Grace Gurisha
WAKATI mgogoro ndani ya CUF ukiendelea kutishia mpasuko mkubwa,
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam imeiruhusu Bodi ya Wadhamini
ya Chama hicho kufungua kesi ya msingi dhidi ya uamuzi wa Msajili wa Vyama vya
Siasa nchini.
Bodi hiyo inaiomba Mahakama hiyo kufuta uamuzi Msajili, Jaji
Francis Mutungi wa kumtambua Profesa Ibrahim Lipumba kama Mwenyekiti wa Chama hicho.
Hivi karibuni, Ofisi ya Msajili ilitoa msimamo na ushauri wake kuhusu mgogoro
ndani ya CUF, ikielezea kumtambua Profesa Lipumba kuwa Mwenyekiti halali wa
Chama hicho huku ikishauri anayepinga hili kwenda mahakamani.
Jana, Bodi hiyo ilipata ruhusa ya kufungua kesi hiyo wakati chama
hicho kikiwa bado kwenye mgogoro na mgawanyiko, upande mmoja ukimwunga mkono
Mwenyekiti Lipumba na mwingine ukimpinga kwa madai kuwa si halali kutokana na
kujiuzulu awali na kurejeshwa na Msajili wa Vyama vya Siasa.
Bodi hiyo ilifikia hatua hiyo, kwa sababu haimtambui Profesa
Lipumba kama Mwenyekiti, kwa hiyo anachokifanya Jaji Mutungi ni kukiuka sheria
na tararibu zilizopo. Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji Ama –Isario Munisi wa
Mahakama hiyo, baada ya kupitia nyaraka zilizotolewa na Bodi hiyo na hati ya
kiapo cha Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad na kuridhia wafungue
kesi hiyo.
Jaji Munisi alisema sababu za kupokea nyaraka hizo za maombi ya
kufungua kesi, ni kutokana na kupitia nyaraka hizo za maombi na kuona kuwa ziko
sahihi, hivyo wanapaswakufungua kesi hiyo ndani ya siku 14 ikiwa na hoja muhimu
wanazobishania.
Baada ya maombi hayo kukubaliwa kwa kupewa kibali hicho, Wakili wa
Bodi hiyo, Juma Nassoro alidai kuwa kisheria wanatakiwa wafungue kesi hiyo
ndani ya siku 14, lakini wao watafungua ndani ya siku saba ili kesi hiyo
isikilizwe na kutolewa uamuzi haraka.
“Tunatarajia ndani ya siku saba tutakuwa tumefungua kesi ili iweze kutoa
nafasi ya kuanza kusikilizwa kwa kesi ya msingi,” alisema Nassoro. Mbali na
Jaji Mutungi na Profesa Lipumba, pia kuna wanachama 12 ambao nao wamefunguliwa
kesi na Bodi hiyo kwa madai ya kukiuka taratibu zilizowekwa na chama hicho.
Awali, Bodi hiyo iliwasilisha mahakamani hapo maombi ya kutaka
Mahakama itoe amri ya kumzuia Msajili kuingilia masuala y ndani ya chama hicho.
Nassoro alisema jukumu la kufungua kesi hiyo alipewa na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim
Seif.
Alisema ilifikia hatua hiyo ya kufungua kesi kutokana na mgogoro
unaoendelea, kwa sababu kuna taratibu na sheria zimekiukwa za kuongoza chama.
Nassoro alisema wanaiomba Mahakama itoe amri ya kumzuia Jaji Mutungi
kufanya kazi nje ya mamlaka yake, kwa kuvunja kanuni na taratibu za kazi yake
kinyume na sheria inayomwongoza kama Msajili. Alisema anachokifanya Jaji
Mutungi ni kuingilia demokrasia ya wananchi jambo ambalo si sahihi. Katika
suala la sharia, Msajili hana mamlaka ya kuengua au kubatilisha uamuzi wa
vyama.
Nje ya Mahakama
Pia chama hicho kimemwonya Jaji Mutungi kutojihusisha na masuala ya
CUF, ikiwamo kuandika barua benki kumruhusu Profesa Lipumba kufungua akaunti
kwa ajili ya ruzuku.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa CUF Taifa, Twaha Taslima alisema
wanaishukuru mahakama hiyo kwa kutoa ruksa ya kuwasilisha maombi yao ya kesi. Taslima
ambaye pia na Mwanasheria wa chama hicho, alisema kwa sasa wanachama wa CUF na
wananchi wanapaswa kutuliza nyoyo zao kwa sababu mgogoro huo umefika kwenye
mikono ya sheria.
“Tunawaambia haki lazima itatendeka na Mahakama itaona ni akina
nani walionayo, hivyo hatutaki misukosuko ndani ya chama chetu,” alisema.
Mtatiro
Mwenyekiti wa Kamati ya Muda ya Uongozi wa CUF, Julius Mtatiro alitoa
onyo kwa Jaji Mutungi dhidi ya kujihusisha na harakati za chama hicho kinyume
na sharia ya vyama vya siasa inavyosema.
Alisema wamesikitishwa na barua ya Jaji Mutungi kwenda benki
mbalimbali ikiwamo NMB tawi la Ilala kwa ajili ya kufungua akaunti nyingine ya
chama huku akifahamu kikatiba hairuhusiwi.
Alisema tayari chama hicho kimebaini njama za kuandaa nyaraka
batili zinazofanywa na Lipumba na Msajili kwa ajili ya kufungua akaunti
nyingine baada ya kukataliwa na NMB.
0 comments:
Post a Comment