Mwandishi Wetu
Marehemu Samuel Sitta |
ILIKUWA Desemba 18 mwaka 1942 wilayani
Urambo mkoani Tabora, ndipo alizaliwa Hayati Samuel John Sitta, Spika wa Bunge
la Tisa.
Sitta alisoma Shule ya Msingi Urambo
kati ya mwaka 1950 – 1953, kisha alikwenda Wilaya ya Sikonge mwaka 1954 - 1957
na kuendelea na masomo ya “Middle School” katika shule ya “Sikonge Middle
School”.
Baadaye mwaka 1958 – 1963 alianza masomo
ya sekondari Shule ya Wavulana Tabora (Tabora Boys), kidato cha kwanza hadi cha
sita.
Baada ya kuhitimu sekondari, Sitta
alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na kusomea Shahada ya Sheria
(LLB) mwaka 1964.
Sitta alisoma shahada hiyo kwa miaka saba
kati ya mwaka 1964 na 1971, baada ya kufukuzwa chuoni hapo mwaka 1966 alipokuwa
mwaka wa pili; akiwa kiongozi wa wanafunzi chuoni hapo, wakati wanafunzi walipogoma
na kuandamana kupinga kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na kukatwa
mishahara yao baada ya mafunzo ya JKT.
Samuel Sitta, Wilfred Mwabulambo na wengine
kadhaa waliokuwa mstari wa mbele kutetea walichokiita haki zao, waliishutumu
Serikali ya wakati huo wakisema; “…ni heri wakati wa Ukoloni kuliko utawala wa
Mwalimu Nyerere.”
Kutokana na kauli hiyo, Rais wa Tanzania
wakati huo, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, alikasirishwa na kuwafukuza chuo
wanafunzi wote 400 kwa kile alichokiita “kwenda kufunzwa adabu majumbani mwao.”
Hata hivyo, baada ya mgomo na shinikizo
hilo la wanafunzi, Mwalimu Nyerere alikubali kupunguza mshahara wake wa Sh. 4,000
bila kodi akaagiza pia mishahara ya mawaziri ipunguzwe kwa asilimia mbili.
Miezi miwili baadaye, akatangaza Azimio
la Arusha (Februari 5, 1967) kuyapa uzito malalamiko ya wanafunzi hao
waliopinga kukatwa mishahara yao wakati mawaziri wakiwa na mishahara mikubwa.
Miezi kumi baadaye, baada ya Mwalimu
Nyerere kushawishiwa na hasira kutulia aliamua kuwarudisha chuoni wanafunzi 392,
lakini Sitta na wenzake saba hawakurejeshwa chuoni.
Hata hivyo, viongozi wa chuo hicho
walitumia busara kuandikiwa barua mbili maalumu mwaka 1967 kwa Mwalimu Nyerere,
kumuomba awarejeshe chuoni wanafunzi hao.
Kuchapwa viboko na Nyerere
Baada ya barua hizo, hatimaye, Mwalimu Nyerere
aliwarejesha chuoni Sitta na wenzake
saba kwa sharti, yeye mwenyewe awatandike viboko Sitta na Mwabulambo, ambapo walitii adhabu
hiyo na kurejea chuoni kuendelea na
masomo hadi walipohitimu mwaka 1971.
Hata hivyo, Sitta alirejea chuoni akiwa tayari
mwajiriwa wa Kampuni ya Mafuta ya “Caltex” akiwa Meneja wa Tawi (1967 – 1969)
na mwaka 1969 – 1975, aliajiriwa na Shirika la Maendeleo la Taifa kuwa Katibu
na Mkurugenzi wa Utawala.
Baadaye mwaka 1976 Sitta aliamua
kujiendeleza kielimu katika masuala ya Usimamizi nchini Uswisi kwenye Chuo
Kikuu cha IMEDE, ambako alihitimu Stashahada ya Juu ya Usimamizi mwaka huo huo
1976.
Chini ya mfumo wa chama kimoja, Sitta
amekuwa kiongozi wa juu wa CCM na Serikali akiwa Mbunge, Mkuu wa Mkoa na Waziri
kwa nyakati tofauti; nafasi alizoshika hata baada ya kurejea kwa mfumo wa vyama
vingi mwaka 1992.
