Suleiman Msuya na Fidelis Butahe
WAKATI
wanasiasa na wasomi wakimnyooshea kidole Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji
Francis Mutungi (pichani) kwa uamuzi wake wa kumtambua aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF,
Profesa Ibrahim Lipumba, mwenyewe ameibuka na kusema kuwa hatua yake hiyo haikulenga
kumrudishia msomi huyo nafasi yake ya uenyekiti.
Aliliambia
gazeti hili jana kuwa alichofanya ni kukishauri chama hicho kuhusu mgogoro
uliokuwa ukikisonga na Lipumba aliamua kutumia ushauri huo kurudi mwenyewe
kwenye nafasi yake hiyo kinyemela.
Kauli hiyo
ya Jaji Mutungi imekuja siku mbili tangu alipotoa waraka unaoelezwa kumtambua Profesa
Lipumba kama kiongozi halali wa CUF licha ya kuandika barua ya kujiuzulu Agosti
6, mwaka jana akipinga vyama vinavyounda Ukawa kumpa fursa Waziri Mkuu wa
zamani, Edward Lowassa kugombea urais.
“Isome
barua yangu…, mimi nimeamua watu waijadili umenielewa? Ni vizuri
wanavyoijadili, ila nilitarajia waijadili kwa tija sio kwa hasira,” alisema
Jaji Mutungi.
Alipoulizwa
kuhusu polisi kumsaidia Profesa Lipumba kuingia katika makao makuu ya CUF kwa mtutu
alisema: “Hizo ni taratibu ambazo (polisi) wanatumia kwa kuzingatia sheria
nyingine za nchi.”
Juni mwaka
huu, Profesa Lipumba alimwandikia barua Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif
Hamad kutengua barua yake ya kujiuzulu na kutaka arejee kwenye kiti chake,
uamuzi uliozusha mtafaruku huku Mkutano Mkuu wa chama hicho ulioketi Agosti 21
ukiridhia kujiuzulu kwake licha ya kuwa ulivunjika.
“Barua
yangu inajieleza sina haja ya kuichambua. Nimekujibu baada ya kuona mjadala huo
(katika mitandao) nilitegemea (waliomtukana) wawashauri CUF cha kufanya badala
ya kuanza kunitukana,” alisema Jaji Mutungi.
“Sasa huko
mahakamani wanakotaka kwenda kama mahakama ikiamua kama Mutungi alivyoshauri
huko nako watatukana pia?” alihoji.
Wanasiasa
na wasomi Mwenyekiti wa
Chama cha Kijamii
(CCK), Constatine Akitanda alisema alichofanya msajili ni kupandikiza zogo ndani ya CUF jambo ambalo linasikitisha.
Akitanda
alisema ndani ya CUF kuna bundi ambaye alikuwa anasumbua watu ila msajili ameongezea
mgogoro huo na kuwa alichokifanya si sawa kwa mujibu wa mamlaka yake.
“Unajua hii
nchi inachezewa sana hivi mtu anajiuzulu mwenyewe halafu anaamua kurejea
mwenyewe bila kufuata taratibu ni aibu, lakini nadhani kuna mkono wa mtu,’
alisema.
Mwenyekiti wa
Chama cha ACT-Wazalendo, Anna Mghwira alisema anachokiona ndani ya CUF ni uwepo
wa biashara haramu ambayo inaweza kuua chama hicho.
Alisema ni
wakati mwafaka kwa wafanyabiashara haramu hao wakajulikana katika pande zote
kwani ni aibu kuvumilia kasoro hizo zitawale vyama vya siasa.
Naibu
Katibu Mkuu wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Dominata Rwechungura alisema
migogoro ndani ya vyama vya siasa ipo, hivyo ni jukumu la CUF kutatua ili
kurejesha amani na upendo kati yao.
Mwenyekiti
wa Chama cha United People Democratic Party (UPDP), Fahimu Dovutwa
alisemakinachotokea ni msiba unaoacha pengo ndani ya CUF na vyama vya siasa
nchini.
Dovutwa
alisema pia pengo la mwasisi wa CUF, marehemu Shaban Mloo linaonekana na
kuwataka wazee wa chama hicho kukaa ili kukinusuru chama. “Huu ni msiba katika
siasa za Tanzania, naomba CUF watafute wazee wao ili waweze kusuluhisha hali
hiyo kwa maslahi ya chama chao kwani pengo la Mloo linaonekana,” alisema.
Katibu wa
Habari na Uenezi wa NCCR Mageuzi, David Kafulila alisema mgogoro wa CUF unaweza
kutolewa uamuzi na mahakama pekee kwa kuwa msajili hana mamlaka ya kufanya
alichokifanya. Kafulila alisema msajili anapaswa kushauri kwa mujibu wa Sheria
ya Vyama vya Siasa na si kama alivyoelekeza kwani anaongeza mgogoro zaidi.
Mwenyekiti
wa ADC, Hamad Rashid alishauri CUF kutumia vikao kumaliza tofauti zao, huku
akibainisha kuwa ndani ya chama hicho kuna viashiria vya udikteta na usultani.
Mbunge wa
Tandahimba CUF, Katani Katani alisema kwa sasa wamethibitisha jinsi Lipumba
anavyotumika kwani pamoja na Jeshi la Polisi kukataza maandamano, wafuasi wa
Lipumba waliandamana bila kuzuiwa.
Alisema
haiwezekani chama kikaendeshwa kwa ajenda za watu wachache ambao wanatumikia
matumbo yao na makundi yao na si chama.
Mhadhiri
Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Kitivo cha Sheria, Dk. Onesmo
Kyauke alisema msajili anakosea na kuwataka CUF wakimbilie mahakamani kupata
haki.
0 comments:
Post a Comment