* Mbowe, Mbatia waeleza kirusi kilichoandaliwa kuiua
Fidelis
Butahe
TAKRIBANI
miaka miwili baada ya vyama vinne vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa) kutiliana saini ya makubaliano saba ya ushirikiano, wenyeviti wake
wametaja changamoto nne zinazokwamisha malengo yao.
Hata hivyo,
viongozi hao wamesisitiza kuwa uhai wa umoja huo kuelekea ushindi kwenye
uchaguzi mkuu mwaka 2020, unategemea zaidi kuaminiana kwa viongozi wa vyama vya
CUF, Chadema, NCCR- Mageuzi na NLD vinavyouunda.
Kwa nyakati
tofauti wenyeviti wa vyama hivyo vilivyoandika historia mpya tangu kuanzishwa kwa
mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, wameliambia JAMBO LEO kwamba bila upinzani
imara ni ngumu kuitikisa CCM na hila zinafanyika kuwagawanya.
Changamoto
za Ukawa Walitaja
changamoto hizo
kuwa ni dola kutumika
kuvigawanya vyama vinavyounda Umoja huo, kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara, kupuuzwa kwa maoni ya Rasimu ya Katiba ya iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na migogoro ya ndani inayovikumba vyama hivyo.
Wenyeviti
hao, Freeman Mbowe (Chadema), James Mbatia (NCCR-Mageuzi) na Julius Mtatiro
ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya uongozi ya CUF, wamesema wataimarisha Ukawa
hadi dakika ya mwisho licha ya kuwa Katiba na sheria za vyama vya siasa,
vinakiukwa kwa lengo la kuwabana.
Oktoba 26
mwaka 2014, viongozi wakuu wa vyama hivyo vitatu pamoja na NLD, walisaini makubaliano
hayo katika viwanja vya Jangwani, huku msingi wa umoja huo ukitokana na kuachwa
kwa maoni ya wananchi yaliyokuwa katika Rasimu ya Katiba ya tume hiyo iliyokuwa
ikiongozwa na Jaji Joseph Warioba.
Katika
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana, vyama hivyo vilisimamisha mgombea mmoja
wa urais na kumuunga mkono, huku vikiachiana baadhi ya majimbo na Kata.
Mbowe
“Msingi
mkuu wa Ukawa ilikuwa kupigania Katiba ya Wananchi, mpaka sasa kumekuwa na
mgogoro mkubwa kuhusu mtizamo na tafsiri ya siasa ni nini kiasi kwamba chama
kimoja kimoja kufanya kazi ya siasa imekuwa taabu achilia mbali kufanya siasa
kwa pamoja,” alisema Mbowe.
“Tulitarajia
kurudi kusaka Katiba ya Wananchi, ambayo ilitegemewa kutoa mwanya wa vyama vya
siasa kuungana kitu ambacho kwa katiba ya sasa (inayopendekezwa) inakataza.
Hicho kimekuwa kikwazo kikubwa kwa upinzani kuimarika na wenzetu wanatumia
wingi wao kukataa umuhimu wa kuwa na mazingira ya kisheria na kikatiba kwa
vyama kuongeza nguvu.”
Mbowe
alitolea mfano jinsi Katiba ya Zanzibar ilivyovunjwa kwa kuundwa kwa Serikali
ya ‘mezani’ ya Umoja wa Kitaifa, “wenzetu hawana utamaduni wa kuheshimu sheria.
Katika mazingira kama hayo unazungumziaje mustakabali wa Ukawa? Tunazungumziaje
wakati hata kufanya siasa ni tatizo.”
Kuhusu
mvutano ulioibuka CUF huku aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim
Lipumba akirudi katika wadhifa wake, Mbowe alisema ni jambo la kustaajabisha.
“Yeye
(Lipumba) alikuwa mtu wa kupinga Ukawa sasa umoja wetu unakwendaje sasa? Kuna changamoto
nyingi za kuzifanyia kazi kabla ya kujua
mwelekeo wetu. Lengo la kuimarisha upinzani lipo pale pale, tutajitahidi kwa
nguvu zetu kama Chadema kuhakikisha tunaendelea na ushirikiano wetu,” alisema.
Mbatia
Akizungumzia
umoja huo, Mbatia alisema kwa muda mrefu dola imekuwa ikifanya hila kuvigawa
vyama vya upinzani, huku akitolea mfano yaliyotokea NCCR-Mageuzi baada ya mwaka
1995 na yaliyokikumba CUF.
“Ukawa
hatuhitaji kanuni zituongoze, tunachohitaji ni ushirikiano na kuaminiana ambako
ndio kulizaa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar. Hata Nyerere (Mwalimu
Julius) na Karume (Amani Abeid) waliaminiana na kuunganisha vyama baadaye
sheria ikafuata.”
Alisema
kitendo cha wabunge wa vyama vinavyounda umoja huo kuaminiana bungeni, ikiwa ni
pamoja na kususia vikao vya chombo hicho cha kutunga sheria kudai kile
alichokiita ‘jambo muhimu kwa maslahi ya wananchi’, ni ishara nzuri.
“Ndani ya
vyama vyetu wapo baadhi ya wanachama hawapendi umoja huu, hivyo kama kiongozi
usipoangalia wapi umoja unataka kwenda hatuwezi kufika…, nawashauri wenzangu
tuangalie maslahi mapana ya Watanzania kuliko maslahi binafsi za kila chama,” alisema
Mbatia.
“Tulivyokwenda
katika uchaguzi, moja ya malengo tuliyokuwa nayo pamoja na ushirikiano ni
kuhakikisha kuwa kabla ya 2020 tunakuwa na chama kimoja cha siasa, lakini
hatukushinda, ila lengo hilo litatimia kama tutaaminiana.”
Mtatiro
“Ukawa ni
jukwaa kubwa zaidi la kisiasa baada ya uchaguzi wa mwaka jana. Uwepo wetu
uliambatana na makosa mengi ya kujifunza, kunafikiana, kutoaminiana, kuchezeana
kete za kisiasa…, hata kama vyama vilinafikiana na kuzungukana bado wananchi
waliamini umoja wetu, kuelekea 2020 tutarajie uimara zaidi,” alisema.
“Kwa sasa
Ukawa tunaogopwa zaidi. Tazama Rais Magufuli kwa sasa hataki kuona viongozi wa
vyama vya Ukawa wakizunguka kufanya shughuli za kisiasa. Woga huo ukupe salamu
kuwa sisi tunaendelea kuwa tishio,” alisema.
“Kwa sasa
Rais anafanya makosa kadhaa ambayo kisiasa ni makubwa, ndiyo anazidi kuipa
nafasi. Rais akimaliza miaka yake mitano bila viwanda, ajira, uchumi kuzidi
kuporomoka, Ukawa itakuwa lulu.”
Alisema kwa
sasa CUF inaendelea kujiimarisha ili ikifika mwaka 2019 chama hicho kiwe
kimejizatiti ipasavyo katika kutengeneza ushirikiano imara.
0 comments:
Post a Comment