*Shule 6 za kata zawekwa kundi la 10 mbovu
*NECTA
yasema ufaulu kitaifa umeongezeka
Celina Mathew na Suleiman Msuya
Dk Charles Msonde |
BARAZA la Mitihani la Taifa (NECTA),
limetangaza matokeo ya kidato cha nne kwa wanafunzi waliomaliza mwaka jana
yakishuhudia shule sita za Dar es Salaam zikifanya vibaya katika kundi la shule
10 zilizofanya vibaya kitaifa.
Akitangaza matokeo hayo jana Dar es Salaam
Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk Charles Msonde, alisema katika matokeo ya mwaka huu
ufaulu umeongezeka kwa asilimia 2.56 ikilinganishwa na mwaka juzi.
Msonde alisema katika mtihani wa mwaka
jana jumla ya watahiniwa 408,372 walifanya wasichana wakiwa 209,456 sawa na
asilimia 51.29 na wavulana 198. 916 sawa na asilimia 48.71 ambapo waliosajiliwa, kama watahiniwa wa shule walikuwa 355,822 na watahiniwa wa kujitegemea 52,550.
“Watahiniwa wa shule 355,822 waliosajiliwa,
watahiniwa 349,524 sawa na asilimia
98.23 walifanya mtihani ambapo wasichana walikuwa ni 178,775 sawa asilimia 97.97
na wavulana ni 170,749 sawa na asilimia 98.50 na watahiniwa 6,298 sawa na
asilimia 1.77 hawakufanya mtihani,’’ alisema.
Dk Msonde alisema kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea, 52,550
waliosajiliwa, watahiniwa 47,751 sawa
na asilimia 90.87 walifanya mtihani na 4,799 sawa na asilimia 9.13 hawakufanya.
Alisema kwa watahiniwa wa mtihani wa Maarifa, kati ya
20,655 waliosajiliwa, 17,347 sawa na asilimia 83.98 walifanya na 3,308 sawa na
asilimia 16.02 hawakufanya.
Matokeo
Akifafanua kuhusu matokeo alisema jumla
ya watahiniwa 277,283 sawa na asilimia 70.09 waliofanya mtihani wamefaulu
wasichana wakiwa 135,859 sawa na asilimia 67.06 wakati wavulana ni 141,424 sawa
na asilimia 73.26.
Alisema watahiniwa wa shule waliofaulu
ni 244,762 sawa na asilimia 70.35 ya waliofanya. “Wasichana
ni 119,896 sawa na asilimia 67.34 na wavulana ni 124,866 sawa na asilimia 73.50, » alisema.
Aliongeza kuwa mwaka juzi watahiniwa 240,996 sawa na asilimia 67.91 wa shule walifaulu
mtihani huo na ufaulu wa watahiniwa wa shule
uliongezeka kwa asilimia 2.44 mwaka jana ikilinganishwa na mwaka juzi.
Wa kujitegemea
Alisema idadi ya watahiniwa wa kujitegemea
waliofaulu ni 32,521 sawa na asilimia 68.19 huku mwaka juzi wa kujitegemea
31,951 sawa na asilimia 64.80 walifaulu hivyo, ufaulu kuongezeka kwa asilimia
3.39 ikilinganishwa na mwaka juzi.
Maarifa
(QT)
Kuhusu watahiniwa wa Maarifa (QT)
waliofaulu ni 8,751 sawa na asilimia 50.48 huku mwaka juzi wakiwa 7,536 sawa na
asilimia 46.63 hivyo, ufaulu kuongezeka kwa asilimia 3.85 ikilinganishwa na
mwaka juzi.
Ubora wa ufaulu
Dk
Msonde alisema takwimu zinaonesha idadi ya watahiniwa wa shule waliopata ufaulu
mzuri wa madaraja ya I - III katika mtihani huo mwaka jana ni 96,018 sawa na asilimia 27.60; wakiwamo wasichana 39,282 sawa na asilimia 22.06
na wavulana 56,736 sawa na asilimia 33.40.
Alisema ufaulu wa watahiniwa wa
shule katika Historia, Jiografia, Kiswahili, Kiingereza, Hesabu, Biolojia,
Kemia, Fizikia, Biashara na Uhasibu ulipanda kwa asilimia 0.12 na 8.08
ikilinganishwa na mwaka juzi.
“Watahiniwa wamefanya vizuri zaidi
katika Kiswahili ambapo asilimia 77.75 ya watahiniwa wa shule waliofanya somo
hilo wamefaulu huku Hesabu hawakufanya vizuri ambapo ni asilimia 18.12 waliofaulu,”
alisema.
