Celina Mathew
Zitto Kabwe |
KIONGOZI Mkuu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, ametetea msimamo
wa aliyekuwa Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru, kuweka fedha za umma kwenye
akaunti za muda maalumu katika benki za biashara, kuwa husaidia kuongezea
mapato mashirika ya umma.
Zitto aliyezungumza na mwandishi wa gazeti hili jana,
alisema kuhamishia fedha hizo kutoka benki za biashara na kuzipeleka Benki Kuu
ya Tanzania (BoT), kutasababisha
mashirika ya umma kupoteza baadhi ya mapato.
Kiongozi huyo aliyepata kuongoza Kamati ya Bunge ya Fedha
za Mashirika ya Umma kwa muda mrefu, alisema katika vyanzo vya mapato vya
mashirika ya umma, riba kwenye miamala ya akaunti za muda maalumu za benki ni
sehemu ya mapato.
Alifafanua kuwa, kwa kawaida miamala hiyo ikiwekwa BoT au
Hazina, badala ya akaunti hizo za benki za biashara, hazipati faida kwa kuwa
hazitoi riba maalumu.
Zitto aliongeza kuwa hata kwenye nchi zingine duniani,
fedha za mashirika ya umma huwekwa kwenye akaunti za muda maalumu za benki za biashara, kwa kuwa ndivyo uchumi
unavyoendeshwa.
Alisisitiza, kuwa kama Mafuru kuruhusu baadhi ya
mashirika ya umma kuweka fedha kwenye akaunti za muda maalumu ndiyo sababu ya
kuondolewa wadhifa wake, ni vema ieleweke kuwa hakuvunja sheria.
Mafuru aliondolewa kwenye nafasi hiyo, siku chache baada
ya kutoa kauli kwamba hakuna tatizo kwa taasisi za Serikali kuweka fedha kwenye
akaunti za muda maalumu, ambayo ilipingana na ya Rais John Magufuli.
Dk Magufuli akielezea sababu za kuvunja Bodi ya Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA), kuwa kuruhusu fedha za umma kuwekwa kwenye akaunti za
muda maalumu kwenye benki tatu za biashara.
Miongoni mwa wajumbe wa Bodi iliyovunjwa ni Mafuru,
mwingine aliyetoa kauli ya kufanana na hiyo, ambaye pia ni mjumbe wa Bodi ya TRA
iliyovunjwa, ni Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu.
0 comments:
Post a Comment