Sijawa Omary, Mtwara
MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi, (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba
amerudia kueleza sababu za uamuzi wake kujiuzulu uenyekiti wakati wa mchakato
wa Uchaguzi Mkuu mwaka jana.
Amesema ukiukwaji wa Katiba ya CUF kwenye baadhi ya mambo
ilimchefua na kulazimika kufanya uamuzi huo mgumu katika kipindi kigumu, lakini
akasema hadi sasa yeye ndiye Mwenyekiti halali wa CUF, akitaka wanaCUF kudharau
mambo aliyoyaita ya uzushi kuhusu chama hicho na yeye kwenye mtandao.
Alisema hayo jana mjini hapa alipozungumza na wanachama wa katika
kikao cha ndani akiwa katika ziara ya siku mbili kabla ya kwenda Lindi
kuendelea na ziara hiyo.
“Ndugu zangu wanachama, nimetengua rasmi uamuzi huo wa kujiuzulu
baada ya kupandwa na jazba kutokana na uvunjwaji wa Katiba yetu, sasa tuendelee
kujenga chama chetu kwani nimerudi. Mimi niko ngangari kinoma, msiamini mambo
ya kwenye mitandao niko ngangari,” alisema Lipumba.
“Msimamo na Mwongozo wangu Profesa Ibahim Lipumba ni Mwenyekiti
halali wa CUF na mwanachama halali na huu ni msimamo na mwongozo ambao
umesimamia Katiba yetu kwani haki ya kujiuzulu ninayo na ya kutengua ninayo,
hapakuwa na sababu ya kufika hapa,” alisema.
Alipongeza wanachama wa jimbo la Mtwara Mjini kwa moyo waliouonesha
hasa katika kukiweka chama hicho kushika madaraka kwenye jimbo hilo.
Alisema lengo la ziara hiyo ni kuijenga na kuiimarisha CUF Tanzania
Bara ambapo alisema jambo muhimu kwa wanaCUF na viongozi ni kuhakikisha
wanaendelea kuijenga ili izidi kupata heshima.
“Mlionesha uamuzi sahihi kuhakikisha CUF inashika madaraka Mtwara
kuanzia jimbo na halmashauri kwa jumla, hongereni sana kwa hili, mmeonesha
uimara wa chama chetu tena kwa ushindi mkubwa, hongereni kwa kazi nzuri,”
alisema Lipumba.
Mwenyekiti huyo aliyefuatana na mbunge wa Mtwara Mjini, Maftaha
Nachuma alifungua matawi mawili ya CUF katika kata za Magomeni na Ufukoni,
ambako pia alitaka wanachama kukilinda na kukikuza chama hicho ili kizidi kuwa
imara.
Mbunge Nachuma aliwahakikishia wapiga kura hao kwa tuhuma
zilizoripotiwa na vyombo vya habari kuwa amesimamishwa uanachama jambo ambalo
si sahihi na kwamba yeye atakuwa wa mwisho kurudisha kadi ya chama hicho.
0 comments:
Post a Comment