‘SASA kumekucha, jogoo limekwishawika Dodoma, kada wa CCM, apewe kura za ndiyo, yule pale tumemuona, yule pale kada wa CCM, apewe kura za ndiyo…’
Mashaka Mgeta |
Hayo ni baadhi ya maneno yaliyokuwa kwenye wimbo mahususi wa kikundi
cha uhamasishaji cha Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tanzania One Theatre (TOT) katika
mchakato wa kumpata mgombea urais kupitia chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa
2005.
Inawezekana ikaaminika kwamba wimbo huo ukiwa ni utunzi wa gwiji
wa nyimbo za kwaya, John Komba (Mwenyezi Mungu azidi kumpumzisha katika
usingizi wa amani) ulilenga kumpata na kumkampenia mgombea urais wa CCM. Inawezekana.
Lakini wimbo huo ulikuwa zaidi ya kumpata na kumkampenia mgombea
urais, bali ulilenga kuashiria matokeo ya uamuzi mzito uliokuwa unafikiwa na
vikao vya Kamati Kuu (CC), Halmashauri Kuu (NEC) na Mkutano Mkuu wa chama hicho.
Kwa wakati huo CCM ikiongozwa na Benjamin Mkapa, jambo kubwa
lililokuwa linasubiriwa kutokea mkoani Dodoma ilikuwa kumpata mgombea urais.
Jakaya Kikwete aliibuka dhidi ya waliokuwa washindani wake, Dk Salim Ahmed
Salim na Profesa Marc Mwandosya.
Mwaka huu chama hicho kikiwa chini ya uongozi wa Rais John
Magufuli kimefungua ukurasa mpya kwa vikao vyake vya NEC kufanyikia jijini Dar
es Salaam badala ya Dodoma kama ilivyo desturi ya chama hicho kwa miongo kadhaa
sasa.
Tofauti na 2005, safari hii CCM hawamtafuti mgombea urais bali
wanajipanga kupata safu ya uongozi itakayoisimamia Serikali iliyoundwa baada ya
ushindi katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, ikiongozwa na Rais John Magufuli. Inawezekana
na kuaminika kwamba kinachosubiriwa kuamriwa katika vikao vya CC na NEC ni
mambo ya kawaida ya kisiasa. La hasha.
Kwa mfumo, asili na mapokeo yake, vikao vya CCM vinavyofanyika
jijini Dar es Salaam ikilinganishwa na hali ya kisiasa, kijamii na kiuchumi
iliyopo nchini, vitakuwa na kazi kubwa ambayo kukamilika kwake kunasubiriwa na
umma.
Vikao vya CC na NEC vina nguvu kubwa katika kutoa mwelekeo wa masuala
tofauti, vikiakisi ilani ya uchaguzi vilivyoshiriki kuitunga, vikaikabidhi kwa
wagombea wake akiwamo Rais Magufuli ili wainadi kwa wananchi, na kupitia ilani
hiyo wakapata ushindi.
Wajumbe wa CC na NEC wakiwa sehemu ya jamii pana ya Watanzania wanajua
kinachojadiliwa kuanzia ngazi ya chini kwenye jamii, wanajua kukubalika kwa
kiongozi waliyemuamini kuwania urais, akashinda, wanajua changamoto na ukosoaji
unaofanywa kwa matukio kadha wa kadha yanayotokea nchini.
Ni dhahiri kwamba inawapasa walio wajumbe wa CC na NEC za CCM ‘kukuna
vichwa’ ili watakapohitimisha vikao vyao jijini Dar es Salaam, wakitambua kuwa
ndio watawala katika mfumo wa uongozi wa nchi, wazungumze, waelekeze, washauri.
Mbali na wajibu huo, wajumbe wa CC na NEC ya CCM wanakutana wakati
ambapo kutokana na uteuzi uliofanywa hivi karibuni na Mwenyekiti wa chama
hicho, Rais Magufuli, miongoni mwa wajumbe wa vikao hivyo wakitakiwa kwenda
kuishi nje ya nchi wakiwa mabalozi, ni dhahiri kwamba chama kitahitaji ‘sura
mpya’.
Ni kweli CCM ina wanachama wengi, mathalani kwa takwimu ya mwisho
kunukuliwa kutoka kwa aliyekuwa Makamu Mwenyekiti, Pius Msekwa, walikuwa takribani
milioni tano.
Kwa hiyo si rahisi miongoni mwa hao wakakosekana wenye uwezo wa
kuziba nafasi zilizoachwa na wajumbe ama viongozi walioteuliwa kushika nyadhifa
tofauti wakiwamo mabalozi.
Ingawa idadi ya wanachama hao inahesabika kuwa kubwa, hoja ya
uwezo wa kila mmoja katika kukitumikia chama hicho na kutekeleza wajibu wake kwa
kadri ya katiba, dira, mweleko, itikadi na miiko yake ni suala linaloweza kuvifanya
vikao hivyo ‘kukuna vichwa’.
Pasipo kuathiri haki ya kila mwanachama kuwa kiongozi, awe wa
kuteuliwa ama kuchaguliwa, CCM haiwezi kuziba nafasi za uongozi na ujumbe wa vikao
vyake kwa ‘kukurupuka’. Inahitaji mapitio huru ya sifa na uwezo wa wanachama
wake, ili kuepuka hatari ya ‘kujimaliza’ katikati ya ushindani wa kisiasa
unaozidi kukua nchini.
Ni ushindani wa kisiasa unaotawaliwa na uwezo mpana wa raia
wakiwamo walio katika vyama vya siasa, kujieleza kwa upana, kushawishi na kujibu
hoja. CCM haiwezi ikabaki kwenye mazoea ya awali, bali kujiweka katika
mazingira ya kukabiliana na changamoto hizo.
CCM inapaswa kuwa na timu inayotambua mageuzi ya kisiasa
yanayotokea ndani nan je ya bara la Afrika. Vyama vya upinzani vinapopata
mwanya wa kuviondoa madarakani vyama tawala, haipaswi kwa CCM kujiridhisha
kwamba ipo salama, hata kama bado ina nguvu na kukubalika nchini.
Ndio maana hivi sasa wananchi wanasubiri. Ni kama giza lilitanda,
usiku ukaingia na sasa kumekucha. Wananchi wanashuhudia jogoo linawika, kwa
maana ya vikao vya CC na NEC ya CCM vinafanyika.
Je, watajibu mahitaji ya umma kwa kadri ya utendaji kazi wa
Serikali ya Rais Magufuli? Je, watajipanga kwa safu iliyo thabiti, ile ambayo
itatekeleza msemo wa `kupeana vijiti’ kwa kukivusha salama chama hicho?
Tusubiri.
0754691540
0 comments:
Post a Comment