Lema kula Krismasi na Mwaka Mpya gerezani


*Mahakama Kuu yafutilia mbali rufaa yake
*Awambia mawakili wasihangaike atasota tu

Seif Mangwangi, Arusha

Godbless Lema
HATIMAYE Mahakama Kuu Kanda ya Arusha imeifutilia mbali rufaa iliyokatwa na mawakili wa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, kupinga kunyimwa dhamana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, baada ya kudaiwa kumtukana Rais John Magufuli.

Akisoma uamuzi mdogo wa Jaji Fatuma Masengi jana, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Angelo Rumisha alisema Mahakama imeifuta rufaa hiyo, kutokana na kuikata nje ya muda.

Rumisha alisema waomba rufaa walitakiwa kuonesha kusudio la kukata rufaa ndani ya siku 10 tangu uamuzi wa maombi ya marejeo kutupwa na Mahakama Kuu, yaliyokuwa mbele ya Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Sekela Moshi Novemba 11.

"Mwomba rufaa hii, Lema kupitia mawakili wake alitakiwa kuonesha kusudio au kutoa notisi ya kuonesha Mahakama sababu ya kukata rufaa na Novemba 21 walipaswa kukata rufaa lakini wao walikata Novemba 22 nje ya muda wa kukata rufaa,” alisema na kuongeza:

"Kutokana na upungufu huo wa kisheria, Mahakama imekubaliana na upande wa pingamizi la upande wa Serikali kupitia kwa Wakili Paul Kadushi akishirikiana na Martenus Marandu, kuwa rufaa hiyo haikufuata misingi ya kisheria kukatwa kwa sababu hakuna kusudio la kukata rufaa, ndipo wakaiomba Mahakama kuitupilia mbali."

Rumisha alisema baada ya pingamizi hilo kutolewa, na upande wa Lema kuomba Mahakama ilitupilie mbali kwani rufaa yao iko ndani ya muda na iliwasilishwa kwa hati ya dharura, Mahakama ilivyopitia hoja za pande zote mbili iliona rufaa hiyo ililetwa Mahakamani hapo nje ya muda unaotakiwa.

Alisema mbali na nje ya muda, pia wakata rufaa hawakuzingatia sheria inavyotaka, kuwa ukikata rufaa lazima uanze na kutoa siku 10 za kusudio la kukata rufaa, jambo ambalo lilisababisha kufikiwa uamuzi wa kuifutilia mbali rufaa hiyo.

Baada ya Msajili Rumisha kuifuta Rufaa hiyo, wakili wa Lema Adamu Jabir, aliiomba Mahakama itoe angalizo kwa askari wanaokwenda mahakamani hapo kuweka ulinzi, kwani wanawazuia na kuwapekua sehemu nyeti wakiwamo wanawake na hata ndugu wa Mbunge huyo ambaye hawana muda wa kumwona hadi pale tu anapofika mahakamani.

Alisema mteja wao Lema anasikitika kuona hali hiyo ikijitokeza wakati yeye ni Mbunge na kesi inasikilizwa kwenye chumba cha wazi ili kila mmoja asikilize na kujua kinachoendelea.

“Tunasikitika watu wanapigwa, wengine wanazuiwa kuingia mahakamani na tumezungumza zaidi ya mara tatu, lakini hali inaendelea vile vile, ulinzi mkali na kuzuia watu wanaofika kufuatilia kesi ya Mbunge wao na ndugu yao,” alisema.

Alisema hata walioingia walifanya hivyo kwa shida na kwa nguvu kubwa ambayo haikuwa ya lazima na kuomba Mahakama iruhusu watu kuingia kwa wingi na chumba kikiwa kidogo watakaa nje au wawekewe spika za kusikiliza.

Akijibu hoja hiyo, Msajili Rumisha alisema Mahakama ikiruhusu watu wote kwenye kesi hiyo watakaa wapi, chumba ni kidogo na ndiyo sababu watu wanadhibitiwa.

Kuhusu kuweka vipaza sauti Rumisha alisema Mahakama haina bajeti hiyo wala haina fedha za kuweka vipaza sauti, ila kwa kesi ya ubunge tofauti na hiyo, kwani ile ya ubunge ina fungu lake, hivyo wanaweza kufanya lolote, ila kesi hiyo haina fungu, hawawezi kuweka vifaa hivyo.

