MKAZI wa Lindi, Dennis Marcus na
mkewe raia wa Uingereza, Antonia Martin, wamefunga ndoa kwa sherehe ya aina
yake wakipanda bajaji na kunywa pombe ya kienyeji pamoja na wageni waalikwa.
Akizungumza na gazeti hili kwa
simu jana, Marcus alisema harusi hiyo ilifanyika Namanga, Lindi na waliamua iwe
hivyo, ili kuonesha tofauti kati ya mila na utamaduni wa kiafrika na wa
kizungu.
Alisema harusi hiyo ilifuata muda
wa harusi za kawaida, lakini waalikwa walikula wali kwa maharage, pilau na
kunywa pombe za kienyeji ili kuonesha utofauti huo.
“Nilitaka harusi iwe tofauti sana
kwa kuwa kama ni gari lilikuwapo, hivyo haikuwa na haja ya sisi kulitumia,
nikaamua kutumia bajaji kwa sababu si kitu kinachotumika katika harusi mara
kwa mara,” alisema.
Mavazi
Kwa mujibu wa Marcus, gauni la
harusi la mkewe lilishonwa nchini kwa ubunifu wake ingawa viatu, suti na ua la
bibi harusi vilitoka Uingereza.
Akielezea historia yao, Marcus
alisema walikutana na mkewe huyo mwaka 2008 Uingereza akiwa kwenye michezo ya
sarakasi.
“Huwa nakwenda mara kwa mara Uingereza
kwa masuala yangu na sarakasi na huko nilikutana naye,” alisema na kuongeza
kuwa mkewe alisindikizwa na binamu yake na mtoto wake aliyezaa kabla ya wao
kukutana.
“Mimi ndiye nilianza kumpenda ambapo
mwaka 2008 nilikuwa nacheza ‘pool table’ ndipo akaja na rafiki yake nami nikamwambia
jinsi ninavyojisikia,” alisema.
Alisema mwaka 2013 kulikuwa na
mashindano ya sarakasi Uingereza ambapo mkewe alikuwa meneja na baadaye mwaka
2014 walikutana tena Dubai wakaendeleza mapenzi yao na Januari mwaka jana
mkewe huyo alikuja nchini.
“Nahisi huyu ni mwanamke sahihi
kwangu, pia kutokana na umri wangu kwenda, hivyo nahitaji mke wa kuishi naye
kama vitabu vya dini vinavyosema,” alisema.
Marcus alisema aliona huyo
mwanamke ndiye chaguo sahihi kwake na kuishi pamoja na kuzaa watoto na kujenga
maisha ya baadaye.
Marcus alisema Julai 23 walifunga ndoa hiyo kwenye Kanisa
Katoliki, Lindi na aliyewafungisha ndoa hiyo ni Padri Alkuine Innocent.
0 comments:
Post a Comment