Lema asherehekea Uhuru akiwa gerezani


Seif Mangwangi, Arusha

Godbless Lema
MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema, ameendelea kukaa gerezani baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kushindwa kusikiliza maombi yaliyowasilishwa na wakili wake, Sheck Mfinanga.

Wakili Mfinanga aliiomba Mahakama hiyo imwongeze muda wa kupeleka notisi ili rufaa yao isikilizwe.

Maombi hayo yaliyokuwa yasikilizwe na Jaji Dk Modesta Opiyo jana yalikwama baada ya upande wa Jamhuri ukiongozwa na Mwanasheria wa Serikali wa Mkoa wa Arusha, Maternus Marandu kuileza Mahakama kuwa wanaomba muda wa kuleta hoja kinzani juu ya maombi hayo.

“Hatuko tayari kusikiliza maombi ya utetezi, kwa kuwa walileta mahakamani hapa jana nasi tunaomba muda wa kuleta hoja zetu kinzani kwa kuwa sheria inaturuhusu," aliieleza Mahakama.

Alisema upande wa utetezi ulileta maombi hayo chini ya hati ya dharura, lakini walitakuwa kuyaleta kama maombi mengine kwa kuwa bado wako ndani ya muda.

“Uamuzi wa Mahakama wa Novemba 11 kisheria wanapaswa kuhesabu siku 45 kutoka tarehe hiyo... leo (jana) ni Novemba 8, bado wako ndani ya muda wa kuleta maombi yao mahakamani hapa, sioni sababu ya upande wa utetezi kuleta maombi hayo chini ya hati ya dharura.”

Baada ya maelezo hayo, Dk Jaji Opio aliutaka upande wa Jamhuri kuwasilisha hoja zao kinzani Desemba 13 ambapo upande wa utetezi  utazijibu siku hiyo hiyo  saa 5 asubuhi na Desemba 14 Mahakama itasikiliza maombi hayo.

Desemba mbili Mahakama hiyo mbele ya Jaji Mfawidhi  Fatuma Masengi ilitupilia mbali maombi ya rufaa ya Mbunge huyo kusikilizwa baada ya Mahakama kuona kuwa yaliwasilishwa nje ya muda.

Akisoma uamuzi huo mdogo wa Jaji  Masengi Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Angero Rumisha alisema Mahakama imefuta maombi hayo ya rufaa, kutokana na wakata rufaa kuwa nje ya muda.

Rumisha alisema kutokana na hoja hizo, Mahakama ilikubaliana na upande wa pingamizi na upande wa Serikali kupitia Wakili Paul Kadushi akishirikiana na Marandu kuwa rufaa hiyo haikufuata misingi ya kisheria kukatwa, kwa kuwa hawakuwasilisha mahakamani hapo kusudio la kukata rufaa na kuiomba Mahakama  itupilie mbali rufaa hiyo.

Hata hivyo, wakati mawakili wa Lema wakiwasilisha hoja yao jana na kushindwa kusikilizwa, Mbunge Lema hakufika mahakamani hapo kutokana na sababu zisizofahamika.

Nje ya Mahakama

Viongozi wa Chadema chini ya Katibu Mkuu, Vincent Mashinji walionekana mahakamani hapo.

Viongozi wengine ni Katibu wa Chadema, Kanda ya Kaskazini, Amani Gulugwa, Mbunge wa Viti Maalumu, Cesilia Pareso, Joyce Mukya wa mkoa wa Arusha na Lucy Magereli wa Iringa.

Akizungumzia kesi hiyo, Mashinji alisema mashitaka dhidi ya Lema yanadhaminika na kuiomba Mahakama kutenda haki kwa Mbunge huyo ili aweze kutumikia wapiga kura wake.

Golugwa aliiomba Polisi iruhusu wafuasi wa Chadema kuingia mahakamani hapo tofauti na ilivyo sasa, ambapo ni wafuasi wachache tu ndio wanaruhusiwa kuingia.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo