Mery Kitosio, Arusha
Egon Kochanke |
SERIKALI ya Ujerumani kupitia shirika lake la maendeleo
ya kimataifa (GIZ), imetoa euro milioni 7 sawa na wastani wa Sh bilioni 16.8,
kwa ajili ya kuwekeza kwenye miradi miwili nchini.
Miradi hiyo ni pamoja na wa kusaidia kupambana na
magonjwa ya kuambukiza na kwenye teknolojia ya habari na mawasiliano katika
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Akizungumza kwenye hafla ya kuwekeana saini mkataba huo
juzi, Balozi wa Ujerumani nchini, Egon Kochanke, alisema msaada huo unalenga
kuboresha na kuimarisha uhusiano kati ya nchi yake na EAC ili kuboresha maisha
ya wananchi wa eneo hilo.
Alisema kati ya fedha hizo, euro milioni 3 (Sh bilioni
7.2), zitawekezwa kwenye mradi wa kupambana na magonjwa ya kuambukiza ili
kukabiliana na vifo vinavyotokana na magonjwa hayo.
“Euro milioni 4 (Sh bilioni9.6), zitakwenda kwenye
teknolojia ya habari na mawasiliano ili kuendesha mafunzo kwenye vyuo vikuu vya
Afrika Mashariki na kuongeza ujuzi kwenye sekta mbalimbali,” alisema Kochanke.
Alifafanua: “Serikali yetu ya Ujerumani tumeamua kutoa
msaada huu kwa Jumuiya hii, ili kuendeleza uhusiano kati yetu na EAC na hizi
fedha zitawekwa kwenye miradi itakayosaidia wananchi wa Jumuiya hii kupambana
na magonjwa yanayoambukiza.”
Akizungumza baada ya kusaini, Katibu Mkuu wa EAC, Liberet
Mfumukeko aliishukuru Ujerumani kwa msaada wake na kwamba wamefaidika nao,
kwani utafanya wananchi kuondokana na changamoto hasa kwenye kupambana na
magonjwa.
“Tangu ushirikiano uanze mwaka 1998 Ujerumani imetoa
zaidi ya euro milioni 240 (Sh bilioni 567) kwa EAC, hivyo ni vema wadau wengine
wakaiga mfano wa Ujerumani ili kuunga mkono jitihada za kuleta maendeleo kwa
nchi za EAC,” alisema Mfumukeko.
0 comments:
Post a Comment