WASHINGTON, D.C., Marekani
Barack Obama |
RAIS mstaafu Barack Obama ameibuka na
kuzungumzia siasa ikiwa ni mara ya kwanza tangu astaafu urais – akiunga mkono
maandamano yanayosambaa nchini kote kupinga agizo la Rais Donald Trump kuhusu
uhamiaji.
“Rais Obama amesikitishwa na kiwango cha
matukio yanayotokea hivi sasa kwenye jamii mbalimbali nchini,” kwa mujibu wa
taarifa iliyotolewa na ofisi yake ya rais mstaafu.
“Wananchi kutekeleza haki yao ya
kikatiba ya kukusanyika, kuandaa na kufanya sauti zao zisikike na maofisa
waliochaguliwa, ndicho hasa tunachotarajia kukiona pale maadili ya Marekani
yanapokuwa matatizoni,” alisema Obama.
Hata hivyo, Rais huyo mstaafu hakuingia
ndani zaidi kuhusu matamko ya Trump – yakiwamo ya kuzuia ruhusa ya wakimbizi
kuingia nchini na kusimamisha uhamiaji wa watu kutoka nchi saba duniani
zikiwamo Iraq na Syria.
Badala yake, Obama ambaye ana haki ya
kuingilia kati pale mambo ya kisiasa na hasa ‘masuala nyeti’ yanapokuwa
hatarini, aliomba “kulinganishwa kwa uamuzi wa sera zake za nje na za Trump.”
“Kwa kuzingatia mlinganisho na uamuzi wa
sera za nje za Rais Obama, kama tulivyosikia kabla, kimsingi rais hakubaliani
na suala la ubaguzi dhidi ya watu kwa sababu ya imani yao au dini,” kwa mujibu
wa taarifa.
Katika mkutano wake wa mwisho na
waandishi wa habari, Obama alisema anaweza kuingilia “nyakati fulani wakati
anapokuwa anadhani kwamba maadili yetu ya msingi yamo hatarini.
Obama kwa kiasi kikubwa alishambulia moja
kwa moja kauli ya Rais Trump: kwamba “Sera yangu ni sawa na alichokifanya Rais
Obama mwaka 2011 alipopiga marufuku viza kwa wakimbizi kutoka Iraq kwa miezi
sita.”
Gazeti la Washington Post lilielezea
kauli hiyo kama madai yasiyo na kichwa wala miguu, “kwa sababu utawala wa Obama
haukupata kuzuia Wairaqi kuingia nchini. Utawala huo ulibana uingiaji wa
Wairaqi nchini mwaka 2011 wakati ilitangaza majina yaliyokuwa kwenye kanzidata
ya nchi, baada ya Mwiraqi ambaye alikuiwa na hifadhi nchini, kubainika kuwa alipata
kutega mabomu barabarani nchini mwake”.
Hata hivyo, msaidizi wa Obama hakujibu
swali la alikokuwa Rais huyo mstaafu wakati akitoa taarifa yake hiyo.
Sehemu ya mwisho inayojulikana kwamba ndiko
alikuwa ni kisiwa cha Necker, kinachomilikiwa na bilionea Mwingereza, Richard
Branson karibu na visiwa vya British Virgin.
Msemaji wa Ikulu ya White House, Sean
Spicer hakujibu maswali mengi katika mkutano wake wa kila siku na waandishi wa
habari, juu ya taarifa hiyo ya Obama, ambayo ilimfikia mara alipoanza kuzungumza
na waandishi hao.
Obama alisema kwenye mkutano wake wa mwisho
na waandishi wa habari akiwa Ikulu, kwamba wakati akipanga kukaa pembeni katika
miaka ya utawala wa Trump, bado atakuwa na haki ya kuwa mtetezi “wakati ambao
anadhani maadili yetu ya msingi yanakuwa kwenye hatari.”
