Joyce Kasiki, Dodoma
MRADI wa ujenzi wa Mji wa Kisasa wa
Kigamboni (Dege Eco Village) umesimama kutokana na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii
(NSSF) kukosa namna bora ya kugharimia mradi huo wenye wabia wawili.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Hesabu za Serikali (PAC), Naghenjwa Kaboyoka alisema jana kuwa pamoja na
majadiliano na wakaguzi wa hesabu, Bodi na Menejimenti ya NSSF na Msajili wa
Hazina, Kamati imeshauri suala hilo kufanyiwa uchambuzi na uhakiki kabla ya kuhitimishwa.
“Katika taarifa ya ukaguzi ya NSSF, jambo
mahsusi la msisitizo lilihusu utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Kigamboni
Satellite Village,” alisema Kaboyoka.
Kwa mujibu wa hoja ya CAG, makubaliano yalionesha
kuwa NSSF watakuwa na hisa asilimia 45 na Azimio Housing Estates (AHEL) asilimia
55 kwenye mradi huo.
“Aidha, AHEL walitakiwa kutoa ardhi ya
ekari 20,000 ambayo itakuwa sawa na asilimia 20 ya hisa zao na asilimia 35
watachangia kwa kutoa fedha, NSSF walitakiwa kuchangia asilimia 45 ya hisa zao
katika mradi kwa kutoa fedha,” alisema.
Kaboyoka aliongeza kuwa Kamati iliamua
kuunda kamati ndogo ambayo itajikita katika kupata welewa wa dhana, dhima na
maudhui ya uwekezaji wa mtaji kwenye miradi ya ujenzi kwa makubaliano ya kutoa
ardhi ili kubainisha vigezo vinavyokubalika katika utekelezaji wa miradi kwa
njia hiyo.
Vile vile alisema lengo la kuundwa kwa Kamati
hiyo ni kuthibitisha iwapo ekari 19,700 zilizotakiwa kuchangiwa katika mradi
huo zipo, kupitia makubaliano ya mkataba wa ugharimiaji wa mradi huo na
mgawanyo wa hisa, kupitia taarifa ya utekelezaji wa mradi na kufanya ulinganifu
wa utekelezaji wa mradi huo na miradi mingine iliyotekelezwa na mashirika ya umma.
“Hoja ya Kamati katika jambo hili ni
kuwa kunahitajika uchambuzi wa kina na taarifa za kutosha kuhusu utekelezaji wa
miradi ya ‘Land for equity‘ kama alivyoibua CAG, ikizingatiwa hoja mahsusi ya
ukaguzi ilihusu suala la ardhi ambayo CAG anahitaji NSSF wajiridhishe iwapo
mbia mwenza anamiliki,” alisema.
Aliongeza
kuwa bado kuna masuala yanahitaji majibu kabla ya kufikia uamuzi wa mwisho na
kwamba kamati itakuwa katika nafasi nzuri ya kulitolea taarifa jambo hilo,
baada ya kukamilika kwa uchambuzi wa kitaalamu wa hoja husika ya ukaguzi utakaofanyiwa
kazi na kamati ndogo.
0 comments:
Post a Comment