10 bora
Katibu Mtendaji alitaja shule 10 bora
kuwa ni Sekondari ya Feza Boys, Dar es Salaam iliyoongoza ikifuatiwa na St.
Francis Girls, Mbeya; Kaizirege Junior, Kagera; Marian Girls, Pwani; Marian
Boys, Pwani; St. Aloysius Girls, Pwani; Shamsiye Boys, Dar es Salaam, Anwarite
Girls, Kilimanjaro; Kifungilo Girls, Tanga na Thomas More Machrina, Dar es
Salaam.
10 za mwisho
Aidha, alitaja
shule 10 za mwisho kuwa ni Kitonga, Nyerubu, Mbopo, Mbondole, Somangila na
Kidete za Dar es Salaam ; Masaki, Lindi, Dahani, Kilimanjaro ; Makiba
Arusha na Ruponda, Lindi.
Wanafunzi 10 bora
“Mwanafunzi wa kwanza kitaifa ni Alfred Shauri wa Feza Boys, Cynthia
Mchechu wa St. Francis Girls, Erick Mamuya wa Marian Boys, Jigna Chavda wa St.
Mary Goreti, na Naomi Tundui wa Marian Girls,” alisema.
Wengine ni Victoria Chang'a wa St. Francis Girls, Brian Johnson wa Marian
Boys, Esther Mndeme wa St. Mary's Mazinde Juu, Tanga, Ally Koti wa Alcp
Kilasara, Kilimanjaro na Emmanuel Kajege wa Marian Boys.
Wasichana 10 Bora
Aidha, Msonde alitaja wasichana 10 bora
kuwa ni Mchechu, Chavda, Tundui, Chang'a na Mndeme.
Wengine ni Christa Kobulungo wa St.
Francis Girls, Nelda John wa Marian Girls, Mariamu Shaban wa Kifungilo Girls, Beatrice
Mwella wa St. Mary's Mazinde Juu na Rachel Kisasa wa Canossa, Dar es Salaam.
Wavulana 10 bora
Wavulana 10 bora kitaifa kwa mujibu wa
matokeo hayo ni Shauri, Mamuya, Johnson Koti, Kajege, John Ng'hwaya wa Nyegezi
Seminary, Mwanza na Clever Yohana wa
Living Stone Boys Seminary ya Tanga.
Wengine ni Desderius Rugabandana wa Morning
Star ya Mwanza, Kennedy Boniface wa Feza na Assad Msangi wa Feza Boys, Dar es
Salaam.
Mikoa 10 bora
Aliitaja mikoa 10 iliyoongoza kuwa ni Njombe,
Iringa, Kagera, Kigoma, Kilimanjaro, Mwanza, Pwani, Ruvuma, Shinyanga na Tabora
huku halmashauri bora zikiwa ni Bukoba Mjini, Njombe Mjini, Kakonko, Kahama
Mjini, Wanging’ombe, Ilemela, Iringa Mjini, Mkuranga, Igunga na Kibaha Mjini.
Matokeo
yaliyozuiwa
Katibu
Mtendaji alisema NECTA imezuia matokeo ya watahiniwa 33 wa shule ambao walipata matatizo ya kiafya
na kushindwa kufanya mtihani kwa baadhi ya masomo na wamepewa fursa ya kufanya mtihani kwa masomo ambayo hawakufanya kwa sababu ya ugonjwa kwenye mtihani
wa mwaka huu.
“Watahiniwa
124 wa shule ambao
walipata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya mtihani kwa masomo yote
wamepewa fursa ya kufanya mtihani wa mwaka huu kama watahiniwa wa shule na 40
wa Sekondari ya Hellens (S2345) wanaodaiwa alama za CA hadi Mkuu wa Shule
atakapowasilisha alama hizo kwa mujibu wa kifungu cha 9 (2) cha kanuni za mitihani, ‘’
alisema.
Matokeo
yaliyofutwa
Dk Msonde alisema NECTA imefuta matokeo yote ya watahiniwa 126
waliobainika kufanya udanganyifu kwenye mitihani. ‘’Kati ya watahiniwa
waliobainika kufanya udanganyifu, 58 ni wa kujitegemea, 58 ni wa shule na 10 ni
wa Maarifa (QT).
Aidha,
Baraza limefuta matokeo ya mtahiniwa aliyeandika matusi kwenye karatasi ya
majibu.
0 comments:
Post a Comment