Wapinzani wampa JPM mambo 9 ya kuzingatia

Fidelis Butahe na Charles James

Dk John Magufuli
LICHA ya Serikali kufanya vizuri katika mwaka wake wa kwanza na kurejesha nidhamu ya kazi kwa kiasi kikubwa, viongozi wa Upinzani wametaja mambo tisa ya Rais John Magufuli kuzingatia ili aweze kufanya vizuri zaidi katika mwaka wake wa pili.  

Ushauri huo umetolewa na baadhi ya viongozi waliozungumza na JAMBO LEO jana wakisema hakuna Rais anayefanya mazuri bila kuwa na dosari kwenye baadhi ya maeneo na kwamba kazi yao na wananchi ni kuhoji na kukosoa ili mambo yaende sawa.

Walitaja mambo ambayo mkuu huyo wa nchi aliyeapishwa Novemba 5 anapaswa kuyaweka sawa kuwa ni utawala bora, kutominya demokrasia, kuweka mikakati imara ya kuinua uchumi na ujenzi wa viwanda, kuboresha huduma za elimu, uhusiano wa kimataifa, kuepuka uamuzi wa ghafla, kushughulikia ipasavyo migogoro ya ardhi na taasisi kuachwa zijisimamie pamoja na kuboresha sekta ya afya.

Tangu Rais Magufuli aingie madarakani, amefanya mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na ununuzi wa ndege, kusimamia miradi ya umeme, kuanzisha Mahakama ya mafisadi na kuzuia matumizi yasiyo ya lazima kwa kufuta sherehe mbalimbali.

“Anapaswa kuacha mifumo ifanye kazi ili kuepuka kuingilia mambo. Aiache mihimili mingine kama Bunge na Mahakama ifanye kazi yenyewe kwa sababu kuiingilia ni sawa na kuua demokrasia,” alisema Salum Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar.

Alisema hali hiyo imesababisha wasaidizi wake, wakiwamo wakuu wa mikoa na wilaya kufanya kazi kwa hofu na kudai kuwa baadhi wanashindwa kufuata sheria na kuishia kutekeleza majukumu yao kwa kumfurahisha Rais.

“Mfano vyombo vya habari kuminywa katika utendaji wa shughuli zake na Jeshi la Polisi kutumika kisiasa. Haya mambo yanaminya demokrasia. Ni baadhi ya vitu ambavyo Rais anapaswa kuvitazama kwa umakini mkubwa,” alisema Mwalimu.

Mwenyekiti wa Chama cha Umma (Chaumma), Hashim Rungwe ambaye aligombea urais mwaka jana, alimshauri Rais kuongoza nchi kwa kufuata sheria na Katiba.

“Ameshamaliza mwaka na sasa anaelekea mwaka wa pili, lakini bado sijaiona Tanzania ya viwanda ambayo (Rais) aliinadi wakati wa kampeni, badala yake tunashuhudia mvutano kati ya Serikali na wawekezaji,” alisema Rungwe huku akitolea mfano mvutano baina ya Serikali na kiwanda cha saruji cha Dangote.

 “Viwanda vinakufa na tayari tumesikia kuwa kiwanda hicho kinasitisha uzalishaji sasa utasema tunapiga hatua au tunarudi nyuma?”

Rungwe alisema Wizara ya Viwanda na Biashara na Nishati na Madini zinapaswa kuacha kubana wawekezaji kwa kuwalazimisha kutumia malighafi za nchini, badala yake zitafute mbinu mbadala za kuwavutia.

Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Danda Juju alisema, “Rais anapaswa kutekeleza wajibu wake kwa kufuata sheria ili walio chini yake nao waige. Mkuu wa mkoa huwezi kutukana na kudhalilisha watumishi, tena hadharani.”

Alisema Rais anapaswa kufanya taasisi kuaminiana kutokana na siku za karibuni baadhi ya vigogo serikalini kuzungumzia jambo moja lakini kila mmoja na msimamo wake.

Juju alitolea mfano kauli ya Rais Magufuli kwamba ni kosa kuweka fedha za umma kwenye akaunti za muda maalumu huku Gavana wa Benki Kuu (BoT), Benno Ndullu akibainisha kuwa hakuna tatizo lolote kuweka fedha za umma kwenye akaunti hizo.

“Tulivutia wawekezaji kwa masharti nafuu wakaja nchini, ila sasa tumegeuka. Nadhani umeona ya kiwanda cha Dangote,” alisema.

Kauli hiyo iliungwa mkono na aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini kwa tiketi ya chama hicho, David Kafulila na kusisitiza kuwa kuzuiwa kwa matangazo ya moja kwa moja ya Bunge ni kuminya demokrasia na kutenganisha wananchi na wawakilishi wao na Serikali.

“Rais anapaswa kutazama upya mikakati ya uchumi maana mzunguko wa fedha haueleweki na biashara zimeyumba. Pia katika uhusiano wa kimataifa kuna tatizo, Serikali inapaswa kuwa na msimamo mmoja ili kuwaondolea hofu wawekezaji ambao wanahisi jambo lolote, zikiwemo sheria zinaweza kubadilishwa muda wowote na kuathiri biashara zao,” alisema.

Katibu Mkuu wa Chama cha Alliance of Tanzania Farmers (AFP), Rashid Rai alishauri kiongozi mkuu wa nchi amulike sekta ya afya kwa maelezo kuwa bado kuna changamoto nyingi.

Alisema kero katika huduma za afya hazipo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) pekee, bali hospitali zote nchini.

Kuhusu hoja ya ‘Tanzania ya Viwanda’, Rai alisema wakati Serikali ikiingia mwaka wake wa pili, hakuna mikakati ya kueleweka ya kujenga viwanda nchini.

Huku akionesha kushangazwa na mawaziri kushindwa kujifunza jinsi Japan na China zilivyokuwa na viwanda vingi, alisema migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji ni tatizo sugu ambalo miaka nenda rudi limekosa ufumbuzi.

“Ni rahisi sana kumaliza mgogoro wa ardhi, Serikali ina maeneo mengi ya wazi ambayo ni mapori na misitu, kwa nini wasiyagawe kwa hawa wakulima na wafugaji ili kuzuia watu kuuana? Serikali sikivu haiwezi kushuhudia mauaji ya raia wake ilhali inaweza kuyatatua na kuyamaliza,” alisema.

Katibu Mkuu wa NLD, Tozi Matwange alisema: “Rais anapaswa kuendelea kushauriwa juu ya uminyaji wa demokrasia kwa kuzuia mikutano ya hadhara na maandamano…ni kinyume na Katiba.

“Pia utawala bora ni tatizo. Huku ‘kutumbua majipu’ kunafanyika kinyume na taratibu, sheria na Katiba ya nchi, ni tatizo kubwa.”

Katibu Mkuu wa CCK, Renatus Muabhi alisema Rais anapaswa kuboresha maisha ya wananchi kwa kuimarisha uchumi wa nchi huku akinukuu taarifa za BoT zinavyoainisha uchumi wa nchi kuyumba.

 “Serikali imekwenda kununua ndege mpya bila kuwa na mikakati halisi ya kuinua shirika la ndege. Nadhani fedha zile zingepelekwa kwanza kuboresha sekta ya afya, elimu na maji, huku ikiendelea kupanga mikakati ya kulifufua shirika hilo, ambalo linahitaji kusaidiwa mengi ili liweze kusimama si kuwa na ndege peke yake,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo