HATIMAYE wachimbaji 15 wa mgodi wa dhahabu
wa RZ Nyarugusu, mkoani hapa akiwamo raia wa China ‘wamepanda’ vyeo, baada ya
Serikali kuagiza uongozi wa mgodi huo, uwape mikataba ya muda mrefu na kuacha kufanya
kazi ya mashimoni.
Kauli hiyo ya Serikali imethibitishwa na
wachimbaji hao ambao walidokeza gazeti hili jana kuwa kwa sasa watafanya kazi
zingine bila kuingia kwenye mashimo na badala yake watasimamia na kuendesha
mitambo ya mgodi huo.
Akizungumza na gazeti hili mmoja wao,
Jonas Kachungwa alisema: “Alikuja Mkuu wa Wilaya hapa jana (juzi) tumezungumza
naye pamoja na uongozi wa mgodi. Viongozi wetu wameagizwa kutupa mikataba
mipya.Tumeambiwa kwa sasa tutakuwa tunafanya kazi za nje ya mgodi na si kuingia
tena machimboni.”
Alisema tayari uongozi wa mgodi
umewahakikishia kuwapa mikataba hiyo na ndani ya wikii hii wanatarajia kuisaini
na kuendelea na kazi mgodini.
Alisema hatua hiyo ni njema kwao, kwani
imeonesha kuwa Serikali na wamiliki wa
mgodi huo wanawajali na kuthamini mchango wao, hivyo wataendelea kufanya kazi
kwa kujituma zaidi kwani kilichotokea wanaona ni ajali kazini tu.
Akizungumzia suala hilo, Mkuu wa Wilaya
ya Geita, Herman Kapufi alisema
ameagiza wachimbaji hao wapewe
mikataba mipya na waliokuwa wamefunikwa na kifusi watapewa mikataba hiyo siku
chache zijazo.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Meja Jenerali mstaafu,
Ezekiel Kyunga alisema baada ya tukio hilo Serikali imeagiza kila mgodi ufuate
taratibu za usalama ikiwamo kuwa na timu madhubuti za uokozi.
Alisema suala la usalama migodini
limekuwa likisemwa na Serikali kwa muda mrefu sasa na wamiliki wa migodi baadhi
yao wamekuwa wakipuuza.
“Serikali kupitia wakaguzi wa migodi
wamekuwa wakipita na kukagua usalama.Taratibu zinaelekeza kila mgodi ufuate na
kuzingatia usalama ikiwamo kuwa na timu za uokozi. Tulifanikiwa kuwatoa hawa
watu 15 kwa sababu migodi mikubwa ina timu nzuri za uokozi ukiwamo mgodi wa
GGM,” alisema Kyunga.
Alisema uchunguzi wa kiini cha
kuporomoka kwa mgodi huo unaendelea na hadi kesho utakuwa umekamilika na kujulikana chanzo cha wachimbaji
hao kufunikwa.
“Kuna watu wanasema mgodi umefungwa, si
sahihi kusema hivyo, mgodi haujafungwa, kilichopo ni uchunguzi ambao unafanyika
kwa siku tano, baada ya hapo shughuli zitaendelea kama kawaida,” alisema.
Akizungumzia wachimbaji hao 15 kupelekwa
hospitali na kukaa kwa muda mfupi, jambo lililosababisha baadhi ya ndugu zao
kulalamika, alisema walipelekwa kwa mapumziko kidogo, kwani hali zao zilikuwa
nzuri.
“Tulivyowatoa hospitali mapema ndugu
walilamika kwa nini wamekaa muda mfupi. Hawa ndugu zetu hawakuwa na tatizo la
kiafya, lakini kwa kuwa walikuwa chini ya ardhi mazingira ambayo ni tofauti na
huku, walihitaji mapumziko na uangalizi kidogo,” alisema Kyunga.
Taarifa ambazo gazeti hili linazo ni
kwamba huenda wachimbaji hao wakapewa mikataba ya mwaka mmoja mmoja tofauti na
awali ambapo taratibu za baadhi ya migodi hutoa miezi mitatu mitatu kwa
watumishi wao.
Novemba mwaka juzi, watu watano
waliokolewa wakiwa hai baada ya kufukiwa na kifusi kwa siku 41 kwenye mgodi wa
Nyangarata wilayani Kahama, Shinyanga.
0 comments:
Post a Comment