*Mabadiliko ndani ya CCM huenda yakatikisa Baraza
*Atarajiwa
kuja na Sekretarieti mpya mwisho wa wiki
Waandishi Wetu
Rais John Magufuli |
KUNA kila dalili kwamba mwaka 2016
hautapita salama bila Rais John Magufuli kufanya mabadiliko japo madogo katika
Baraza lake la Mawaziri, hatua inayowaweka mawaziri wake 35 mguu ndani mguu
nje.
Hatua hiyo inatajwa kuchagizwa na mambo
mbalimbali, mawili makubwa yakiwa mabadiliko yanayonukia ya Sekretarieti ya CCM,
lakini pia utendaji wa mawaziri takribani mwaka mmoja tangu kuteuliwa kushika nyadhifa
hizo.
Uchunguzi wa JAMBO LEO na maoni ya watu
wa kada mbalimbali unabainisha kwamba Rais Magufuli kimfumo na matukio ndani ya
CCM ambayo pia yeye ni Mwenyekiti, atafanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri akiongozwa
na namna anavyotaka kuunda Sekretarieti mpya ya chama hicho.
Aidha, anatarajiwa kufanya mabadiliko
hayo pia kutokana na kuuelewa vizuri utendaji wa mawaziri wake, udhaifu na
nguvu zao katika kazi baada ya kuwapima tangu alipowateua.
“Serikali ni ya CCM, hivyo kada yeyote
ndani ya Serikali anaweza kuingia kwenye sekretarieti. Kama hilo likitokea,
hakutakuwa na jipya ni kama mwendelezo tu ambao pia ulifanywa na marais
waliopita,” alisema Dk George Kahangwa, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanataaluma wa
Chuo Kikuu Dar es Salaam (Udasa).
“Tangu aingie madarakani, Rais Magufuli
amekuwa akitumia makada wa CCM zaidi pengine anawaamini kuwa wanaweza kwenda
naye sambamba katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama hicho,”
aliongeza.
Alisema katika uteuzi, kitu kinachopaswa
kuangaliwa ni taaluma ya mteule husika ili iendane na nafasi ya utendaji
anayopewa.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM), Richard Mbunda alisema: “Anachokifanya Rais ni kuleta sura mpya na
anatumia mtindo mzuri wa kuondoa waliokuwepo na kuwapa nafasi nyingine ili
kuepusha maneno, wakati huo huo akichukua wapya kujaza nafasi hizo.”
Katika uteuzi aliofanya hivi karibuni,
Rais Magufuli aliwateua Naibu
Katibu Mkuu wa CCM Bara, Rajab Luhwavi kuwa balozi sambamba na Dk Emmanuel
Nchimbi, Dk Pindi Chana na Dk Asha Rose-Migiro ambao walikuwa wajumbe wa Kamati
Kuu ya Chama hicho.
Dk
Migiro baada ya kuteuliwa kuwa balozi wa Uingereza, nafasi yake ilikaimiwa na
Dk Chana ambaye naye ameteuliwa kuwa balozi, jambo linaloashiria kufanyika
uteuzi wa sura mpya kuziba nafasi hizo.
“Kuhusu nani na nani watateuliwa hilo
siwezi kulieleza kiundani, ila kuna uwezekano kukawa na mabadiliko,”
alisisitiza Mbunda.
Sekretarieti
Uchambuzi huru unaonesha kuwa Rais Magufuli
atafanya mabadiliko kwenye Baraza lake la mawaziri iwapo ataamua kuteua wajumbe
wa Sekretarieti ya CCM kutoka miongoni mwa mawaziri wake hasa nafasi za Katibu
Mkuu, Naibu Katibu Mkuu.
Tayari Sekretarieti ya CCM ikiongozwa na
Katibu Mkuu wake Abdulrahman Kinana ilishaomba kupumzika, lakini Mwenyekiti wa
chama hicho, Rais Magufuli akaiteua tena bila kufanya mabadiliko na kuiomba
iendelee na kazi.
Kinana na timu yake waliomba kupumzika
Julai, katika Mkutano Mkuu Maalumu
wa CCM, Dodoma ambao ulimchagua Rais Magufuli kuwa Mwenyekiti, akipokea
kijiti kutoa kwa, Rais mstaafu Jakaya Kikwete.
Tayari wanaCCM kadhaa wakiwamo mawaziri
wanatajwa huenda wakaingia katika Sekretarieti mpya ya chama hicho, ambayo duru
za kisiasa zinabashiri itawekwa wazi wiki ijayo, baada ya kumalizika kwa vikao
vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu vinavyotarajiwa kuanza Jumapili.
Wanaotajwa kuunda timu hiyo mpya ya CCM
ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi anayetajwa
kuweza kuwa Katibu Mkuu wa CCM, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Humphrey Polepole wanaotajwa huenda mmoja wao
akarithi mikoba ya Nape Nnauye ya Katibu wa Itikadi na Uenezi.
Wengine ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos
Makala na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi, Abdallah Bulembo.
Aliyekuwa Msemaji wa CCM, Christopher ole
Sendeka ni miongoni mwa waliotajwa kuingia katika sekretarieti hiyo.
Utendaji wa mawaziri
Rais Magufuli pia anaweza kufanya
mabadiliko ya Baraza kwani muda huo unatosha kufahamu yupi anakwenda vizuri au
anayehitaji kubadilishwa.
Akiunda Baraza lake Rais alitangaza
kuunda wizara 18 zenye mawaziri 19 na naibu 16, huku sita kati yao wakiwa
wanawake na tayari alishafanya mabadiliko kwa kutengua uteuzi wa aliyekuwa
Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga kisha kumteua Mwigulu Nchemba
aliyekuwa Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo kushika wadhifa huo.
Kupitia mabadiliko hayo, Rais alimteua
Dk Charles Tizeba kuziba nafasi ya Mwigulu.
Katika mwaka mmoja wa utawala wake, Rais
Magufuli alimwacha waziri mmoja, kuhamisha mmoja na kuteua mmoja wakati
mtangulizi wake, Kikwete alihamisha mawaziri 18.
0 comments:
Post a Comment