Obama alijiweka katika “juhudi za
kulinda watoto ambao wamekulia hapa na kwa vyovyote vile ni watoto wa
kimarekani, hivyo haipendezi kuwapeleka kwingineko wakati wanaipenda nchi hii.
“Ni marafiki wa watoto wetu na wenzao walionao
madarasani na hivi sasa wanaingia kwenye vyuo vya jumuiya au, katika matukio
mengine, wanahudumia kwenye Jeshi letu,” Rais huyo alisema.
“Fikra kwamba tunaweza kufanya hivi kinyemela,
au kwa sababu ya kisiasa, kuadhibu watoto ambao hawajafanya lolote baya, nadhani
litakuwa jambo ambalo inafaa kulisemea.”
Kwa wiki mbili mfululizo, waandamanaji
wamekusanyika Washington, D.C. na majiji mengine kupinga hatua za Trump.
Upinzani wa chama cha Democratic unaendelea
kujipanga. Kiongozi wa Democratic ndani ya Bunge la Seneti, Charles Schumer juzi
alipandisha jazba kwenye mkutano na waandishi wa habari akiwa na wakimbizi wa
Syria wakipinga agizo la Trump. Hata hivyo Trump alimkejeli Schumer juzi kwa
kujifuta “machozi bandia”.
“Nani kocha wake wa kuigiza?” Trump
aliuliza.
Obama alipinga sera yoyote ya uhamiaji inayobagua
kidini katikati ya Novemba mwaka jana baada ya Democrats kupoteza Ikulu.
“Na hivyo tunapaswa, kila mmoja wetu,
kutimiza wajibu wetu. Na Marekani inapaswa kutimiza wajibu wake. Na
nitakaposikia watu wanasema hivyo, sawa, yawezekana tutapaswa kuwakubali
Wakristo lakini si Waislamu; ninaposikia viongozi wa kisiasa wanapendekeza
kwamba kutakuwa na kipimo cha udini kama kigezo cha kumpokea mtu anayekimbia
vita nchini mwake, wakati baadhi ya watu hao wanatoka familia zilizonufaika na ulinzi
walipokimbia vurugu za kisiasa – ni aibu,” alisema.
“Huo si umarekani. Hivyo sivyo tulivyo.
Hatuna vipimo vya udini kwa ajili ya kuonesha huruma yetu.”
Amri ya Trump inahusu nchi saba, karibu
zote za kiislamu, lakini zinawaacha wanaoteseka kutokana na ubaguzi wa kidini.
Trump katika kutetea sera hiyo anawaombea Wakristo wauawe na ISIS nchini Syria
na Iraqi.
Wakati
huo huo, Rais Trump amemfuta kazi Kaimu Mwanasheria
Mkuu wa Serikali baada ya kukataa kutetea amri yake tata kuhusu uhamiaji.
Mkurugenzi wa Uhamiaji na Forodha,
Daniel Rogsdale naye alifutwa kazi saa mbili baadaye bila maelezo yoyote.
Kaimu Mwanasheria Mkuu, Sally Yates,
mteule wa Democratic, alikuwa akituhumiwa kwa ‘kuisaliti’ Marekani, baada ya
kuelekeza wanasheria wa Wizara ya Sheria kuacha kutetea kinachoitwa ‘Marufuku
ya Uislamu’ ya Trump juzi. Alisema hakuwa anaridhishwa na amri hiyo ambayo inapingana
na sheria.
Dana Boente aliapishwa kukaimu nafasi
hiyo juzi saa 3 usiku katika hafla iliyoandaliwa haraka haraka baada ya Trump
kumtimua mtangulizi wake. Baada ya kuapishwa, Boente naye haraka haraka
akaelekeza Wizara ya Sheria kutetea amri hiyo ya Trump.
Katika hatua nyingine, Thomas Hooman
ameteuliwa kujaza nafasi ya Rogsdale ya Mkurugenzi wa Uhamiaji na Forodha.
0 comments:
Post a Comment