* Amri ya Mahakama ililenga nyumba 5 tu
* Wabomoaji wanogewa na kuvuka mpaka
Stella Kessy
UBOMOAJI nyumba 500 uliofanywa Kivule,
Dar es Salaam hivi karibuni ulifanyika kimakosa kwa kuwa zilizotakiwa
kubomolewa zilikuwa ni tano tu.
Kutokana na zahama hiyo, wakazi
waliiovunjiwa nyumba hizo kimakosa wamepanga kwenda Mahakama Kuu kufungua kesi
ya madai.
Uamuzi wa wakazi hao, unakuja siku
chache baada bomobomoa hiyo, huku ikielezwa kuwa hati ya Mahakama iliyotoa idhini
ya kubomoa nyumba hizo haikulenga nyumba 500.
Chanzo cha bomoabomoa hiyo ni mgogoro
kati ya wananchi wa eneo ilo pamoja na Umoja wa Vijana wa Kikristo Tanzania
(Uvikiuta) ambao unadai kuwa mmiliki halali wa eneo ilo.
Akizungumza kwa niaba ya wakazi hao jana,
Diwani wa Kivule, Wilson Molel alisema wanakwenda mahakamani kufungua kesi hiyo
ya madai, kwa kuwa nyumba zao zilibomolewa bila hatia na tano zilizopaswa
kubomolewa ziko eneo tofauti na zilikokuwa nyumba hizo.
"Mahakama ya Temeke ilitoa idhini
ya kuvunjwa kwa nyumba tano, lakini badala yake wakavunja nyumba 500, katika
kesi ya msingi pande zote mbili hazikuwa zimesikilizwa, ila ulisikilizwa upande
mmoja ambao ni walalamikaji Uvikiuta," alisema Mollel.
Tukio la kubomolewa kwa nyumba hizo,
lilitokea Novemba 29, ambapo kwa mujibu wa Mollel, alipata taarifa za nyumba
hizo kubomolewa saa 12 asubuhi kutoka kwa wananchi.
Alipofika eneo hilo alihoji sababu za
kubomoa na kuomba kuoneshwa vibali, lakini akakamatwa na askari na kupekekwa Kituo
cha Polisi Maturubai.
Alisema walipofika kituoni hapo, dalali
wa Mahakama alitoa kibali kilichotolewa mwaka 2012 walichooneshwa kwa mbali na
kuomba wakipige picha, lakini wakakataliwa, badala yake wakazingirwa na polisi.
Mollel alisema waliomba kujua utaratibu
wa kisheria kuhusu kubomolewa kwa nyumba hizo kutoka kwa Ofisa Upelelezi wa Temeke
na kujibiwa kuwa kilishatolewa.
Alisema baada ya kuhoji hayo, ndipo
walipogeuziwa kesi na polisi kumpa karatasi Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara
wakimtaka aandike maelezo kwa nini alihamasisha wananchi kushambulia polisi,
akagoma akieleza kuwa anamsubiri mwanasheria wake.
“Viongozi hawana taarifa yoyote zaidi ya
ubabe wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma (Jordan Rugimbana), ndiye aliyefanya jambo
hili, tumepiga simu kwa Mkuu wa Mkoa (Paul Makonda) haikupokewa, Kamanda Simon
Sirro alisema yuko kwenye mkutano, sijui wananchi leo watalala wapi? Kama
utendaji ndio huu ni kosa,” alisema Mollel.
0 comments:
Post a Comment