Mwanafunzi adai kulishwa kupe, kupigwa


Claudia Kayombo, aliyekuwa Kibaha

MHITIMU wa kidato cha nne Shule ya Sekondari Simba Kibaha, Tyson Mwandika (18), yupo hoi kitandani baada ya kudaiwa kupigwa kikatili huku akilazimishwa kula kupe na watu wanaodaiwa ni wafugaji jamii ya Kimang’ ati wakati chanzo kikitajwa kuwa ng’ombe.

Mwanafunzi huyo mkazi wa Mtaa wa Msangani, mkoani humo ambaye amehitimu kidato cha nne mwaka huu anadaiwa kufanyiwa ukatili huo wiki iliyopita na hadi sasa yupo kitandani ambapo huinuka kwa msaada wa watu wengine.

Akisimulia kisa kizima, Mwandika ameliambia JAMBO LEO kwamba siku ya tukio alitoka nyumbani saa 12 asubuhi akiwa na mbwa wa baba yake kwenda kuwinda wanyama wadogo waharibifu wa mazao wanaopatikana umbali mdogo na makazi wanayoishi yaliyo jirani na msitu.

“Baada ya kipigo cha vijana hao wanne sikuweza tena kutembea, nilipopatwa na kiu walinilazimisha kunywa maji kutoka kwenye dimbwi, baadaye nililazimishwa kula kupe waliokuwa wakimnyonya damu ngíombe. Awali nilikataa, lakini nililazimishwa kwa kipigo nikala wawili vijana hao wakishabikia,” alisema Mwandika.

Akisimulia ilivyotokea alisema wakati akitokea kwenye pori hilo baada ya kuwinda alishangaa kumwona ngíombe akiwafuata mbwa hao na kupata wasiwasi ambapo alimpigia simu baba yake, aliyemshauri wamwache kwani akiwa nyumbani kwao, mwenye ng’ombe huyo atapatikana.

Mwandika alisema akiwa njiani kuelekea nyumbani alikutana na vijana watatu waliomhoji alikompata ngíombe huyo naye alisimulia kama alivyomweleza baba yake, lakini wakamtaka abaki kwanza eneo hilo wakidai kuna mtu amepotelewa na ngíombe, wanamwita ili aje amtambue.

Kwa mujibu wa kijana huyo, punde alifika mtu aliyedai kuwa ngíombe huyo ni wake na kuanza kudai kwamba ameiba ngíombe huyo hivyo hapakuwa na namna nyingine zaidi ya kumwadhibu, kisha kumuua ambapo alijitetea lakini haikusaidia.

“Alipofika yule mtu na kudai nimeiba yule ngíombe, walininyangíanya begi langu dogo la mgongoni nililoweka maji ya kunywa, wakanywa na kutupa lile kopo, wakanilazimisha nimshike mkia yule ngíombe hadi tutakapofika huku wao wakinipiga na virungu na fimbo zenye unene wa mti wa fagio la chelewa miguuni.

“Wakati tunaelekea yule ngí ombe alikuwa anakatiza porini na mimi nililazimika kwenda huko huku nikipigwa hadi sehemu yenye udongo mwekundu hapo ndipo wakaniambia kuwa ni mwisho wangu kama siyo kuniua nichague kukatwa mkono au kungíolewa jicho,” alisimulia Mwandika.

Aliongeza: “Wakati huo nilikuwa nimechoka sana, mwanzoni sikujibu chochote wakaniongezea kipigo huku wakazidi kunihoji, ndipo nikachagua nikatwe mkono kwa sababu niliona jicho ni muhimu zaidi.”

Hata hivyo, alisema baada ya tukio hilo alitokea mtu mmoja anayejulikana kwa jina la Dulla ambaye ni kiongozi wa mgambo Kijiji cha Buma, Bagamoyo ambaye aliwasihi wamwache kwa kuwa amepewa taarifa kuwa kijana huyo hana tabia hiyo na baba yake ni ofisa wa jeshi.

Alidai kuwa baada ya hapo, kwa kuwa hakuwa anaweza kutembea, walimbeba hadi katika Ofisi ya Serikali ya Kitongoji cha Mlatange, Kata ya Kiromo, ambako baadaye alichukuliwamaelezo kisha kumfikisha polisi kabla ya kupelekwa kupatiwa matibabu.

Tyson anaiomba Serikali isifumbie macho matukio ya kikatili yanayofanywa na wafugaji kwa sababu hasira za watu mbalimbali wanaofanyiwa ukatili zinaweza kuzaa matunda mabaya katika jamii.

Baba mzazi wa Tyson, Ezekiel Mwandika, aliomba vyombo vya dola vitende haki dhidi ya ukatili aliofanyiwa mtoto wake, kwani haki itaondoa vinyongo katika mioyo ya walioguswa na ukatili huo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi (DCP), Bonaventura Mushongi, alipoulizwa mwishoni kuhusu tukio hilo, alisema alikuwa na likizo fupi na kwamba atafuatilia kufahamu undani.

Hata hivyo, alisema matukio ya ugomvi baina ya wafugaji na jamii nyingine yanaota mizizi kwa kuwa baada ya tukio wanaombwa radhi kwa kulipwa fidia kienyeji hali inayowafanya walalamikaji kukataa kutoa ushahidi dhidi wa kesi zinazofikishwa mahakamani.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo