Fidelis Butahe, Dodoma
SIKU 10 baada ya Ofisi ya Rais, Utumishi
wa Umma na Utawala Bora kuanza safari ya kuhamia Dodoma, kutekeleza agizo la
Rais John Magufuli la Serikali kuhamia makao makuu ya nchi, zipo taarifa za
wizara takriban tano kutumia majengo ya Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).
Hatua hiyo ilisababisha manung’uniko na
upinzani dhidi ya hatua hiyo kutoka kwa kambi ya Upinzani kupitia bungeni jana.
Wapinzani walisema matumizi ya majengo
hayo ni sawa na kuingilia shughuli za Chuo na wanafunzi, jambo ambalo halikubaliki
katika uendelezaji na usimamizi wa vyuo vikuu nchini, huku wakibainisha kuwa
watumishi wa Serikali wanaohamia Dodoma hawaendi na wake zao, jambo ambalo ni
hatari kwa wanafunzi wa kike chuoni hapo.
Mbali na Wizara hiyo, zingine ambazo
zinatajwa kuwa ziko kwenye mchakato wa kuhamia kwenye majengo hayo, ni pamoja na
ya Katiba na Sheria, ya Kilimo na Mifugo, ya Mambo ya Ndani ya Nchi na ya Wizara
ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi.
Hoja hiyo iliibuka wakati wa kipindi cha
maswali na majibu baada ya Mbunge wa Viti Maalumu, Susan Lyimo (Chadema) kutaka
kujua sababu za Serikali kubadili
majengo ya Chuo hicho kuwa ya wizara.
“Ni kama tunachukua wanafunzi na
kuwapeleka kwenye midomo ya simba. Nataka kujua huu utaratibu wa kuhamia Dodoma
maana yake ni kubadilisha miundombinu ya elimu kuwa ofisi za Serikali au…?” Alihoji
Lyimo ambaye pia ni Waziri kivuli wa Elimu.
Licha
ya Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Stella Manyanya kujibu
swali hilo, wabunge wa Upinzani huku wakizomea na kuimba ‘peoples power’,
walionekana kutoridhishwa na majibu hayo
jambo lililosababisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na
Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama kuingilia
kati.
Januari 24, Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki alitangaza mpango huo
wa kuhamia Dodoma akiwa Dar es Salaam, kutekeleza agizo la Rais Magufuli Julai
mwaka jana wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu ya Siku ya Mashujaa
yaliyofanyika mjini hapa.
Katika majibu yake, Manyanya alisema,
“chuo si majengo peke yake bali inajumuisha walimu na vitendea kazi. Chuo hiki
kilipojengwa kilijiwekea utaratibu wa namna ya kuwa na majengo yake na taasisi
au wizara kuhamia hapo ni suala la muda mfupi.
“Majengo hayo kwa sasa hayatumiwi na
wanafunzi na wizara zinatafuta majengo yake chini ya CDA (Mamlaka ya
Ustawishaji Makao Makuu Dodoma) ambayo inatoa viwanja.”
Alisema utaratibu wa kuhamia Dodoma
utaongeza tija na ufanisi hasa kwa wananchi kwa sababu watakuwa wakipata huduma
kirahisi kwenye mji huu ambao hauna foleni.
Baada ya majibu hayo Mhagama alisimama
na kusisitiza: “Nia ya Serikali katika kuendeleza chuo hiki ilijidhihirisha
kutokana na nia njema ya CCM kutoa ukumbi wake na kuwa sehemu ya chuo. Chama hiki kinaendeleza mpango wa taifa wa Ilani
ya Uchaguzi ya kuhamishia Serikali Dodoma.”
Alisema majengo yanayotumika na Serikali
chuoni hapo yalijengwa na Serikali inayoongozwa na chama hicho na ni mengi
hivyo kuliko kuyaacha ni vema yakatumiwa na baadhi ya wizara.
“Niwahakikishie wabunge, majengo yale
hayaingiliani na shughuli yoyote ya elimu pale chuoni, nazipongeza wizara zote
kwa kuyalinda na kuyatumia na Serikali ambayo itaendelea kuyaongeza na uhamiaji
wa watumishi Dodoma utabaki pale pale,” alisema Mhagama.
Baadaye Mchungaji Msigwa aliomba Mwongozo
kuhusu suala hilo kusisitiza kuwa kiutaratibu si sahihi kuchanganya shughuli za
Serikali na chuo huku akisisitiza kuwa hilo linatokea kwa sababu katika mwaka
wa fedha wa 2016/17, Serikali haikuwa na bajeti ya kuhamia Dodoma.
“Ndiyo maana inavuruga wanafunzi
wanaosoma, watumishi wa Serikali wanahamia Dodoma bila wake zao, jambo ambalo
ni hatari kwa wanafunzi badala ya kumaliza na alama A watamaliza na maambukizi
ya Ukimwi,” alisema Msigwa.
“Kwa nini Serikali inahamia Dodoma na
kwenda kuingilia mipango mingine, kwa nini Bunge libariki mambo haya yasiyo
sahihi ambayo Serikali inafanya?”
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Bunge, Najma Murtaza
Giga hakutoa majibu ya Mwongozo huo kwa maelezo kuwa tayari Mhagama alishajibu.
0 comments:
Post a Comment