Mary Mtuka
JESHI la Polisi kwa kushirikiana na
Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), linashikilia watu 17 kwa tuhuma za kupiga mawe injini
ya treni na mabehewa na kusababisha uharibifu na hasara kwa Shirika.
Watu hao walikamatwa kutokana na tukio
la watumiaji usafiri huo wa treni kutoka Stesheni Dar es Salaam kwenda Pugu
kuvunja vioo vya madirisha kwa mawe.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Kamanda
wa Polisi Reli, Simon Cillery alisema watu hao walikamatwa juzi baada ya tukio
hilo na uchunguzi unaendelea ili wafikishwe mahakamani kwa tuhuma za kuhusika
na uharibifu wa miundombinu ya reli.
Alisema Novemba 7 saa mbili usiku eneo
la Kalakata baadhi ya watu walipiga mawe treni na kuharibu miundombinu baada ya
kuambiwa kuwapo tatizo la usafiri kutokana na treni ya mizigo kupinduka eneo la
Pugu na hivyo kufanya usafiri huo kutofuata ratiba yake ya kawaida.
Alisema cha kushangaza licha ya wahusika
wa TRL kutoa taarifa, watu wachache walifanya vurugu kwa kurusha mawe na
matokeo yake kuharibu miundombinu ya usafiri huo.
"Baada ya watu hao kufanya vurugu,
tuliendesha msako na kuwakamata 17 ambao uchunguzi dhidi yao unaendelea," alisema
Chillery.
Kamanda alisema ni vema wananchi
wanapopewa taarifa kuwa usafiri huo una tatizo wavumilie na akahoji mbona
kwenye usafiri wa daladala kuna wakati wanakaa hadi saa tatu na hakuna vurugu
wanazofanya.
Alitoa mwito kwa wananchi kuwa walinzi
wa mali ya umma na kuwa sehemu ya wasamaria wema kwa kutoa taarifa pindi
wanapoona baadhi ya watu wanaharibu miundombinu ya reli hiyo ambayo inatumia
gharama kubwa kuijenga na kuikarabati.
Awali akitoa taarifa ya kuharibiwa kwa
miundombinu hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa TRL, Masanja Kadogosa alisema kitendo
hicho ni uvunjifu wa sheria na kinahatarisha amani na usalama wa watumiaji wa
usafiri huo.
"Uongozi wa TRL umeshauri watumiaji
wa treni za Jiji kufuata sheria, taratibu za kutoka kituo cha Dar es Salaam
kwenda Ubungo Maziwa na Pugu," alisema.
Alitaja baadhi ya maeneo ambayo
yamekithiri na matukio ya uharibifu wa miundombinu ya treni kuwa ni Gongo la
Mboto na Karakata.
0 comments:
Post a Comment