CUF yajitenga na Ukawa uchaguzi mdogo


Suleiman Msuya

Abdul Kambaya
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimesema kuwa kinajiandaa kushiriki kikamilifu uchaguzi mdogo wa madiwani unatarajiwa kufanyika katika 22 Januari 23 mwakani.

Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano CUF, Abdul Kambaya, alibainisha hayo wakati akizungumza na JAMBOLEO jijini Dar es Salaam jana, huku akitaja maeneo watakayowekea mkazo.

Kambaya ambaye yupo upande unaomuunga mkono Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema chama hicho kitaweka nguvu katika kata saba ambazo wanaamini watashinda, huku akiweka bayana kuwa watashiriki kama chama na si Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

“Tumejipanga vilivyo kushiriki uchaguzi wa marudio ambao utafanyika Januari 23 mwakani naamini kata saba zinatuhusu tunaweza kuibuka washindi,” alisema.

Tayari Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetoa maelekezo kwa chama hicho kikitaka fomu za wagombea ziwe zimesainiwa na pande zote mbili za CUF zinazotofautiana ili waweze kupitishwa.

Naibu mkurugenzi huyo alisema kutokana na uchaguzi huo wameahirisha ziara za Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba mikoani ili kujikita katika uchaguzi.

Kambaya aliwataka wana CUF katika maeneo ambayo yanahusika na uchaguzi huo kujipanga vilivyo ili waweze kuibuka kidedea.

Aidha, alitoa wito kwa wanachama wa CUF nchini kote kuendelea kujenga ushirikiano na mshikamano ili kuhakikisha kuwa chama kinaimarika.

Kuhusu mgombea ubunge wa jimbo la Dimani ambalo lipo wazi kutokana na kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo Hafidh Ally Tahir aliyefariki mwezi uliopita mjini Dodoma, alisema hilo linashughulikiwa na chama upande wa Zanzibar.

“Sisi tunahangaika na kata 22 za huku bara ubunge tunawaachia Zanzibar wapange na kupitisha kwani wao ndi wanajua mazingira ya siasa za huko,” alisema.

Alisema iwapo wakiamua kushirikiana na vyama vya Ukawa hilo litakuwa ni jukumu lao kwani wana mamlaka hayo.

Juzi Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitangaza kuitisha uchaguzi katika kata 22 na jimbo moja la Dimani Zanzibar ili kuziba nafasi zilizoachwa wazi kutokana na wahusika kufariki.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo