Ukataji wa
miti katika misitu ya kitropiki umechangia ongezeko la malaria kwa asilimia 50
hivi. Hivyo ndivyo wanavyosema watafiti fulani ambao wamekuwa wakichunguza
habari kutoka wilaya 54 za nchini Brazili, pamoja na picha za satelaiti
zinazoonyesha shughuli za ukataji miti.
Malaria
inasambazwa sana katika eneo hilo na mbu anayejulikana kama Anopheles darlingi. Huyo ni aina ya mbu anayeeneza malaria kwa wingi katika
ukanda wa kitropiki wa Mexico na kusini mwa eneo hilo.
Sarah
Olson, aliyeandika ripoti hiyo anasema, “Eneo lililokatwa miti na kuachwa wazi
na lenye vidimbwi vya maji vinavyopata kiasi kidogo cha mwanga wa jua, huandaa
mahali pazuri pa mbu hao kuzaana.” Maeneo ambayo yaliyoripotiwa kuwa na visa
vingi vya malaria ni yale yaliyokatwa miti.
Watafiti katika Chuo Kikuu cha Wisonsin-Madison nchini Marekani
walijiuliza, “Kukata mti mmoja katika Msitu wa Amazon kunamaanisha chochote kwa
mbu anayeeneza malaria?” Baada ya utafiti wao wakapata jawabu la “NDIYO”.
Watafiti hao waligundua kuwa kitendo cha kupungua kwa asilimia nne ya
mistu ya mvua kumesababisha ongezeko la asilimia 50 la visa vya malaria magharibi
mwa Brazil, na hali ilikuwa hivyo mwongo baada ya miti kuwa imekatwa.
Timu ya watafiti hao iligundua kuwa ukataji wa miti ulikuwa unajenga
mazingira bora kwa aina hiyo ya mbu ambao hupendelea sana sehemu yenye mwanga
wa jua.
Utafiti mwingine uliochapishwa katika tovuti ya Kituo cha Kinga na
Udhibiti wa Afya cha Marekani ulisema: “…kuna uhusiano mkubwa kati ya ukataji
miti na ongezeko la malaria…”
Kwa mujibu wa taarifa ya Taasisi ya Kimataifa ya Afya, mtafiti wa afya
ya mazingira, Jonathan Patz, alikaririwa akisema: “Kama wizara za afya za nchi
waathirika hazitafanya kazi pamoja kuzuia hili (ukataji miti), kamwe hatutapata
suluhisho … tutakuwa tunatafuta suluhisho la juu juu tu.”
0 comments:
Post a Comment