Grace Gurisha
MAHAKAMA Kuu Kitengo cha Biashara, leo inatarajia kutoa
uamuzi kama itamwita Mwenyekiti wa Kampuni za IPP, Dk Reginald Mengi kwenda
kuulizwa maswali kutokana na kiapo alichojieleza kwa nini asifungwe jela kwa
kushindwa kutekeleza hukumu ya kulipa dola 598,750 za Marekani sawa na Sh
bilioni 1.2 au la.
Malipo hayo ni ya wafanyabiashara watatu; Muganyizi
Lutagwaba, Eric Mshauri na Charles Mgweo, kutokana na mgogoro unaohusu malipo
ya uuzaji hisa kwenye kampuni ya Douglas Lake Minerals Ltd, ambayo kwa sasa
inaitwa Handeni Gold Inc.
Mahakama hiyo ilifikia hatua hiyo jana, baada ya Wakili
wa wafanyabiashara hao, Mafuru Mafuru kuomba Dk Mengi afike mahakamani ili aulizwe
maswali yanayotokana na kiapo chake, lakini Wakili wa Mwenyekiti huyo,
Deogratias Ringia alipinga mteja wake kuitwa mahakamani hapo.
Kutokana na mabishano hayo, Jaji Amir Mruma alisema
uamuzi huo atautoa leo saa 3:30 asubuhi. Katika kiapo kinzani cha Mwenyekiti
huyo kuna maombi aliyawasilisha mahakamani hapo akiomba kuongezwa muda wa
kukata rufaa kupinga hukumu iliyotolewa.
Hata hivyo, Ringia aliwasilisha pingamizi la awali la
kisheria dhidi ya hukumu iliyotolewa na Mahakama ikimwamuru Dk Mengi alipe
fedha hizo kutokana na alichodai kuwa hukumu ilikuwa na kasoro za kisheria, kwa
sababu haikusainiwa na pia hakuna maombi sahihi ya kisheria waliyoomba ya kutiwa
hatiani.
Baada ya Ringia kuwasilisha pingamizi hilo, Jaji Mruma
alisema litaamuriwa kwa maandishi, hapo hapo akatoa maelezo kuwa majumuisho ya kwa
nini Dk Mengi asifungwe yataendeshwa kwa pamoja kwa njia ya maandishi.
Wakili Mafuru alipinga na kudai kuwa ni jambo ambalo
haliwezekani, kwa sababu pingamizi linatakiwa kwanza litolewe ufumbuzi ndipo
masuala mengine yaendelee, kwa hiyo akataka
mambo hayo mawili yatenganishwe, na hilo nalo Mahakama italitolea uamuzi.
Kesi hiyo inatarajiwa kusikilizwa na Jaji Amir Mruma,
ambapo awali katika uamuzi wake, alikubali Dk Mengi atoe maelezo yake kwa kiapo
huku akitoa siku saba kwa Mwenyekiti huyo kukamilisha hilo.
Awali, katika uamuzi wa Jaji Mruma alisema kama kiapo
kinzani kitaacha maswali mengi, basi nafasi
ya Dk Mengi kuitwa mahakamani itakuwapo.
Hatua hiyo ya Mahakama inatokana na wafanyabiashara hao
kuwasilisha maombi kuitaka Mahakama ikazie hukumu hiyo ya Januari 28.
Kesi hiyo iliyofunguliwa na wafanyabiashara hao
ilisikilizwa na Jaji Agathon Nchimbi huku Dk Mengi na kampuni ya K.M.
Prospecting Limited wakiwa walalamikiwa.
Hati ya kiapo cha pamoja cha wafanyabiashara hao,
ilieleza kuwa walifungua shauri kwenye
Mahakama hiyo wakidai malipo, ambapo juhudi kama hizo zilifanyika pia na Kampuni ya K.M. Prospecting zikashindikana
kwa kuwa mali na akaunti zake za benki hazijulikani ziliko.
0 comments:
Post a Comment