Celina Mathew
Francois Kanimba |
WAZIRI wa Biashara na Viwanda wa Rwanda,
Francois Kanimba amesema uhusiano wa kibiashara kati ya nchi yake na Tanzania
umeimarika na sasa inapitisha asilimia 70 ya mizigo kwenye bandari ya Dar es
Salaam.
Kanimba alitoa kauli hiyo jana alipotembelea
Bandari hiyo kuona namna inavyofanya kazi na maboresho yaliyofanywa na Rais
John Magufuli kudhibiti upotevu wa mizigo uliokuwapo awali.
Katika maelezo yake, Waziri huyo alisema
kipindi cha nyuma kulikuwa na upotevu mkubwa wa madini na kukiri kuwa kwa sasa umetoweka.
Alisema baada ya changamoto hiyo,
walifanya mazungumzo na watu wa Bandari hiyo kuhakikisha mizigo ya Rwanda inakuwa salama.
“Nimetembelea Bandari hii kuangalia
namna inavyofanya kazi, kwa kiasi kikubwa changamoto hiyo imepungua, japo
ilikuwa na matarajio tofauti na ilikuwa ikitugharimu sana, lakini kwa sasa
ulinzi umeimarika hivyo mizigo inapita salama,”alisema na kuongeza:
“Kuna mabadiliko makubwa na
wafanyabiashara wa Rwanda wanasema Bandari imebadilika kwa kiasi kikubwa na
mizigo yetu inapita kwa asilimia 70.”
Aliongeza kuwa Rwanda na Tanzania zina
mpango wa kuanzisha mfumo wa kuagiza mizigo pamoja ambao kwa kiasi kikubwa utawezesha
mizigo inayotoka nchi hiyo kuwa salama na kufika kwa wakati.
Alisema pia watahakikisha wanaweka
watendaji wazuri na mamlaka zitakazokuwa zinakagua mizigo yakiwamo mashirika ya
viwango ya nchi hizo mbili kwa lengo la kuwezesha soko kuwa kubwa na la
uhakika.
Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda,
Biashara na Uwekezaji nchini, Charles Mwijage alisema Tanzania inashika nafasi
ya 108 kati ya nchi 189 kwenye masuala ya kuhakikisha biashara zinakwenda
vizuri na kwamba hali hiyo, inatokana na ucheleweshwaji wa mizigo kwenye
mipaka, mizani na bandarini.
Alisema awali tulikuwa nafasi ya 139
lakini kwa sasa 132, jambo ambalo bado hakijapungua kitu na kwamba hiyo
inatokana na changamoto hizo, hivyo wataangalia namna ya kufanya maboresho
makubwa kwenye suala hilo ili kuendeleza biashara zilizopo sasa.
0 comments:
Post a Comment