Grace Gurisha
RAIA watatu wa Pakistani wamehukumiwa kulipa faini ya Sh milioni
120, baada ya kupatikana na hatia ya kuingilia mawasiliano ya Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA), bila kibali na kuisababishia Serikali hasara ya Sh
milioni 140.
Washitakiwa hao ni Hafees Irfan, Mirza Irfan Baig na
Mirza Rizwani Baig, ambapo walikiri kuingilia mawasiliano hayo bila kibali huku
wakijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu Respicius
Mwijage, baada ya kupitia hoja zilitolewa na upande wa Jamhuri, vielelezo na
sheria.
Alisema washitakiwa walikiri makosa kwa mujibu wa sheria hivyo
wanapaswa kulipa faini ya Sh milioni tano katika kosa la kwanza ambalo
wanashitakiwa kwa kuingilia mawasiliano ya Mamlaka hiyo.
Pia alisema katika kosa la pili na la tatu watatakiwa
kulipa Sh milioni tano kwa kila kosa, jumla Sh milioni 15 katika makosa matatu
na wakishindwa watatumikia kifungo cha mwaka mmoja jela kwa kila kosa.
Hakimu Mwijage alisema katika kosa la nne kila mshitakiwa
anatakiwa kulipa faini ya Sh milioni 35 kutokana na kuisababishia Serikali na
TCRA hasara ya Sh milioni 140, ili kuepuka kutumikia kifungo cha mwaka mmoja
jela. Washtakiwa hao walilipa faini.
Kabla ya hukumu hiyo kutolewa, Wakili wa Serikali, Esther
Martin aliwasomea washitakiwa hao maelezo ya awali kwa kudai kuwa katika tarehe
Dar es Salaam, walikutwa na vifaa vya kuunganishia mawasiliano ya kimataifa
bila kibali cha TCRA.
Ilidaiwa kuwa katika kufanikisha malengo yao, walitoka
nchini kwao Pakistan na kwenda maeneo mbalimbali ikiwamo Falme za Kiarabu,
Malaysia, Msumbiji na hatimaye nchini ili kutumia vifaa hivyo.
Martin alidai walifika nchini tarehe tofauti na kufikia
kwenye hoteli ya Butterfly iliyoko Kariakoo, Dar es Salaam chumba namba 905.
Alidai kuwa Oktoba 5 mwaka jana maofisa wa Polisi wakifuatana
na wa TCRA walifika maeneo hayo na kuichunguza na kuwakamata washitakiwa hao.
Ilidaiwa kwenye chumba hicho, walikutwa na vifaa vya
mawasiliano ambavyo ni kadi za simu 15, CPU 18, kompyuta mpakato saba, kadi za
Airtel 258, modemu ya Huawei na vocha zilizotumika.
Baada ya kukutwa na vifaa hivyo, washitakiwa walifikishwa
kituo cha Polisi Kijitonyama na baada ya uchunguzi ilibainika kuwa
waliisababishia Serikali na TCRA hasara hiyo.
Baada ya kusomewa maelezo hayo, washitakiwa walikiri
kukutwa na kutenda makosa hayo wakiwa kwenye hoteli ya Butterfly.
Wakili Martin aliiomba Mahakama kutoa adhabu kali kwa
washitakiwa ili iwe funzo kwa wengine.
Hata hivyo, Wakili wa Utetezi Shadrack Ishengoma aliiomba
Mahakama hiyo kuwapunguzia adhabu washitakiwa kwa sababu walikiri makosa, pia
wanategemewa na familia zao.
0 comments:
Post a Comment