Kuanzia mwaka 1975 - 1995 enzi za mfumo
wa chama kimoja, Sitta alikuwa Mbunge wa Urambo (kabla jimbo hilo halijagawanywa
na kuwa Urambo Magharibi na Mashariki) na pia alikuwa Waziri kwa nyakati
tofauti. Kwa mfano wakati wa kipindi cha mwisho cha Mzee Mwinyi, Sitta alikuwa
Waziri za Katiba na Sheria.
Kuangushwa jimboni
Mwaka 1995, Sitta aliingia kwenye
mapambano mapya ya siasa za vyama vingi na kwa bahati mbaya akawa mmoja wa
vigogo walioangushwa na wabunge wa NCCR-Mageuzi.
Mshindani wake mkuu alikuwa Msina Jacob
Abraham. Msina alishinda kwa kura 10,788 dhidi ya 9,497 za Sitta.
Sitta alirudi tena kwenye jukwaa la
siasa mwaka 2005 ambapo kwenye Uchaguzi Mkuu aliwashinda wapinzani wake wakuu;
Lumatiliza Lubungila wa NCCR-Mageuzi na Wilson Ntakamulenga wa CUF. Sitta
alipata kura 28,660 (asilimia 72.3) na kurejesha heshima yake jimboni Urambo
Mashariki.
Kurudi kwa nguvu kulimpa nafasi ya
kuwania na kuteuliwa na CCM kugombea uspika wa Bunge la Tanzania na akaliongoza
Bunge la Tisa kwa mafanikio.
Kurejesha heshima
Mwaka 2010 Sitta alishiriki tena uchaguzi
Urambo Mashariki akawashinda wapinzani wake wakuu Msafiri Abdulrahmani Mtemelwa
(Chadema) na Zombwe Lotto Edward (CUF) kwa kupata kura 19,947 sawa na asilimia 70.47.
Sitta alipoteza ndoto za uspika na
ukahamia kwa mwanamama Anne Makinda.
Rais Jakaya Kikwete alipotangaza Baraza
la Mawaziri mwaka 2010, alimpa Sitta Wizara ya Afrika Mashariki kuwa Waziri,
wadhifa aliodumu nao hadi mwaka jana mwanzoni alipobadilishwa na kupelekwa
Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi.
Mbio za urais
Sitta alianza mbio za urais ‘kimyakimya’
tangu alipokuwa Spika wa Bunge la Tisa (2005 – 2010) maana kuna nyakati alikuwa
akitoa kauli zinazoashiria kuwa nchi inayumba na haina uongozi thabiti, huku
akionesha kuwa viongozi thabiti waliopo hawajapewa uongozi, akiwemo yeye.
Hata alipoliongoza Bunge la Katiba mwaka
2014, mara nyingi Sitta alionekana kama mtu mwenye shauku kubwa na urais na
alipohojiwa mara kwa mara, juu ya urais alionesha ana ndoto hizo. Mara kadhaa,
alilalamika kuwa wala rushwa wakubwa wanampiga vita kwa sababu ni msafi.
Sitta aliingia katika kinyang’anyiro cha
Uchaguzi Mkuu ambapo jina lake halikufika kwenye Halmashauri Kuu ya CCM (Nec),
hiyo ikawa ndio mwisho wake kisiasa kwani hajawahi kuonekana katika harakati
hizo tangu kipindi hicho.
Changamoto za afya
Baada ya kimya kirefu, taarifa zilianza
kusambaa kuwa afya yake si nzuri na baadae akasafirishwa kwenda nchini
Ujerumani kwa ajili ya matibabu ambapo usiku wa kuamkia jana alifariki.
Kwa mujibu wa mwanae ambaye ni Meya wa
Manispaa ya Kinondoni, Benjamin Sitta, baba yake alikuwa akisumbuliwa na
ugonjwa wa saratani ya tezi dume kwa muda mrefu.
Alisema Marehemu Sitta aligundua ugonjwa
huo ukiwa umeathiri sehemu kubwa ya mwili hivyo ikashindikana kutibika.
0 comments:
Post a Comment