Mwandishi Wetu
SHIRIKA la Ndege
la Tanzania (ATCL) limeanza kuachiwa soko la usafiri wa anga, baada ya
mashirika pinzani kufuta safari za baadhi ya maeneo, huku Serikali ikitajwa
kumaliza kusaini ununuzi wa ndege mpya tatu.
Taarifa
zilizopatikana jana, zilieleza kuwa Tanzania imeingia makubaliano ya
ununuzi wa ndege tatu mpya zinazotengenezwa na kampuni ya Bombardier ya Canada,
ikiwemo moja aina ya Q400NG, inayofanana na mbili zilizozinduliwa na Rais John
Magufuli, Septemba.
Kwa mujibu wa taarifa hizo kutoka Bombardier, ambazo ziliripotiwa
kwenye mitandao ya kijamii jana, ndege zingine mbili ni aina ya CS300, ambazo
ni toleo jipya la ndege za Bombardier na kila moja ina uwezo wa kubeba abiria
kati ya 100 na 150.
Ndege hizo aina ya CS300, zinatajwa kuongoza kwa sifa ya
matumizi madogo ya mafuta kwa safari ndefu, ambazo zinatarajiwa kufufua safari
za ATCL katika nchi mbalimbali za Afrika na nje ya Afrika.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Tanzania ndiyo nchi ya kwanza
kuagiza CS300 katika nchi za Afrika, baada ya hivi karibuni kampuni hiyo kuuza
ndege hizo kwa Shirika la Ndege la Baltic na Swiss, ambayo ni mashirika yaliyo
chini ya mwavuli wa Kundi la Mashirika ya Ndege ya Lufthansa.
Hivi karibuni, Rais
Magufuli akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari, Ikulu Dar es Salaam,
aliahidi ununuzi wa ndege hizo ambapo alisema alishalipia asilimia 30 na zinatarajiwa kufika nchini mwanzoni mwa mwaka 2018.
Rais Magufuli alitaja pia
mpango mwingine wa kununua ndege aina ya Boeing, yenye uwezo wa kubeba abiria
242, ambayo kabla ya mchakato wa ununuzi kuanza, Serikali ilitakiwa kulipa dola
za Marekani milioni 10, ambazo zimeshalipwa, hivyo mazungumzo ya awali
yangeanza.
Taarifa ya jana ilieleza kuwa
ndege inayozungumzwa ni aina ya Boeing B787 Dreamliner, ambayo mazungumzo ya ununuzi wake yameanza.
Inatarajiwa ununuzi wa
ndege hizo, utasaidia ATCL kuanza safari za nje ya Afrika, baada ya
Bombardier Q400NG, zilizopo nchini kuanza safari za baadhi ya nchi jirani.
Kuachiwa soko
Ununuzi huo wa ndege mpya umetajwa kufanyika kwa wakati
mwafaka, wakati washindani katika biashara ya usafiri wa anga, Precision Air na Fastjet, wakitangaza
kupata hasara na kupunguza safari za baadhi ya miji, huku hatua za kuahirisha
safari zikichukuliwa mara kwa mara.
Miongoni mwa masoko ambayo imeelezwa kuwa ATCL ni kama
imeanza kuachiwa ni pamoja na za Dar es
Salaam- Entebbe na Nairobi, ambazo wachambuzi wa mambo walieleza kuwa ni soko
ambalo halikutarajiwa, lakini linaloweza kukamatwa na shirika hilo kwa kutumia
ndege zake ndogo, ambazo zina sifa ya matumizi madogo ya mafuta.
Hatua hizo za ATCL zilifananishwa na zinazochukuliwa na
Serikali ya Rwanda kupitia RwandAir, ambayo imeamua kununua ndege mbili aina ya
Airbus A330.
Hata hivyo, ilielezwa kuwa hali hiyo huenda ikazorotesha
jitihada za kufufua Air Uganda kwa kuwa soko la Afrika Mashariki, limeanza
kujaa kutokana na nguvu za Shirika la Ndege la Kenya (KQ).
Ilielezwa kuwa kuibuka kwa RwandAir inayoonekana kuwa shirika
linalojiamini na linalokua kwa kasi kiasi cha kuhudumia Uganda na kufufuliwa
kwa ATCL, ambayo huenda ikapata zaidi ya ndege mpya sita, ikijumlishwa na tatu
zilizopo, kunafanya biashara hiyo ya usafiri wa anga kuwa na ushindani
utakaoathiri kampuni mpya za usafiri wa anga.
0 comments:
Post a Comment