Peter Akaro na Lunyamadzo Mlyuka (DSJ)
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam limepiga marufuku ‘disco toto’ kwenye siku kuu ya Maulid na kutaka
wazazi kuwa karibu na watoto wao ili kuhakikisha usalama wao.
Akizungumza jana Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo,
Simon Sirro alisema Jeshi lake kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na
usalama, wamejipanga kuhakikisha siku hiyo ya Jumatatu inakuwa ya utulivu
zaidi.
“Tumejipanga na kutakuwa na makachero kila
kona, doria za miguu, askari kanzu, askari wa mbwa na farasi, Kikosi cha Kutuliza
Fujo (FFU) na magari ya doria ili kuhakikisha amani na usalama unatawala kila
mahali,” alisema Sirro.
Kamishna Sirro aliwataka wazazi na walezi
kufunza watoto wao maadili mema ili kujiepusha na makundi mabaya kama ya Panya
Road, ulevi na vurugu.
“Wazazi tulinde watoto wasizurure ovyo pia
tukielekea maeneo ya starehe, nyumbani tuache ulinzi wa uhakika,” alisema.
Katika hatua nyingine, Jeshi hilo limekamata
watuhumiwa sugu 103 wa makosa mbalimbali Dar es Salaam kuanzia Desemba 2 hadi jana.
Makosa hayo ni pamoja na kucheza kamari,
wizi wa magari, kutengeneza, kunywa na kuuza pombe haramu ya gongo na kueleza
kuwa operesheni hiyo ni endelevu.
Pia Jeshi hilo kupitia kikosi cha usalama
barabarani Kanda Maalumu lilikusanya zaidi ya Sh milioni 400 kupitia
tozo za makosa ya usalama barabarani,
Kiasi hicho kilipatikana kuanzia Desemba 2
hadi juzi ambapo jumla ya makosa 15,053 yaliripotiwa.
0 comments:
Post a Comment