Grace Gurisha
Josephat Gwajima |
ASKOFU wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima na
wenzake wanatarajia kujitetea Januari 13, katika kesi inayomkabili ya kushindwa
kuhifadhi silaha sehemu salama.
Askofu huyo alitakiwa ajitetee jana mbele ya Hakimu Mkazi
Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, lakini
ilishindikana kutokana na kwamba Hakimu huyo alikuwa na majukumu mengine, kwa
hiyo alishindwa kusikiliza utetezi.
Kutokana na sababu hiyo, kesi hiyo iliahirishwa na Hakimu
Mkazi wa Mahakama hiyo, Victoria Nongwa, ambapo alisema kesi hiyo itaendelea
kusikilizwa siku hiyo kwa upande wa utetezi.
Hatua hiyo, ilifikiwa na Mahakama hiyo baada ya kupitia
ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande wa Jamhuri na vielelezo na kuwaona
washitakiwa hao wana kesi ya kujibu na watapaswa kujitetea.
Wakili wa washitakiwa hao, Peter Kibatala alidai kuwa
wateja wake watajitetea chini ya kiapo, kwa hiyo siku hiyo Gwajima na wenzake
watajitetea chini ya kiapo na wataita mashahidi watatu.
Awali, mpelelezi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam, Sajini Abogasti (46) alidai kuwa wasaidizi wa Askofu
Gwajima walimpelekea bastola saa nane usiku kwenye hospitali ya TMJ alipokuwa
amelazwa baada ya kuanguka kwenye kituo cha Polisi wakati akihojiwa.
Shahidi huyo alitaja wasaidizi hao kuwa ni Yekonia Bihagaze , George Mzava na Geofrey Milulu, ambao walitenda kosa hilo
kinyume na sheria kwa sababu kwa hali ya kawaida haiwezekani mgonjwa kupelekewa
silaha hiyo.
Alidai kuwa Mkuu wa Upelelezi Kinondoni alimuunganisha na Mkuu wa Kituo cha Kawe,
Pamphil ambaye alimkabidhi begi lililokuwa na bastola namba CAT 5802, risasi tatu zilizokuwa kwenye magazini, CD
mbili, risasi 17 za bastola aina ya SMG
na kitabu cha umiliki wa silaha, nguo ya ndani na hati ya kusafiria ya Mchungaji
huyo.
0 comments:
Post a Comment