Dotto Mwaibale
Mussa Mlawa |
VIJANA zaidi ya 250 wamejiunga na klabu
za kupinga ukatili wa kijinsia katika masoko ya Ilala Boma, Mchikichini na
Temeke Sterio, Dar es Salaam.
Mchakato wa kujiunga na klabu hizo ulitokana
na mafunzo waliyopata kutoka kwa wawezeshaji sheria wa Shirika la Equality for
Growth (EfG) waliyotoa kwa nyakati tofauti katika masoko hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari
mwishoni mwa wiki, Mratibu wa Mradi wa kufungua klabu za mabadiliko katika
masoko hayo ambaye pia ni Mwanasheria wa Shirika hilo, Mussa Mlawa, alisema
mwitiko wa vijana kujiunga na klabu hizo ni mkubwa mno.
"Hatukutarajia kama mwitiko wa
vijana wa kujiunga na klabu hizi ungekuwa mkubwa kiasi hiki," alisema
Mlawa.
Alisema changamoto kubwa waliyokuwa nayo
ni kwenye soko la Ilala Boma kutokana na ukubwa wake, lakini ndilo liliongoza
kwa vijana kujitokeza kwa wingi kuanzia mtu mmoja hadi vikundi.
Alisema mradi huo unafanyika kwa
usimamizi wa Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake Tanzania (WLAC) kupitia
kampeni ya Tunaweza ambapo EfG wanaiendesha kwenye masoko matano jijini Dar es Salaam ambayo ni Ilala
Boma, Ferry, Mchikichini, Temeke Sterio na Buguruni.
Mlawa alisema vijana hao zaidi ya 250
walijitokeza kujiunga na klabu hizo kutoka masoko ya Temeke Sterio, Mchikichini
na Ilala Boma ambapo wataendelea na mchakato huo katika masoko ya Buguruni na
Ferry.
0 comments:
Post a Comment