Grace Gurisha
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru),
imeieleza Mahakama kuwa upelelezi wa kesi ya kuomba rushwa inayomkabili
aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Ephraim Mgawe
na wenzake haujakamilika.
Katika kesi hiyo, Mgawe na wenzake wanadaiwa kuomba
rushwa ya ya dola za Marekani milioni nne sawa na zaidi ya Sh bilioni nane
kupitia wakala wa Kampuni ya DB
Shapriya, ili kuiwezesha kampuni hiyo kupata
zabuni ya ujenzi wa bomba la kupakulia mafuta kwenye rasi ya Mji Mwemaya,
Kigamboni Dar es Salaam.
Kutokana na kutokamilika kwa ushahidi huo, Wakili wa
Takukuru, Emmanuel Jacob jana aliomba tarehe nyingine ya kutajwa kwa kesi hiyo,
mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,
Dar es Salaam ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika au la.
Baada ya Jacob kudai kuwa upelelezi haujakamilika, hakimu
alikubaliana na ombi lao na kuahirisha kesi hiyo hadi Novemba 30 kwa kutajwa.
Mbali na Mgawe, vigogo wengine wanashitakiwa katika kesi
hiyo ni Mkurugenzi wa zamani wa Uhandisi wa TPA, Bakari Kilo (59), aliyekuwa
Meneja wa Mazingira wa TPA, Theophil Kimaro (54) na Mkurugenzi Mtendaji wa
Kampuni ya DB Shapriya, Kishor Shapriya (60).
Jacob alidai kuwa kosa la kuomba rushwa linamkabili
Mgawe, Kilo na Kimaro; ambao kwa pamoja wanashitakiwa kutenda kosa hilo katika
tarehe tofauti na maeneo tofauti ambayo hayafahamiki kati ya mwaka 2009 na
2012.
Ilidaiwa kuwa kwa kutumia nafasi zao, waliomba rushwa ili
Shapriya ashinde zabuni iliyokuwa ikishindaniwa yenye namba
AE/0116/2008-2009/10/59 kwa ajili ya ujenzi wa bomba hilo katika rasi ya
Mjimwema, ambapo likijengwa meli zinaweza kupita juu ya pomba hilo.
Katika kosa la pili, linalomkabili Shapriya peke,
mshitakiwa huyo anadaiwa kuwa katika tarehe tofauti kati mwaka 2008 na 2009;
akiwa Mkurugenzi wa DB, alitoa rushwa ya dola za
Marekani milioni nne kwa vigogo hao.
Inadaiwa kuwa rushwa hiyo ilitolewa ili kushawishi kuiwezesha
kampuni ya Leighton Offoshore Pte, kupata zabuni ya ujenzi wa Bomba la Kupakulia
Mafuta kwenye rasi ya Mji Mwema ya TPA.
Shapriya anadaiwa alitoa kiasi hicho kwa Mgawe, Kilo na
Kimaro kwa ajili ya kuiwezesha kampuni yake ishinde zabuni namba
AE/0116/2008-2009/10/59 ya ujenzi huo wa bomba hilo la TPA katika rasi ya
Mjimwema Kigamboni.
Vigogo hao walinusurika kwenda rumande baada ya kutimiza
masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili waaminifu waliosaini bondi ya
Sh milioni 500 kwa kila mmoja.
0 comments:
Post a Comment