* Kila mmoja kati ya wanne ana tatizo hilo
· *
Wizara
yaanika dalili za kuwa na kichaa
Hussein Ndubikile
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Ummy
Mwalimu amesema utafiti unaonesha kuwa kwa kila watu wanne duniani, mmoja ana
matatizo ya afya ya akili.
Alisema hayo jana kwenye maadhimisho ya Siku ya Afya ya Akili Duniani
yaliyofanyika kitaifa Dar es Salaam chini ya kaulimbiu: “Utu katika Afya ya
Akili, Huduma za Kisaikolojia na Afya ya Akili kuwa Huduma ya Kwanza kwa Wote”.
Kwa mujibu wa Waziri Ummy wananchi wanapaswa kuwa makini kuchunguza
afya zao za akili kwa sababu utafiti wa Shirika la Afya Duniani (WHO)
zinaashiria kuwa jamii kwa sasa inakumbwa na maradhi mengi ya namna hiyo.
“Takwimu kwamba kila watu wanne, mmoja wao ana ugonjwa wa akili ni
kielelezo tosha kwamba ipo haja ya jamii kujitambua na kuona umuhimu wa kupewa
elimu ya afya ya akili na kisaikolojia,” alisema na kufafanua:
“Magonjwa ya akili ni yanayoathiri uwezo wa mtu kufikiri, kuhisi,
kutambua na kutenda, hivyo kuwa na tabia au mwenendo ulio tofauti au usioendana
na jamii husika kiimani, kimila, desturi na nyanja nyingine za kijamii.”
Aliongeza: “Tunapaswa kukumbuka kuwa hakuna afya njema ya kimwili
kama hakuna afya ya akili; na pia nchi yetu ikiwa na wananchi wenye afya bora
ya akili ni hazina kubwa kwa Taifa.”
Ummy alibainisha: “Miongoni mwa watu wanaopata matatizo ya kiakili
ni wachache tu ambao wanaweza kufikia na kupata huduma ya afya ya akili, hata
hao wanaohudhuria vituo vya afya, ni wachache wamekuwa wakipata huduma stahiki.
“Katika nchi yetu tumekuwa tukikabiliwa na matatizo kama hayo
kutokana na ufinyu wa bajeti, ukosefu wa wataalamu katika vituo vya kutolea
huduma, ukosefu wa vifaatiba na dawa kwa wagonjwa wenye matatizo ya akili, kijamii
na kisaikolojia.”
Waziri Ummy alisema hali hiyo inatokana na matatizo yanayoikabili jamii
yakiwamo majanga yanayoiandama dunia.
Mwalimu alitoa mfano kwamba, mwaka jana Tanzania ilionesha kuwa na
wagonjwa wa afya ya akili 311,789 kulingana na takwimu za waliokwenda hospitali
kuchunguzwa. Alibainisha kwamba hali hiyo inaashiria kuwa idadi hiyo ni kubwa
zaidi, kwa sababu kuna ambao wana matatizo hayo lakini hawaendi hospitali au
wamekuwa wakienda kupata huduma tofauti.
Alisisitiza kuwa katika kukabaliana na ukweli huo, jitihada
zimefanywa na serikali kutoa huduma za afya ya akili na saikolojia.
Mwalimu alisema Serikali itaendelea kuongeza juhudi katika kutoa huduma
na elimu ya afya ya akili kuanzia ngazi ya msingi na kuwa na kitengo maalumu
kinachotoa huduma hizo katika hospitali zote nchini.
Hatua nyingine alisema ni kuboresha upatikanaji wa dawa za kutibu
magonjwa ya akili katika hospitali zote za Serikali.
Aliongeza kuwa Serikali imeimarisha matibabu ya akili na saikolojia
katika hospitali za mikoa na rufaa hii ikiwa ni pamoja na kupeleka wataalamu wa
afya ya akili wakiwamo madaktari bingwa na wauguzi ili kuboresha huduma kwa
wagonjwa wa nje na waliolazwa.
Alifafanua kuwa sababu za kijamii zinazoweza kusababisha mtu kupata
magonjwa ya akili ni umasikini uliokithiri, kutengwa na kubaguliwa na jamii.
Sababu zingine alizitaja kuwa ni kunyanyaswa kimwili na kingono, kuwa tegemezi,
kupoteza mali, kazi, ulevi, kukosa huduma muhimu na unyanyapaa.
Aliiasa jamii kuachana na Imani potofu kuwa chanzo cha ukichaa ni
ushirikina na hivyo kupoteza fedha na mali nyingi kwa waganga wa kienyeji wasio
waaminifu.
0 comments:
Post a Comment