Wengi wataka maovu ya Serikali yaanikwe


Celina Mathew

Twaweza
UTAFITI uliofanywa na taasisi ya Twaweza baada ya Rais John Magufuli kusaini Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, unaonesha kuwa watu 19 kati ya 20 sawa na asilimia 95, wanataka vyombo vya habari viripoti maovu ya Serikali iliyo madarakani.

Utafiti huo ni kama umejibu wa taasisi ya Afrobarometer uliofanyika kati ya mwaka 2013 na 2014, ambao ulionesha theluthi mbili ya wananchi sawa na asilimia 65 walitaka vyombo hivyo kuripoti maovu hayo.

Rais Magufuli alisaini Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, Novemba 16 baada ya kupitishwa na Bunge la 11 katika mkutano wake wa tano Dodoma, akisisitiza kuwa itasaidia kuboresha sekta ya habari kwa manufaa ya wana taaluma na Taifa.

Lakini akitangaza matokeo ya utafiti wao jana Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze alisema takwimu hizo ni matokeo ya utafiti uliofanyika baada ya kusainiwa kwa sheria hiyo.

Alisema takwimu zilizotumika katika utafiti huo zinatoka katika vyanzo viwili; sauti za wananchi, uwakilishi wa kitaifa unaotumia simu za mkononi, vyote kutoka Tanzania Bara.

Katika ufafanuzi wake, Eyakuze alisema mwaka huu umegubikwa na changamoto dhidi ya haki za kiraia za kupata taarifa na kutoa maoni yao kwa uhuru, sambamba na  matangazo mbashara ya Bunge kupitia televisheni na redio kusitishwa, jambo ambalo wananchi wamekuwa wakilidai kila uchwao.

“Wananchi wengi wanatambua uhuru wa kupata taarifa. Wananchi wanane kati ya 10 sawa na asilimia 79 wanapinga uamuzi wa Serikali wa kusitisha matangazo ya Bunge ya moja kwa moja,” alisema.

Aliongeza: “Pia wananchi tisa kati ya 10 sawa na asilimia 92 wanasema ni muhimu matangazo ya Bunge yakarushwa mbashara kupitia luninga na redio. Wananchi tisa kati ya 10 sawa na asilimia 88 wakisema gharama isitumike kama sababu ya kusitisha matangazo hayo.”

Alifafanua, kwamba wananchi wanane kati ya 10 sawa na asilimia 80 walisema uhuru wa kupata taarifa ungesaidia kupunguza vitendo vya rushwa, idadi kama hiyo wanaunga mkono wananchi kupata taarifa za Serikali.

Kuhusu sheria hiyo, alisema Watanzania kadhaa wamechukuliwa hatua kali chini ya sheria ya uhalifu wa mitandao kwa kosa la kutoa maoni yao.

“Vilevile mwaka huu ndipo sheria kandamizi ya Huduma za Habari ilipitishwa na Bunge na kusainiwa na Rais,” alisema.

Alisema takwimu hizo zinaonesha, kwamba wananchi wanathamini sana nguzo kuu tatu za demokrasia imara, uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa maoni na haki ya kupata taarifa.

Aliongeza kuwa wananchi pia wana uelewa mpana juu ya madhara ya kuminywa kwa haki hizo muhimu kwa raia, wanaelewa umuhimu wa kuwa na vyombo vya habari visivyokaliwa kooni.

Alisema ni vema maoni ya wananchi yaheshimiwe na kwamba busara, hekima, uamuzi sahihi usio na upendeleo pamoja na fikra chanya, vitaongoza utekelezaji wa sheria hiyo ya huduma za vyombo vya habari.

Aliongeza kuwa kutokana na takwimu hizo wanaiomba Serikali ifanye busara, kwa kutozidisha makali katika utekelezaji wa sheria hiyo, ili kupunguza uminywaji wa vyombo vya habari.

“Kwa kuwa taarifa za kuikosoa Serikali zitapungua hali hiyo itasababisha umasikini wa wananchi kutokuwa na uwezo wa kujua Serikali inafanya nini na rasilimali zao,” alisema Eyakuze.

Eyakuze ambaye aliainisha utafiti wa Afrobarometer, alisema unaonesha kuwa asilimia 65 wanataka maovu ya Serikali yaoneshwe, asilimia 31 wanasema utoaji wa taarifa hizo utaiathiri nchi.

Pia, alisema wananchi wanane kati ya 10 ambao ni asilimia 75 wanasema vyombo vya habari vinafanya kazi nzuri ya kufichua maovu na rushwa, huku wananchi wawili kati ya kumi (18%) wakisema havifanyi kazi vizuri.

Kwa upande wa uhuru wa kutangaza habari, asilimia 53 wanasema vyombo vya habari viwe huru kutangaza habari yoyote huku asilimia 44 wakisema Serikali iwe na mamlaka ya kufungia magazeti yanapochapisha habari zinazoikera Serikali.

Vilevile, asilimia 65 wanasema vyombo vya habari havijawahi au kama vimewahi ni mara chache sana, kutumia vibaya uhuru wao kwa kutangaza vitu vya uongo.

Alisema takwimu za sauti za wananchi za hivi karibuni zinaonesha asilimia 69 walichagua demokrasia kuliko aina nyingine ya Serikali.

Alisema uungwaji huo mkono wa demokrasia pia unadhihirika kupitia takwimu za Afrobarometer (mwaka 2014) zinaonesha asilimia 79 ya wananchi wanasema Serikali inayoongoza kidemokrasia ndiyo wanayoipenda huku asilimia 81 wakisema ni vema wachague viongozi wao kupitia uchaguzi huru.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo