Mwandishi Wetu
MTI mrefu kuliko yote barani Afrika wenye urefu wa meta
81.5 na umri unaokadiriwa kuzidi miaka 600, umegundulika Tanzania katika bonde
nje ya Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa).
Ugunduzi huo ni wa mtafiti wa Chuo Kikuu cha Bayreuth,
Ujerumani, Andreas Hemp na kutangazwa hivi karibuni, baada ya kufanya utafiti
wa uoto wa asili katika hifadhi hiyo miaka 20 iliyopita.
Hata hivyo, kwenye utafiti huo miaka hiyo, hakufanikiwa
kufika eneo ulipo mti huo unaotajwa kuwa aina ya Entandrophragma
excelsum, kutokana na umbali na tekinolojia aliyokuwa nayo hadi
mwaka 2012 aliporejea kufanya kutafiti tena, akiwa na jopo la watafiti wenzake
na teknolojia ya kisasa ya kupima urefu wa miti.
Taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa Mother Nature
Network (MNN) Novemba 27, ilieleza kuwa Hemp akishirikiana na jopo la watafiti
hao wa chuo hicho, waligundua mti huo.
Katika utafiti huo, watafiti walipima miti 32 kati ya mwaka
2012 na mwaka huu kwa teknolojia ya kisasa, wakapata miti 10 yenye urefu unaoanzia
meta 59.2 na kufanikiwa kupata huo wa meta 81.5, ambao ndio huo ulioweka rekodi
ya Afrika.
Kabla ya ugunduzi huo, mti uliokuwa ukishika rekodi hiyo ni
aina ya Sydney blue gum (Eucalyptus saligna) uliokuwa Limpopo, Afrika Kusini,
ambao hata hivyo ulianguka mwaka 2006.
Inadaiwa kuwa mti mrefu kuliko yote duniani uko
California, Marekani wenye meta 115.7 na wa pili uko Tasmania, Australia, ukiwa
na meta 99.8.
Mti wa tatu kwa urefu uko California pia, una meta 94.9, ukifuatiwa
na wa nne ulioko Tasmania, wenye urefu wa meta 89.0. Wa tano kwa urefu uko kisiwa
cha Mindanao, Ufilipino na wa sita kwa urefu duniani ndio huo wa Tanzania.
Ilielezwa kuwa Afrika hakuna taarifa za uwepo wa miti
mingi mirefu na yenye umri mrefu, kutokana na upungufu wa utafiti katika Bara
hilo, unaosababisha miti mingi kutofanyiwa vipimo na hali ya umasikini wa Bara
hilo, unaochangia miti mingi kukosa fursa ya kurefuka.
Hata hivyo, hali hiyo inaelezwa kutokuwapo Kinapa, ambayo
ina udongo wenye rutuba inayotokana na asili ya volcano, unaoelezwa kuchangia kukua
kwa mti huo.
“Ni kama Jiji katikati ya msitu,” alisema Hemp, alipokuwa
akielezea mazingira ya mti huo na mingine iliyofanyiwa vipimo.
Hemp alitaja sifa nyingine iliyochangia kurefuka kwa mti
huo kuwa ni kuwa mbali na wakataji magogo, ambao wamekuwa wakiharibu mazao ya
misitu kwingineko.
Hata hivyo, mtafiti huyo alihadharisha kuwa miti hiyo iko
nje ya mpaka wa Kinapa, hali inayoonesha kuwa bado iko hatarini na kueleza
matarajio yake, kuwa ugunduzi huo huenda ukasababisha kuongezwa kwa mipaka ya
hifadhi hiyo, ili kulinda mti huo.
Ni jukumu la Serikali na vyombo vyake na wananchi
kuilinda hazina hiyo ambayo inaweza kuchangia mapato kupitia sekta ya utalii.
0 comments:
Post a Comment