Dotto Mwaibale, Morogoro
MTAFITI na Mhadhiri wa Kitengo cha Afya
ya Jamii, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Dk Abdul Katakweba ametoa hadhari
kwa wafugaji na walaji wa mazao ya wanyama kama maziwa, nyama na damu kuwa
makini na usugu wa dawa zinazotumika kwa binadamu na wanyama.
Dk Katakweba alisema hayo mwishoni mwa
wiki iliyopita alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu utumiaji wa dawa kwa
wanyama na binadamu wanaofuga.
Alisema ni asilimia 12 tu ya watu ndio hununua dawa hizo
kwenye maduka halisi ya dawa yenye wataalamu waliobobea.
Alisema kutokana na utafiti huo
uliofanyika kwa miaka mitano kupitia wadudu watatu wanaopatikana kwenye pua na
matumbo ya wanyama ilibainika kuwa wadudu wote wamekuwa sugu kwa viwango
tofauti.
Aliongeza kuwa kuna watu hutumia dawa za
binadamu kutibu wanyama au dawa za wanyama kutibu binadamu, hivyo inawezekana
kiwango cha dawa kinachotumika hakitibu maradhi yaliyopo bali kinaongeza usugu
na kuwa changamoto kubwa.
Alitaja wanyama waliotumika kwenye
utafiti huo kuwa ni mbwa, nguruwe, paka, ng’ombe, kuku wa kienyeji na wa
kisasa.
Dk Katakweba alisema katika utafiti huo
ulifanyika chuoni hapo na sampuli zingine kupelekwa Denmark ilibainika kuwa
kuna matumizi mabaya ya dawa za wanyama kutokana na elimu ndogo kwa watu, lakini
pia hakuna usimamizi wa sheria za nchi.
Alisema ni kawaida watu wasio na taaluma
ya dawa kuhusishwa katika ununuzi wa dawa au kuuza, pia watu huenda kununua
dawa bila kibali cha daktari wa mifugo au mtaalamu wa dawa.
Dk Katakweba alisema katika utafiti huo
walitumia wadudu; staff, e.coli na entercococci
ambapo mdudu wa kwanza anaishi
kwenye pua za wanyama na binadamu au karibu na koo ambapo matokeo yalionyesha
kuwa dawa aina ya ampicillin haiwawezi wadudu hao kwani wamekuwa sugu kwa
asilimia 100.
Akitoa ufafanuzi alisema wadudu
wanaopatikana kwa wanyama kwenda kwa binadamu husababishwa na maziwa, nyama na
damu kwa kuwa baadhi ya watu hawachemshi vizuri vyakula hivyo na wengi wao
kufanya usafi kwenye mazizi wanamoishi wanyama hao bila vifaa kinga na wanapomaliza
kufanya usafi huo, wanakula bila kunawa jambo ambalo linachangia maambukizi.
0 comments:
Post a Comment