Celina Mathew
Samia Suluhu Hassan |
MAWAZIRI tisa jana kwa mara ya kwanza walikutana
kuelezea mpango mkakati wa wizara zao katika kushughulikia masuala ya ukatili
dhidi ya wanawake na watoto kwa miaka mitano kuanzia 2017 hadi 2022.
Mawaziri hao ni wa Katiba na Sheria,
Harrison Mwakyembe; Kilimo, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Charles Tizeba; Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage; Naibu Nishati na Madini, Dk
Medard Kalemani na wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama,
Wengine ni Naibu Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia, Stela Manyanya, Naibu wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo Anastazia Wambura, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango na wa Mambo
ya Ndani aliyewakilishwa na Naibu Katibu Mkuu wake, Balozi Simba Yahya.
Akizungumza kwa niaba ya Makamu wa Rais,
Samia Suluhu Hassan, ambaye alikuwa mgeni rasmi wakati akizindua mpangokazi wa
taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto ambao ni wa miaka
mitano, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu alisema ni mara ya kwanza kuona masuala ya watoto na wanawake
yanakutanisha mawaziri tisa.
“Ni jambo la faraja sana, kuona masuala
ya watoto yanakutanisha mawaziri tisa pamoja tena meza moja, pia hiyo ni kwa
mara ya kwanza kutokea nchini hivyo najisikia faraja sana kwa niaba ya Samia
ambaye ameshindwa kuhudhuria kutokana na kikao cha Kamati Kuu ya CCM,” alisema
Waziri Mwalimu.
Alisema mpango mkakati huo una lengo
kuwa ifikapo mwaka 2022 matatizo ya ukatili yawe yamepungua kwa asilimia 50 kwa
upande wa wanawake na idadi ya watoto 35,916 kwa asilimia 50.
Alisema kwa kiasi kikubwa ukatili kwa
wanawake na watoto umekuwa ukisababishwa na umasikini wa familia, mila na
desturi potofu zenye athari kwa jamii, malezi na makuzi mabovu na sheria kandamizi
na kwamba kabla ya kuandaliwa, Tanzania ilikuwa na mipango kazi minane ya aina
hiyo.
Alisema Tanzania ni kati ya nchi ya nne
za kwanza duniani na nchi pekee Afrika iliyowezeshwa kupitia jukumu
lililoanzishwa la kuwezesha nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN) kuandaa
mpango huo.
Waziri Mpango alisema mpango kazi huo
utatumia Sh bilioni 267.4 na kwamba utatekelezwa na serikali, sekta binafsi na
wadau huku akiahidi Serikali kuhakikisha fedha hizo zinapatikana haraka.
Mhagama alisema kwa kiasi kikubwa watoto
wanafanyiwa unyanyasaji wakiwamo wenye ulemavu ambao walemavu wamekuwa
wakifungiwa ndani na hivyo kukosa haki ya elimu na afya kwa kujumuika na wenzao
katika michezo.
Mwijage alisema ukatili ni ukiukwaji wa
sheria na haki za binadamu na kutaka wanawake kuacha kulalamika badala yake
wajiingize kwenye viwanda vidogovidogo ili kujiendeleza kijasiriamali.
Tizeba alisema asilimia 78 ya wanawake
wanafanya kazi kwenye kilimo, lakini wanapata kipato kidogo kuliko wanaume
ambao hawafanyi kazi kubwa na kuahidi kuwa suala hilo litafanyiwa kazi.
Dk Mwakyembe alisema Wizara yake
imejipanga kuhakikisha inafanyia marekebisho sheria ya ndoa ambapo itabuni
mchakato usio na gharama ili mwafaka upatinake kukidhi mahitaji.
Manyanya alisema ukatili kwa kiasi
kikubwa umekuwa ukijitokeza shuleni na kwamba Wizara yake imejipanga
kuhakikisha inatoa elimu kwa wananchi kuwa ukatili wa kijinsia kwa watoto na
wanawake si mzuri.
Dk Kalemani alisema kwa kiasi kikubwa
masuala ya ukatili yamekuwa yakifanyika gizani hivyo Wizara yake itahakikisha
inapeleka umeme wa kutosha vijijini hususan shuleni na vituo vya afya.
Balozi Yahya alisema licha ya kuwa
ukatili ni kosa la jinai, bado vitendo hivyo haviripotiwi kwenye vyombo vya
habari huku takwimu za Polisi zikionesha kuwa kesi 42,538 ziliripotiwa, 4,268
zilifungwa huku 15,575 zikiendelea tangu mwaka 2012.
0 comments:
Post a Comment