Salha Mohamed
Kamanda Mohamed Mpinga |
JESHI la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani,
limekamata pikipiki 16 na kuzitoa matairi baada ya kupita kwenye barabara ya
mwendo kasi (BRT).
Utoaji wa matairi kwenye pikipiki hizo
ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli la kulitaka Jeshi hilo kutoa
matairi ya magari na pikipiki zinazopita kwenye barabara hizo.
Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili
jana Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani nchini,
Mohamed Mpinga alisema pikipiki hizo ni kati ya 61 zilizokamatwa kwenye operesheni
ya siku mbili.
“Tunatekeleza agizo la Rais na litakuwa
endelevu, tutatoa matairi na madereva tutawaweka ndani na wengine wametoka leo (jana),”
alisema Mpinga.
Alisema madereva wa pikipiki 54
wamekamatwa katika operesheni hiyo, huku pikipiki 45 zikikamatwa kutokana na makosa
mbalimbali kama kupita sehemu ambazo hawaruhusiwi kuingia, kutovaa kofia ngumu
na 16 kupita BRT.
Mpinga alisema bado hawajakamata magari
yanayopita kwenye barabara hizo ambapo wakiyakamata watayatoa matairi kama
walivyofanya kwenye pikipiki.
“Magari bado, tukiyaona tutayatoa
matairi yote…nadhani wanaogopa si kama pikipiki hawaogopi, Rais keshasema
lazima tutekeleze agizo,” alisema.
Alisema mbali na kukamata pikipiki hizo,
kikosi hicho kilikamata abiria wanne kwa kukaidi kuvaa kofia ngumu jambo
linalohatarisha usalama wao.
Katika hatua nyingine, Mpinga alisema walikamata
magari zaidi ya 580 yaliyoweka taa zenye mwanga mkali, huku akibainisha kuwa na
mwitikio mkubwa wa utoaji taa hizo.
“Nilifanya utafiti nikagundua kuna
mwitikio mzuri, magari mengi wametoa wenyewe, lakini tumekamata magari makubwa
zaidi ya 400, magari madogo zaidi ya 180 na kuwatoza faini,” alisema.
Alisema ni vema madereva wakaheshimu
sheria na taratibu za Jeshi hilo ili kulinda usalama wao huku akitoa hadhari
kwa wanaofunika taa hizo mchana na kuzitumia usiku.
“Tunafanya operesheni usiku, tukimgundua
tunamtolea na kumkamata, lakini kama magari yatakuwa na operesheni maalumu kama
kuwinda yataruhusiwa ila mchana wayafunike,” alisema Mpinga.
0 comments:
Post a Comment