Fidelis Butahe, Dodoma
Mwita Waitara |
MBUNGE wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema),
amesema kitendo cha makatibu wakuu, wakuu wa mikoa na wilaya kuvaa sare za
Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) wakati wa utekelezaji wa majukumu yao, ni
kinyume na Katiba ya nchi na kwamba ni dalili ya nchi kuendeshwa kijeshi.
Tangu alipoapishwa Novemba 5 mwaka juzi,
Rais John Magufuli amekuwa na utaratibu wa kuteua maofisa JWTZ katika nyadhifa
mbalimbali jambo ambalo wabunge wa Upinzani wamekuwa wakilipinga mara kwa mara.
Waitara alitoa kauli hiyo bungeni jana
wakati akiomba Mwongozo, baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu,
akisisitiza kuwa wanajeshi hao kufanya shughuli za kisiasa si sawa.
Huku akitumia kanuni ya Bunge ya 68 (7) na
kurejea taarifa ya habari ya Shirika la Utangazaji (TBC) alisema: “Wakati
naangalia taarifa ya habari nikamwona Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na
Utalii, Meja Milanzi (Meja Jenerali, Gaudence) akifanya shughuli zake huku
amevaa kijeshi kinyume cha Ibara ya 147 ya Katiba yetu.”
Baada ya kikao cha Bunge kuahirishwa saa
7 mchana, Waitara aliliambia gazeti hili kuwa ni kawaida kwa wateule wa Rais
kuvaa sare hizo na kusisitiza: “Wakuu wa mikoa ni wanasiasa na ndani ya CCM ni
wajumbe wa kamati za siasa za mikoa. Mkuu wa Wilaya ni mjumbe wa kamati ya
siasa ya wilaya, sasa wanaanzaje kuvaa au kujihusisha na mavazi ya kijeshi?”
Akiwa bungeni, Waitara alisisitiza kuwa
siku za karibuni Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Kanali Hosea Ndaga naye alionekana
akifanya shughuli zake huku amevaa sare hizo.
“Ukisoma Katiba pamoja na mambo mengine,
inapiga marufuku wanajeshi kujihusisha na siasa. Hawa viongozi wanaovaa nguo za
kijeshi wanawatisha wananchi wanapokwenda kusikiliza matatizo,” alisema.
Ibara ya 147 (3) inasema: “Itakuwa
marufuku kwa mwanajeshi kujiunga na chama chochote cha siasa, isipokuwa tu kama
atakuwa na haki ya kupiga kura iliyotajwa katika ibara ya 5 ya Katiba hii”.
Mbunge huyo alihoji: “Inakuwaje wengine
wanavaa sare za Jeshi na vyeo juu wakati wamestaafu?”
Akijibu Mwongozo huo, Mwenyekiti wa
Bunge, Najma Giga alisema kwa mujibu wa kanuni ambayo Mbunge huyo aliombea
Mwongozo, hoja aliyotoa ni suala ambalo halijatokea ndani ya Bunge wakati
likiendelea na shughuli zake, hivyo asingeweza kutoa majibu yoyote.
0 comments:
Post a Comment