Fidelis Butahe
Dk Emmanuel Nchimbi |
BALOZI mteule na mbunge wa zamani wa
Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher ole
Sendeka jana walitumia mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM
uliofanyika Ikulu, Dar es Salaam, kutoboa siri ya imani waliyonayo kwa Rais John
Magufuli.
Wana CCM hao walitoa yao ya moyoni
walipopewa nafasi ya dakika moja kila mmoja pamoja na wana CCM wengine
walioteuliwa na Rais Magufuli kuwa mabalozi.
Akitoa neno kwenye mkutano huo, Nchimbi
ambaye Julai 10 mwaka jana akiwa na wenzake wawili walijitokeza hadharani kutangaza
kujitenga na uamuzi wa Kamati Kuu ya chama hicho, baada ya kutangaza majina
matano ya waliowania kuteuliwa na CCM kugombea urais, likiwamo la Rais huyo, alisema
Dk Magufuli akiwa Waziri wa Ujenzi na baadaye Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, alifanya makubwa kwa Umoja wa Vijana wa Chama hicho (UVCCM).
Kada huyo aliyeanza kukitumikia chama
hicho tangu akiwa na umri wa miaka 10 ngazi ya chipukizi, alikuwa miongoni mwa
wateule watano wa Rais Magufuli waliopewa nafasi na Katibu Mkuu, Abdulrahman
Kinana kuaga wajumbe wa mkutano huo baada ya hivi karibuni kuteuliwa kuwa
mabalozi.
Wengine waliozungumza kwenye mkutano huo
ni aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Bara, Rajab Luhwavi, Dk Pindi Chana, Omary Yusuf
Mzee (wote mabalozi) na Sendeka ambaye pia alikuwa Msemaji wa CCM.
Katika salamu zake, Dk Nchimbi aliomba
azungumze kwa dakika mbili badala ya moja aliyopewa na Kinana akibainisha: “Nimekuwa
mjumbe wa NEC kwa miaka 19 na mjumbe wa Kamati Kuu kwa miaka 14. Nilianza kuwa
Mwenyekiti wa chipukizi katika ngazi ya mkoa nikiwa na umri wa miaka 10, nina
matumaini makubwa na uongozi wako, nina ushahidi wa moja kwa moja.”\
Aliongeza: “Kwanza, mradi mkubwa kuliko
yote ya chama chetu, jengo la vijana CCM. Hati ya kiwanja cha Umoja wa Vijana
ilitapeliwa wakati (Rais Magufuli) ukiwa Waziri wa Ujenzi, nilikuja kukuona
ukatusaidia tukaikomboa. Tusingekuwa na jengo lile bila wewe.”
Alisema kibali cha kujenga eneo hilo kilieleza
kuwa zilitakiwa kujengwa ghorofa nane, lakini baada ya kuhangaika kwa takribani
mwaka mmoja, walikwenda kumwomba Rais Magufuli na kubadili kibali hicho kwa saa
24 tu.
“Hayo ndio yanayonipa matumaini makubwa
kwa chama chetu, kwamba kama ulikuwa Waziri wa Ardhi na kufanya makubwa vile,
je ukiwa Rais na Mwenyekiti wa Chama chetu, mambo yatakuwa makubwa zaidi,”
alisema Dk Nchimbi.
Sendeka alisema: “Baada ya kumteua Nape
Nnauye kuwa Waziri, wewe Mwenyekiti (Rais Magufuli) na Kikwete (Jakaya-Rais
mstaafu) na makamu wako wawili na Katibu Mkuu mliniita nikiwa Simanjiro na kunitaka
niwe Msemaji wa chama.
“Juzi tu hapa umeniamini na kuniteua
kuwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe. Nakushukuru wewe na wasaidizi wako waliokushauri.
Sijui kazi nyingine, nimekulia CCM maana serikalini nilifanya kazi miaka mitatu
tu.”
Sendeka aliwatania wenzake walioteuliwa
kuwa mabalozi kuwa wao hawatakuwa wakivaa sare za chama hicho, lakini yeye kwa
nafasi yake, ataendelea kuvaa sare hizo, “hawa uliowateua watakuwa wakivaa suti
tu huko watakakoenda.”
0 comments:
Post a Comment