Joyce Anael, Moshi
KANISA la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), limepongeza
ukali wa Rais John Magufuli, kwa maelezo kuwa umesaidia kupatia ufumbuzi baadhi
ya changamoto ambazo awali zilionekana haziwezekani.
Mkuu wa KKKT nchini, Askofu Fredrick Shoo alisema
hayo jana mjini hapa kwenye harambee ya kuchangia ujenzi wa wodi ya wagonjwa wa
saratani ya Hospitali ya Rufaa ya KCMC, iliyoongozwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.
Dk Shoo alisema pamoja na kinachoonekana kuwa ni
mkali, lakini ameonesha ana uchungu na wananchi wake na Taifa kwa jumla.
Aidha, alisema yale ambayo awali yalionekana
hayawezekani kabisa, baadhi yao ameyafanya au kuyatafutia ufumbuzi katika mwaka
mmoja wa uongozi wake na kutaka Watanzania kumwombea na Serikali yake, ili
kufika kwenye malengo.
Dk Shoo ambaye pia ni Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini
ya KKKT, alisema yapo mambo mengi mazuri yamefanywa na Rais Magufuli katika
mwaka mmoja, hivyo anahitaji pongezi na kuungwa mkono.
“Ndugu Waziri, nakuomba mpelekee Rais Magufuli
pongezi zetu za dhati, mwambie Kanisa linaona na linafuatilia juhudi anazofanya
kwa ajili ya Taifa letu,” alisema.
Alisema juhudi za Rais zina mwelekeo wa kujali
Watanzania wengi, hivyo anastahili kuungwa mkono ili kufikia malengo kusudiwa.
Dk Shoo alisema pamoja na kinachoonekana kuwa
mkali, ukweli kuhusu utendaji wake unaonesha wazi kuwa ukali huo unatokana kuwa
na uchungu na wananchi wake na Taifa pia.
Akizungumzia kitengo kipya cha tiba kwa wagonjwa wa
saratani hospitalini hapo, Dk Shoo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Shirika la Msamaria
Mwema linalomiliki na kuendesha KCMC, alisema kitakuwa mkombozi kwa wananchi
wengi wa Kanda ya Kaskazini ambao walilazimika kusafiri hadi Dar es Salaam au
Mwanza kutafuta tiba ya ugonjwa huo.
Alilipongeza shirika la FCCT la Marekani kwa msaada
mkubwa lililoutoa na linaoendelea kutoa kwenye huduma hiyo mpya hospitalini
hapo.
Waziri Mwalimu alisema Serikali itaendelea kuiunga
mkono KCMC katika kutoa huduma hiyo ambayo ni mchango mkubwa wa kuboresha
huduma za afya kama ilivyo sera ya afya nchini.
Alisema saratani ni changamoto kubwa kwa Taifa,
kutokana na kuongezeka kila mwaka, hivyo
kuna kila sababu ya kuongeza mapambano ya kukabiliana na ugonjwa huo.
Alisema Takwimu zinaonesha kuwapo wagonjwa kati ya
20,000 na 30,000 wa ugonjwa huo nchini na ndiyo sababu Serikali inaliangalia
suala hilo kama changamoto kubwa kwa Taifa.
Aidha, alisema ugonjwa huo pia ni tishio kwa sera
ya Taifa ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda, kutokana na hofu ya kupoteza
Watanzania wengi kwa ugonjwa huo kama hatua za haraka hazitachukuliwa mapema.
Aliongeza kuwa Serikali imepanga mkakati wa
kushughulikia suala la kinga sambamba na tiba ili kuhakikisha wananchi wengi
hawapati magonjwa ili kulinda nguvukazi
ya Taifa ya sasa na ijayo.
Akitoa salamu kwenye hafla hiyo, mwakilishi wa FCCT,
Profesa Mark Jacobson aliishukuru Tanzania kwa kuishirikisha kwenye vita dhidi
ya saratani kupitia KCMC.
Harambee hiyo ilikusanya zaidi ya Sh milioni 200 kwa
ahadi na fedha taslimu, huku Dk Shoo akichangia Sh milioni 15.
0 comments:
Post a Comment