Charles James
Nape Nnauye |
WAKATI wadau wa habari wakihoji sababu za Serikali
kuharakisha kupitisha Sheria ya Huduma za Habari iliyosainiwa hivi karibuni na
Rais John Magufuli, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye
amesema sheria zinatungwa na binadamu, hivyo haziwezi kuwa sahihi kwa asilimia 100.
Waziri alitoa kauli hiyo jana kwenye uzinduzi wa Mkutano
wa Jukwaa la Wahariri (TEF), na kuwataka waandishi wa habari kuondokana na hofu
juu ya sheria hiyo, ili wasiathiri utendaji kazi wao.
Nape alisema upungufu ulio kwenye sheria hiyo unaweza
kujadiliwa na licha ya sheria hiyo kutomridhisha kila mtu, haifanani na
iliyotungwa mwaka 1976.
“Sheria hii mpya ni tofauti sana na ya 1976, hii haimpi
mamlaka makubwa waziri na nilihakikisha baadhi ya vipengele vinawekwa kwenye
kanuni na si sheria, ili baadaye vikionekana kuwa vigumu basi tuweze kujadili
kwa pamoja na kurekebisha.
“Kwa mfano, jambo lililozua mjadala ni la vigezo vya nani
anapaswa kuwa mwandishi kulingana na elimu yake, hilo nimelirudisha kwa wadau
na TEF tushirikiane kuamua vigezo hivyo, hata kama mtaamua kiwe kiwango cha
chini ni nyie wenyewe lakini lengo ni kukuza tasnia ya habari,” alisema.
Alitoa mwito kwa wanahabari kufanya kazi kwa kujiamini
bila hofu na kuwataka kuendelea kukosoa na kuandika maovu yote yanayofanywa na
Serikali, lakini kwa lengo la kujenga si kubomoa na kuvitaka vyombo vya habari
kusaidia wafanyakazi wao kusoma ili kuongeza ufanisi.
Mwenyekiti wa TEF, Theophil Makunga alitaka wanahabari
kutokuwa na hofu, “ tembo akishaanguka hupaswi kumgeuza bali unatakiwa umchinje
hivyo hivyo,” akiwa na maana kuwa tayari sheria imesainiwa hivyo inapaswa
kutumika busara kwenda nayo sawa.
Akitoa salamu za shukrani kwa Waziri, Mhariri Mtendaji Mkuu
wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, Absalom Kibanda alisema si kweli kwamba
wanahabari wana hofu kama Waziri Nape alivyosema bali ipo kwa Serikali na ndiyo
maana wamekuwa wakipambana kutunga sheria mpya tangu mwaka 1993.
Alisema wanahabari makini hawawezi kuwa na hofu yoyote na
kumjibu Nape kuwa si kweli kwamba waandishi wa Tanzania hawajui kuuliza maswali,
bali wanauliza maswali yanayokera na kutolea mfano jinsi Rais mstaafu, Benjamin
Mkapa alivyokasirika baada ya kuulizwa swali la kuudhi na mwandishi wa CNN,
Sebastian Kim mwaka 1999.
“Nimshukuru Waziri na Mkurugenzi wa Maelezo, Hassan Abbas
kwani wamekuwa na ushirikiano mkubwa nasi na kwa hali ilivyo kwenye Serikali
hii, ni wazi tunapaswa kuwaombea waendelee kuwemo mpaka mwisho kutokana na jinsi
wanavyotupambania.
“Kipindi Muswada huu unaandaliwa na sisi tulitakiwa
tuandae wetu halafu tuupeleke, ndivyo ambavyo hata wenzetu Kenya walifanya na
wakafanikiwa, Spika alikuwa tayari kutetea lakini alivyoona tumekaa kimya naye
akakosa la kufanya,” alisema Kibanda.
Katibu wa TEF, Neville Meena alimwomba Waziri kushughulikia
suala la wasemaji wa Serikali kutokana na wengi wao kutokuwa na ufanisi mzuri,
ikiwamo kuchelewa kutoa taarifa kwa wakati, kutokuwa na majibu ya uhakika
wanapotafutwa kutolea ufafanuzi jambo husika.
0 comments:
Post a Comment