Grace Gurisha
JOPO la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani Tanzania,
limebatilisha amri ya kutaifisha nyumba ya aliyekuwa askari Polisi, Konstebo Dickson
Muganyizi aliyefungwa kwa kosa la kukutwa na mali ya wizi.
Jopo hilo lililosikiliza rufaa mbili linaundwa na majaji
Mbarouk Mbarouk (Mwenyekiti), Sauda Mjasiri na Semistocles Kaijage, lilifikia
hatua hiyo baada ya kukubaliana na hoja za rufaa iliyokatwa na Muganyizi
kupinga hukumu ya rufaa yake Mahakama Kuu ya Tanzania.
Muganyizi alifikia hatua hiyo licha ya kutengua hukumu
dhidi yake na kumfutia adhabu iliyokataa kutoa amri kuhusu mali yake
iliyotaifishwa.
Hukumu ya jopo hilo, ilisomwa na Naibu Msajili wa
Mahakama ya Rufani, Elizabeth Mkwizu ikisema amri ya kutaifishwa mali hiyo ina
muunganiko na hukumu na adhabu aliyopewa mrufani (Mganyizi).
“Mahakama Kuu baada ya kutengua hukumu na adhabu dhidi ya
mrufani, basi pia ilipaswa kutoa amri kuhusu mali iliyotaifishwa, kwa hiyo
tunatupilia mbali hoja ya rufaa iliyowasilishwa na Jamhuri kwa sababu zina
upungufu,” alisema Mkwizu.
Katika kesi ya msingi, Muganyizi na wenzake wawili, makonstebo
Wanyuba Nyahura na Steven Sipuka, kwa pamoja walikuwa wakikabiliwa na mashitaka
matano kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ya kuvunja ghala la Kitengo cha
Kudhibiti Dawa za Kulevya.
Muganyizi na Nyahura walidaiwa kuiba dawa hizo aina ya
cocaine na heroine gramu 8,441.87, zenye thamani ya Sh 176,424,970 kutoka ghala hilo, kuuza dawa hizo kwa Sipuka
na kukutwa na mali zilidaiwa kuibwa kutoka ghala hilo.
Sipuka alikuwa akikabiliwa na mashitaka ya kununua dawa
za kulevya aina ya cocaine na heroine
zenye thamani ya Sh 176,423,920, kutoka kwa Muganyizi na Nyahura, huku
Muganyizi pia akidaiwa kukutwa na bangi.
Hata hivyo, Mahakama ya Kisutu iliwatia hatiani Muganyizi
na Nyahura katika mashitaka ya nne ya kukutwa na mali iliyoibwa na hivyo kuwahukumu
kifungo cha miaka mitatu jela, huku ikiamuru nyumba ya Muganyizi aliyokuwa
ameinunua itaifishwe na Serikali.
Mwaka 2010 Muganyizi alikata rufaa Mahakama Kuu akipinga
hukumu ya adhabu hiyo na Mahakama Kuu katika hukumu yake iliyotolewa na Jaji
John Utamwa ya April 16, 2013, ilikubaliana na rufaa yake kutengua hukumu na
adhabu dhidi yake.
Lakini Mahakama Kuu haikutoa amri yoyote kuhusu mali iliyotaifishwa,
ikisema kuwa mrufani alikata rufaa kupinga kutiwa hatiani na adhabu aliyopewa
tu na si amri ya kutaifishwa mali, ndipo akakata rufaa Mahakama ya Rufani.
Hivyo, Muganyizi alikata rufaa Mahakama ya Rufani akitoa
hoja kuwa baada ya Mahakama kutengua hukumu na adhabu aliyopewa, Jaji wa
Mahakama Kuu alikosea kukataa kuamuru mali yake iliyotaifishwa irejeshwe.
0 comments:
Post a Comment