Suleiman Msuya
Lawrence Mafuru |
SIKU moja baada ya Rais John Magufuli kutengua
uteuzi wa aliyekuwa Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru na kumteua Dk Osward
Mashindano kushika nafasi hiyo, baadhi ya wachumi wamesema Msajili huyo hakusoma
alama za nyakati.
Kauli hizo za wachumi zinakuja huku
ikidaiwa kuwa Mafuru aliondolewa kutokana na kauli yake, kwamba hakuna tatizo
kwa taasisi za Serikali kuweka fedha kwenye akaunti za muda maalumu inayoelezwa
kupingana na ya Rais Magufuli.
Katika mazungumzo yake mengi, Rais
Magufuli amekuwa akizungumzia kutoridhishwa na utaratibu wa taasisi za Serikali
kuweka fedha kwenye akaunti hizo kwenye benki binafsi, hali iliyochangia kuvunjwa
kwa Bodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hivi karibuni.
Wakati Rais anahutubia mahafali ya Chuo
Kikuu Huria (OUT), alisema Bodi ya TRA iliruhusu Sh bilioni 26 kuwekwa kwenye
akaunti za muda maalumu na kutumiwa kwa maslahi binafsi, jambo ambalo alishalikataza.
Akizungumzia sakata hilo, Mhandiri
Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Damian Gabagambi alisema: “Kimsingi
alichosema Mafuru kiuchumi ni cha kweli na kama Msajili huyo amewajibishwa kwa
kauli hiyo, tatizo lake ni kutosoma alama za nyakati.”
Gabagambi alisema akaunti hizo ndizo hutumika
kwa wawekezaji kukopa, hivyo zina faida tofauti na kuweka akaunti za kawaida.
“Hakuna madhara ya fedha kuwekwa kwenye
akaunti kama hizo na kama kilichomwondoa ni kauli yake, hajatendewa haki kwani
aliongea ukweli kiuchumi labda tumlaumu kwa kutosoma alama za nyakati za
uongozi wa sasa,” alisema.
Alisema pamoja na changamoto ambazo
wanataaluma wanaweza kukutana nazo katika uongozi bado hawapaswi kukata tamaa,
kwani hilo ndilo jukumu lao.
Dk Christopher Awinia wa OUT, alisema
kinachotakiwa ni watendaji kutambua kuwa kila uongozi una mfumo wake, hivyo kupaswa
kwenda nao.
Alisema changamoto zingine ambazo
zinaonekana katika uongozi wa sasa zinajibu mahitaji ya Katiba mpya ambayo
ilikuwa inaondoa madaraka makubwa kwa baadhi ya watu hasa Rais.
Dk Awinia alisema mhasibu aliyebobea
katika kazi hiyo, atashawishi utumiaji wa akaunti hiyo, hasa kwa fedha za
miradi ambayo inahitaji utekelezaji wa baada ya miezi mitatu, kwani ina faida
tofauti na akaunti za kawaida.
Aidha, alisema hakuna taarifa yoyote ambayo
inatoka kwa Msajili ikionesha kuwa akaunti hiyo ina madhara kwa wawekaji fedha
za umma jambo ambalo linaonesha kuwa na faida.
Hata hivyio hakuna mahali ambako Rais
alisema kutumia akaunti hizo ni kosa, bali matumizi ya faida itokanayo ambayo
imekuwa ikitumiwa kwa maslahi binafsi.
Pamoja na hayo inasemekana Mafuru ‘ametumbuliwa’
kutokana na kuwa na maslahi kwenye benki ya CRDB ambayo yeye ni Mkurugenzi
Huru.
Kutona na nafasi hiyo ambayo aliigombea
na kushinda, moja kwa moja Mafuru anaingia kama mjumbe wa bodi ya CRDB hali
ambayo inadhaniwa kuwa ilichangia kubainisha kuwa hakuna madhara kwa taasisi za
umma kuweka fedha huko, ambapo wachumi wanasema si kosa.
Aidha, Mafuru alipata kuwa Mkurugenzi wa
Benki ya NBC, kuanzia Juni 2010 hadi Desemba 2012 na pia Mwenyekiti wa Chama
cha Benki nchini kuanzia Januari 2010 hadi Desemba 2012.
Halikadhalika alifanya kazi katika Ofisi
ya Rais kwenye taasisi ya Matokeo Makubwa Sasa (BRN) kama Mkurugenzi wa
Rasilimali na Uchumi.
0 comments:
Post a Comment