Jemah Makamba
Kamishna Valentino Mlowola |
MAOFISA Kodi Wasaidizi Liberatus
Ligumasi (30) na Kenes Mawele (29)
wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja
na mfanyakazi Nassoro Saidi (42) wamefikishwa kwenye Mahakama ya Wilaya ya Ilala, wakishtakiwa na Taasisi ya Kuzuia
na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa tuhuma za kuomba rushwa kwa mfanyabiashara,
Humphrey Lema.
Katika mashitaka yaliyoongozwa na
wawakilishi upande wa Jamhuri kutoka Takukuru, Mwakatobe akisaidiwa na Sophia
Gura mbele ya Hakimu Adelf Sachore, walidai kuwa katika tarehe tofauti washitakiwa
waliomba rushwa huku wakijua ni kosa na kinyume cha sheria za taratibu za nchi.
Mwakatobe alidai kuwa katika mashitaka
ya kwanza yanawahusu maofisa kodi ambao ni mshitakiwa namba moja na namba mbili
ambapo Novemba 18, Ofisi za TRA zilizo Kariakoo waliomba rushwa ya Sh milioni 50
kwa mfanyabiashara huyo, ili wampunguzie kodi ya mapato ya biashara zake.
Katika mashitaka ya pili yanayohusu maofisa
kodi hao Novemba 23, katika duka la kubadilishia fedha lililo kwenye hoteli ya
Cate, Kariakoo, walimwomba mfanyabiashara huyo Sh milioni 10 ili wampunguzie
kodi.
Kwenye mashitaka ya tatu yanayohusu wote
watatu, ilidaiwa kuwa Desemba mosi katika ofisi za TRA za Kariakoo walijipatia dola 2,754 za Marekani kutoka kwa
mfanyabiashara huyo, wakidai kumpunguzia kodi.
Ilidaiwa mahakamani kuwa upelelezi
haujakamilika, hivyo upande wa Jamhuri ulimwomba Hakimu awapangie siku nyingine
ili kuja kuona kama upelelezi umekamilika.
Hakimu alisema dhamana ya kesi hiyo iko
wazi kama washitakiwa watakidhi masharti watakayopewa na kama watashindwa
watarudi rumande.
Sachore aliwapa masharti ya dhamana ambayo
ni kuwa na wadhamini wawili wanaofanya kazi katika taasisi inayofahamika
watakaosaini bondi ya Sh milioni mbili kwa kila mmoja na kuambatanisha barua za
sehemu wanakofanyia kazi.
Mshitakiwa wa pili alipata dhamana huku wa
kwanza na wa tatu wakishindwa kukidhi masharti, hivyo kurudishwa rumande hadi
Desemba 27 kesi hiyo itakapotajwa.
0 comments:
Post a Comment