na kuelezwa kuhusu uuzwaji wa mtambo huo na kufuatiwa na mshikemshike wa
vigogo wa chama hicho kuitwa kutoa maelezo ya kina kuhusu mambo yaliyoibuliwa
na wafanyakazi wa kampuni hiyo.
Habari
kutoka ndani ya Chama hicho zilizoifikia JAMBO LEO zilieleza kuwa kazi hiyo ya
kuwahoji watu mbalimbali ilifanywa na wasaidizi wa Rais, huku watoa taarifa
kuhusu ‘madudu’ hayo, wakiwamo wanahabari na watumishi wa chama hicho,
wakiahidiwa kulindwa ili wasifukuzwe kazi au kuwajibishwa na uongozi wa
kampuni.
Baadhi ya
vigogo hao walilazimika kupanda ndege kuwahi mahojiano hayo yaliyofanyika juzi
na jana, huku taarifa zaidi zikieleza kuwa hali imekuwa tete kwa baadhi ya
‘wapigaji’ kutokana na Rais kuonesha wazi kutaka kukirejesha chama hicho katika
ramani iliyoanza kupotea.
Juzi Rais
Magufuli akifuatana na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Sendeka,
alifanya ziara ya ghafla katika ofisi ndogo ya makao makuu ya CCM na UPL na
kuzungumza na wafanyakazi walioibua sakata hilo.
Miongoni
mwa yaliyoibuliwa ni kuuzwa kwa mtambo huo, malimbikizo ya madeni na uongozi
kulegalega katika utendaji.
Mtambo huo
ulisitisha huduma ya kuchapisha magazeti tangu mwaka 2012 ambapo kwa sasa kampuni
hiyo inachapisha katika mtambo wa Jamana kwa Sh milioni 52 kwa mwezi.
Wanaotajwa
kuhojiwa ni pamoja na mwenyekiti wa CCM katika moja ya mikoa Kanda ya Kati na
kada wa chama hicho ambaye hivi karibuni aliteuliwa na Rais kuwa Mkuu wa
Wilaya.
“Yupo mmoja
alikuwa mkoani alipigiwa simu na kutakiwa kufika leo (juzi) kwa ajili ya
kuhojiwa juu ya masuala mbalimbali, likiwamo hilo la mtambo,” alisema mtoa habari
huyo.
Taarifa
zaidi zilieleza kuwa baada ya ziara hiyo, baadhi ya vigogo walikuwa
wakijadiliana kuhusu suala hilo katika mitandao ya kijamii, huku wakiponda
watoa taarifa kwa Rais, “hao nao watashughulikiwa maana walichokuwa
wakijadiliana, nacho kimechukuliwa na wahusika. “Rais alitaka kupata maelezo ya
kina kuhusu jambo hili, ndiyo maana alituma wasaidizi wake kuhoji watu
mbalimbali, wakiwamo waliompa hizo taarifa.”
Gazeti hili
lilimtafuta Katibu wa Uchumi na Fedha wa CCM, Zakia Meghji na kumwuliza kuhusu suala
hilo, lakini badala ya kujibu alikata simu, hata alipopigiwa kwa zaidi ya mara
tatu hakupokea.
Baadaye CCM
ilitoa taarifa ya kujiuzulu kwa Bodi hiyo ya UPL, ikieleza kwamba Mwenyekiti wa
CCM, Rais Magufuli amepokea barua ya kujiuzulu kwao ambayo nakala yake pia
imetumwa kwa Kinana.
0 comments:
Post a Comment