“Lakini wakija wakakosa kukaa ndani wakakaa nje watasikiaje shauri hili likiendelea? Bora wakae nje huko huko,” alisema.

Alipomaliza, Lema alinyoosha mkono akitaka kuongea, lakini Msajili akamtaka aongee na wakili wake ambaye atawasilisha hoja yake mahakamani hapo.

Hata hivyo, wakati Lema anataka kuzungumza na wakili wake, Msajili aliahirisha kesi hiyo na kunyanyuka akatoka nje na kuashiria kuwa Mahakama imemaliza kazi yake.

Nje ya Mahakama

Akizungumza nje ya Mahakama, Wakili wa Lema, John Mallya alisema walizungumza na mteja wao baada ya uamuzi ya Mahakama akawaomba wasijishughulishe na suala lolote la kukata rufaa, ingawa wao wanaona bado kuna njia za kufanya kwenye Mahakama za juu.

Alisema Lema aliwaambia yuko tayari kukaa gereza la Kisongo bila shida na kuhusu hoja kuwa walikata rufaa nje ya muda, alisema wanafahamu ni ndani ya muda, ila Mahakama ikishatoa uamuzi si rahisi kuukataa, lazima kukubaliana nao, hivyo waliahidi kukutana mawakili wote wa Lema kupanga mbinu za kumpigania kupata haki yake ya dhamana.

Katibu

Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa, alisema chama kimesikitika kuona Mahakama imefuta rufaa yao.

Alisema kimefedheheshwa katika shauri hilo tangu lilipoanza, kwani mara mbili Jaji na Msajili wamekuwa wakitoa maelekezo juu ya Mahakama hiyo ya wazi inayoruhusu watu wote kuhudhuria, lakini haki ya Mbunge na wapiga kura wake imekuwa ikinyimwa kwa kuzuiwa na kutishwa na askari.

Golugwa alisema wananchi wana haki ya kufuatilia shauri la Mbunge wao, lakini baadhi yao wanapigwa na kuumizwa ili wasiingie mahakamani hapo.

Alisema kutokana na maelekezo hayo na mwenendo wa kesi, licha ya kuruhusiwa dhamana, lakini ameendelea kunyimwa, hivyo kuona bora akae Kisongo na hatachukua uamuzi wowote mpaka Jamuhuri itakapoona inafaa atoke.

“Kuhusu hili suala, Chama tutatoa tamko na kueleza mazingira ya kesi hiyo na alichoonesha Msajili na hali hiyo imeonesha kweli kuna kitu, mwenye akili amepata majibu, ila sisi viongozi tumekaa na familia kuwapa moyo wasiogope na familia iko vizuri,” alisema.

Awali mawakili wa Lema akiongozwa na Peter Kibatala, walikata rufaa namba 112/113 ya mwaka 2016 Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, ili kudai haki ya dhamana ya Mbunge huyo aliyonyimwa kutokana na makosa ya kisheria yaliyofanya na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.

Walisema waliamua kufungua maombi ya rufaa kwa ajili ya kujua sababu ya Lema kukosa dhamana ambayo awali Hakimu Desdery Kamugisha alisema iko wazi.

Aidha, walisema sababu ya kufungua rufaa hiyo ni mbili; kwamba hawakuridhishwa na hatua ya Hakimu Kamugisha kumnyima dhamana Lema, huku akijua kuwa alifanya kosa kwa sababu mawakili wa Serikali akiwamo Kadushi, walisema wameonesha nia ya kukata rufaa.

"Tunapinga Lema kunyimwa dhamana iliyo wazi na ndiyo maana tumeamua sasa kukata rufaa na tunasubiri Mahakama Kuu kutupangia Jaji wa kusikiliza maombi ya rufaa yetu,” alisema.

Hali hiyo ilikuja baada ya mawakili wa Serikali wakiongozwa na Kadushi, kupinga dhamana ya Lema, kwa madai kwamba alifanya kosa akiwa amepewa dhamana na Mahakama hiyo.

Pia walidai iwapo Lema atapewa dhamana, kuna hatari ya usalama wa maisha yake.

Akitupilia mbali hoja hizo, Hakimu Kamugisha alisema Mahakama haitoi dhamana kama hisani, bali ni haki ya msingi ya mtuhumiwa, kama ilivyoainishwa kwenye Katiba ya nchi na sheria.

Alisema iwapo mtuhumiwa ananyimwa dhamana, sheria inatakiwa kutamka bayana.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo