VYAMA vya Wafanyakazi na Asasi za Kiraia Nchini, vimetaka
wabunge kukataa mjadala wa Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Mifuko ya Hifadhi
za Jamii unaotarajiwa kusomwa kwa mara ya kwanza bungeni, usisomwe hadi
Serikali irejeshe kipengele cha fao la kujitoa.
Hayo yamo kwenye tamko lililotolewa jana kwa vyombo vya
habari na likiwa limesainiwa na jumuiya za wafanyakazi zikiwamo NUMET, TUCTA,
RAAWU, TUIKO, CWT, CHODAWU na Mitandao ya Asasi za Kiraia Tanzania chini ya
Mwavuli wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC).
Muungano huo ulisikitishwa na lengo la Serikali kutaka
kuondoa utaratibu wa Fao la Kujitoa kupitia Muswada huo.
“Tunawasihi wabunge kama wawakilishi wetu, na wao kama
waathirika wa mabadiliko haya, kusitisha majadlilano ya Muswada wa Mabadiliko
ya Sheria ya Mifuko ya Hifadhi za Jamii unaotarajiwa kusomwa kwa mara ya kwanza
kwenye vikao vinavyoendelea vya Bunge la Nne, usisomwe hadi Serikali irejeshe
kipengele cha fao la kujitoa,” lilieleza.
Muungano huo ulizitaka jumuiya hizo kutumia muda kutetea
maslahi ya wafanyakazi wao, kwani kutofanya hivyo kunaweza kuleta tafsiri mbaya
ya kuwepo kwa jumuiya hizo.
“Watanzania wote wapaze sauti kuukataa Muswada huu, kwani
unakwenda kuminya haki za Watanzania wengi wanaofanya kazi kwa jasho lao katika
maeneo mbalimbali,” taarifa hiyo ilisema.
Iliongeza kuwa mchakato huo wa kubadilisha Sheria za
Mafao ulipaswa kuwa shirikishi kwa kuhusisha wenye mifuko hiyo-
wafanyakazi-kupitia vyama na vikundi vyao vinavyotambuliwa kisheria.
"Kinachoshangaza ni usiri mkubwa katika hili hasa
lengo la kutaka kupeleka Muswada huo kwa hati ya dharura bila ushiriki wa
wadau," lilisema tamko hilo.
Lilieleza kuwa pamoja na changamoto nyingi kwenye Muswada
huo, lakini haki ya fao la kujitoa kwa mfanyakazi anayeacha kazi kabla ya muda
wa kustaafu iko pale pale.
Lilisema Watanzania wafanyakazi hasa katika maeneo
yasiyokuwa na ajira za kudumu kama migodini, viwandani, mashambani na kwenye
mashirika yasiyo ya kiserikali (AZAKI) wanastahili kupata fao la kujitoa.
Tamko hilo liliongeza kuwa ni haki ya wafanyakazi kudai
fao la kujitoa kutokana na kuwa ajira katika sekta binafisi si za kudumu, ni za
mikataba ya muda mfupi, wanafunzi wengi wanapomaliza shule au vyuo hupenda
kufanya kazi kwa muda na baadaye kutumia fao la kujitoa kujiendeleza kielimu.
Vyama hivyo viliitaka Serikali itoe tamko mara moja la
kuruhusu mafao hayo kutolewa kwa wafanyakazi ambao hawako kazini kwa sasa,
kuishauri Serikali kuacha utaratibu uliokuwapo uendelee, kwa maana kwamba,
mfanyakazi awe na hiari ya kuchukua mafao yake au kusubiri kustaafu badala ya
kuwawekea vikwazo kwenye pesa zao.
0 comments:
Post a Comment