Suleiman Msuya
Dk. John Magufuli |
RIPOTI ya Mtazamo wa Hali ya Haki za Kiraia
na Kisiasa Tanzania 2016, imebainisha mambo matano makubwa yaliyotikisa mwaka
huu unaofikia ukingoni Desemba 31.
Ripoti hiyo ambayo imeandaliwa na Kituo
cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar,
imetaja mambo hayo kuwa ni pamoja na sheria mpya ya huduma za habari, uzuiaji holela
wa mikutano ya kisiasa na Serikali kuwalinda wazee na watu wenye ulemavu hasa
wenye ualbinism.
Matukio mengine ni uamuzi ya Mahakama
dhidi ya mauji yanayofanywa na vyombo vya dola na ajenda ya matukio ya wananchi
kujichukulia sheria mkononi.
Ripoti hiyo imeeleza pia kuwa Tanzania
imeshuka katika viwango vya uhuru vya kimataifa kutoka asilimia tatu hadi asilimia
3.5, ikiwa ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 20 iliyopita.
Imebainisha kuwa kushuka huko kunatokana
na kutungwa kwa Sheria ya Takwimu na Sheria ya Makosa ya Mtandao za mwaka 2015
ambazo zinaathiri utendaji wa vyombo vya habari, taasisi za kielimu na asasi za
kiraia.
Aidha, ripoti hiyo inabainisha kuwa
kutungwa kwa sheria zingine kunaweza kushusha zaidi alama zilizopo pamoja na
kwamba taasisi ya utafiti huo haijatoa taarifa ya mwaka 2016.
Ripoti hiyo inaonesha kuwa matukio
ambayo yametokea katika kipindi cha mwaka 2016 hayaoneshi matumaini ya haki
hiyo kupata alama nzuri, huku utendaji wa watawala katika kipindi hiki
ukionesha kuathirika.
Eneo la pili katika matukio hayo makubwa
ni uzuiaji holela wa mikutano ya kisiasa ambapo ripoti inabainisha kuwa hatua
hiyo inakiuka haki ya watu kukusanyika ambayo inatolewa na Katiba.
Ripoti hiyo imebainisha kuwa katika
kuzuia mikutano hiyo kuna maamuzi ambayo yalikuwa yanatolewa bila kufuata
utaratibu na hakukuwa na sababu za msingi za kufanya hivyo, hali ambayo
ilisababisha kuwepo kwa shaka juu ya nia ya uzuiaji huo.
“Mwaka 2016 Rais John Magufuli alitoa
pendekezo la kuzuia mikutano hadi 2020 ambapo Jeshi la Polisi na baadhi ya
viongozi walilitafsiri kuwa ni kupiga marufuku mikutano ya kisiasa ya ndani na
hadhara ikiwemo Ukuta,” ilisema ripoti hiyo.
Aidha, ripoti inaendelea kusema kuwa
pamoja na katazo hilo kuondolewa, bado kuna maeneo ambayo polisi inaendelea
kuzuia.
Mwenendo chanya wa Serikali kuchukua
hatua kuwalinda wazee na watu wenye ualbino ni moja ya eneo ambalo limetajwa na
ripoti hiyo kuwa Serikali kwa mwaka huu imechukua hatua muhimu kukabiliana
nalo.
Ripoti hiyo inasema kuwa Serikali
imefanikiwa kubadilisha mtazamo wa Watanzania kuhusu wazee na walemavu. Moja ya
hatua hizo ni kuteuliwa watu wa wenye ulemavu katika nafasi mbalimbali za
uongozi kama albino na wasiona.
Ripoti hiyo ilitolea mfano kuteuliwa kwa
Naibu Waziri wa Ajira, Kazi, Bunge, Sera na Watu Wenye Ulemavu, Dk, Abdallah
Posi, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Sheria na Katiba, Amon Mpanju kuwa ni matokeo
chanya katika eneo hilo.
Halikadhalika upande wa Zanzibar wapo
watu wawili wenye ulemavu ambao wameteuliwa kuwa wawakilishi wa Baraza la
Wawakilishi na ziara za viongozi katika makundi ya watu wenye ulemavu.
Ripoti hiyo pia imebainisha uamuzi wa
mahakama dhidi ya mauji yanayofanywa na vyombo vya dola na matamko ya kutia
shaka yanayochochea mauji hayo hali ambayo inachangia haki ya kuishi kuwa
mashakani.
Ripoti imependekeza Polisi kufuata
taratibu pale wanapowashughulikia watuhumiwa wa uhalifu mbalimbali.
Katika mwaka 2016, ripoti hiyo
imebainisha kuwa viongozi wametoa matamko ambayo yanaweza kuwa kichocheo cha
kukumbatia na kuchochea ukatili mikononi mwa vyombo vya dola.
“Kwa mfano Mkuu wa Dar es Salaam, Paul
Makonda alinukuliwa akisema polisi watumie nguvu dhidi ya watuhumiwa ambao
wanahusishwa na mauji ya polisi,” ilisema ripoti.
Ripoti hiyo imeonesha kuwa tukio kubwa
la tano ni kujichukulia hatua sheria mkononi imekuwa hali ya kitaifa na si
kimkoa ambapo ilitolea mfano tukio la mauji ya watafiti.
Kulingana na ripoti hilo tukio hilo
lilikemewa na viongozi mbalimbali hadi ngazi ya kitaifa hali ambayo ilichangia
wakamatwe wahusika na kufikishwa mahakani.
0 comments:
Post a Comment