Abraham Ntambara na Suleiman Msuya
BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) limesikitishwa na tabia
iliyoanza kujengeka ya kuihusisha Dini ya Kiislamu na vitendo vinavyoashira
ugaidi vilivyojitokeza nchini katika siku za hivi karibuni na kugharimu maisha
ya watu.
Kwa hiyo, limependekeza kuundwa kwa kamati maalumu ya
kitaifa na mkoa kwa ajili ya kuangalia suala hilo kwa undani zaidi ili kuondoa
hofu inayojengeka katika jamii dhidi ya Uislamu.
Wito huo ulitolewa jana na katibu mkuu wa Bakwata,
Sheikh Suleiman Lolila
wakati akitoa salamu kwenye Baraza la Maulid lililofanyika kitaifa wilayani
Iramba, mkoani Singida.
Alisema miezi kadhaa iliyopita pamekuwepo na matukio ya
kutisha maeneo ya Mwanza, Mkuranga mkoani Pwani, Morogoro na Tanga ambayo yamesababisha
vifo vya Watanzania kadhaa wasio na hatia.
“Baraza Kuu la Waislamu Tanzania limesikitishwa sana na
matukio hayo ambayo yameleta vifo vingi. Baraza linasikitika sana Uislamu
kuhusishwa na ugaidi,” alisema Lolila.
Alibainisha kuwa suala linalowasikitisha zaidi Waislamu
ni wahalifu hao wa ugaidi mara nyingi kujitambulisha kuwa ni waumini wa dini ya
Kiislamu.
Alisisitiza kuwa Uislamu hauungi mkono vitendo hivyo vya
ugaidi kwa kuwa ugaidi ni haramu, hivyo ni lazima upigwe vita kwa namna yoyote
ile.
Alisema Mtume
Muhammad alihimiza amani, umoja
na mshikamano baina ya Waislamu wote ambapo alilinganisha umoja huo sawa na
viungo vya mwanadamu.
Aidha, Bakwata itaendelea kukariri wito wake wa kuwataka
Waislamu nchini kuondoa mafarakano baina yao na kuimarisha umoja, mshikamano na
mambo yote yenye maslahi kwao.
Akitoa salamu za
serikali, Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa alionya kuwa vitendo vya ugaidi
havitavumilika na kusema kuwa kutokana na tukio la kuokotwa kwa miili saba katika kingo za mto Ruvu,
wilayni Bagamoyo vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea na uchunguzi ili
kubaini waliohusika na hatimaye watachukuliwa hatua za kisheria.
Aidha alisema
serikali itaendelea kulinda na kuheshimu haki ya kila raia kuwa huru kuabudu
dini anayoiamini na kwamba itaendelea kushirikiana na viongozi wa taasisi zote
za dini.
Waziri Majaliwa
aliwataka viongozi wa dini kutotumia nyumba za ibada kupandikiza chuki kwa
waumini wao dhidi ya watu wa dini nyingine na badala yake wahimize umoja, amani
na mshikamano wa taifa.
Awali, Waziri wa
Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba aliwataka wananchi kutofautisha kati ya udini
na kumcha Mungu.
Alisema mtu
anayeshika dini yake ni mcha Mungu, huku mdini ni yule ambaye anakosoa dini za
watu wengine.
Aidha aliwaambia
kuwa mtu mmoja anapofanya kosa ahukumiwe yeye siyo dini wala taasisi yake.
Alifafanua kwa kusema kuwa kama ni Mkristo amefanya kosa hilo lisiwe kosa la
waumini wote na kadhalika kosa likifanywa na Muislamu ahukumiwe mwenyewe na
siyo dini yake.
“Wananchi wanatakiwa
kufichua watu wote wanaotenda maovu ili lawama zisiende kwenye taasisi hizi,
hii itasaidia kuimarisha umoja na amani,” alisema Nchemba.
Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakary Zubery, amewataka Waislamu
kujitambua na kubadilika ili waweze kukabiliana na changamoto mbalimbali
zinazowazunguka.
Alisema iwapo Waislamu watajitambua na kubadilika itakuwa
rahisi kukabiliana na changamoto mbalimbali kama uchumi, umaskini, ajira, elimu
na kilimo.
Mufti alisema katika miaka 23 ya uongozi wake, Mtume
S.A.W alijikita katika kuhakikisha jamii anayoiongoza inatambua na kubadilika.
Sheikh Mkuu huyo alisema jamii ya kiislamu inapaswa
kujitolea kwa kusoma elimu dunia na akhra ili waweze kuendesha maisha yao
vizuri na kuachana na tabia ya kulalamika.
Alisema kumekuwepo na kasumba kwa Waislamu kuibuka na
kudai kuwa kuna uonevu dhidi yao, huku juhudi za kufanya kazi zikiwa ni za
kusuasua.
“Napenda kusisitiza kuwa katika Baraza Kuu la Waislamu
Tanzania (Bakwata) hii mpya kauli mbiu yetu ni kujitambua na kubadilika,”
alisema.
Alisema Mtume S.A.W alifanikiwa kusisitiza maendeleo na
busara katika jamii jambo ambalo linaendelea kuenziwa katika vizazi vya sasa.
Mufti alisema katika kuhakikisha kuwa jitihada za Mtume
zinaenziwa kikamilifu, ni jukumu la kila mwanafamilia kumpatia elimu mwanaye.
“Mtume amewaletea neema jamii ya Kiislamu, hivyo
tunapaswa kumlipa kwa kumuombea kwa Mungu, kwani ndio uwezo wetu,” alisema.
Naibu Kadhii, Sheikh Ally Muhidini alimzungumzia Mtume
S.A.W kama moja ya kiigizo chema katika jamii kwa kupenda makundi yote hasa
watoto na wanawake.
Sheikh Muhidini alisema iwapo jamii itaishi katika
misingi na mafundisho ya Mtume hoja za kutaka haki za wanawake na watoto
zisingeweza kutokea katika kizazi hiki.
“Leo hii unasikia wiki ya kutetea wanawake na watoto,
sijui siku ya haki za binadamu yote haya Mtume aliyasema na akafundisha jambo
ambalo kwa sasa limesahaulika,” alisema.
Alisema kila mwananchi akijifunza mafunzo ya Mtume
hakutakuwa na sababu ya jamii kuingia katika mitafaruku ambayo haina tija kwao.
0 comments:
Post a Comment